Ni mwishoni mwa mwaka jana nilipata mawasiliano ya jamaa yangu tuliyepotezana kwa takriban miaka mitano, nakumbuka mara ya mwisho kuonana naye ni 2016 baada ya mimi kurejea toka kwenye majukumu nje ya nchi, kiukweli kiuchumi alikuwa ameyumba nilimuuliza sasa jamaa yangu una mpango gani kujikwamua kimaisha?
Akanijibu rafiki yangu sina ramani yoyote ila ningepata kama M 1 ningejua nini cha kufanya, kwa vile nilisota nae sana mimi nikampa cash milioni moja alishukuru mara mbilimbili hakuamini. Tangu siku hiyo hatukuonana tena sababu mimi nilirudi kwenye kituo changu cha kazi na yeye aliendelea na mishe zake.
Hivi karibuni nilipata taarifa zake kutoka kwa ndugu yake kwamba ni mmiliki wa mgodi wa madini aina ya ruby huko Mahenge, baada ya kupata taarifa hizo na mawasiliano yake, nilimtafuta kwa njia ya simu alipopokea akauliza nani?
Nikamjibu mimi ni fulani loh! jamaa alifurahi sana sana, akanitamkia aisee rafiki yangu wewe ndio umenifanya niheshimike na kuonekana mtu, ile milioni moja ulionipa kwa kweli imebadilisha maisha yangu kabisa, uliponipa nikakimbilia Mahenge baada ya kusikia kuna madini ya ruby green na red.
Baada ya kufika kwenye eneo husika nilitulia kwa mwezi mzima nikisoma mazingira na kuona jinsi shughuli zinavyofanyika, baadae nilianza kwa kununua madini hayo kwa wachimbaji wadogo wadogo, na sasa hivi nimekuwa mmiliki wa mgodi na ninasafiri hadi Thailand na nchi zingine kupeka mzigo.
Namshukuru Mungu kwa kukugusa wewe na kunipa ile milioni moja ambayo imezaa mamilioni ya fedha.Tafadhali ukipata nafasi rafiki yangu nitembelee uje uone maendeleo niliyoyapata, na nakuandalia donge nono kwa sababu kama sio wewe mimi sijui ningekuwa katika hali gani. Ndio najipanga nikipata likizo nimtembelee mshkaji.