Wakati umefika wa kuwachapa viboko viongozi wazembe

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,023
Salehe Mohamed

Tuanze kuwachapa viboko viongozi
Tanzania Daima~Sauti ya watu

JANA katika vyombo mbalimbali vya habari kulikuwa na taarifa kuwa Mkuu wa Wilaya Bukoba, Albert Mnali, ameamuru polisi kuwachapa viboko walimu wa wilaya hiyo kwa kosa la uzembe kazini.

Kwa mujibu wa taarifa hizo uzembe anaousema DC huyo ni kuchelewa kufika kazini, kutofundisha kwa kiwango kinachotakiwa, jambo lililofanya wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika mtihani wa darasa la saba. Walimu hao wapatao 32 kila mmoja alichapwa viboko viwili.

Kwa mtazamo wangu huu ni udhalilishaji na uoneve ni lazima DC aliyehusika awajibishwe kwa kufanya kituko hicho. Ni ajabu kwa kiongozi mwenye dhamana kubwa kufikiria zaidi kuwa matokeo mabaya ya wanafunzi wa darasa la saba, husababishwa na uchelewaji wa walimu shuleni au kutofundisha vizuri.

Walimu hivi sasa wanaishi katika mazingira magumu, hawana mishahara ya kutosha, nyumba, miundombinu mibovu na matatizo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na serikali ndiyo maana hata ufundishaji wao hauridhishi.

Ni ukweli usiopingika kuwa walimu wa shule binafsi wamekuwa wakifanya vizuri zaidi kwa sababu ya mishahara mizuri, nyumba, usafiri na mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Kama kweli kuwachapa viboko walimu hao ndiyo njia nzuri ya kutaka wafanikiwe, basi ni vema na utaratibu huo sasa uukageukia kwa wanasiasa ambao wamekuwa wakilipwa posho nono zaidi lakini wameshindwa kutimiza ahadi walizozitoa!

Hii leo tuanzie viongozi wa juu wa serikali kuanzia kwa Rais, Mawaziri, Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa na wakuu wa wilaya ambao wameshindwa kuleta maisha bora waliyoyaahidi kwa kila Mtanzania - barabara, hospitali shule na huduma nyingine ni mbovu kupita kiasi lakini kila kukicha viongozi wetu wamekuwa wakitumia mamilioni ya fedha katika mambo yasiyo na manufaa kwa taifa lakini bado hatujawachapa viboko hadi sasa.

Kwa nini tusiwachape viboko wabunge wetu ambao kila kukicha wamekuwa wakipigania kuongezwa kwa maslahi yao bila kujali fedha hizo ndizo zinazotolewa na wananchi wenye vipato duni vinavyotokana na kuuza mifugo au mazao yao?


Kama kweli tuna nia ya dhati ya kuboresha elimu kwa nini tusimchape viboko Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, ambaye kwa miaka miwili sasa viwango vya kufaulu kwa wanafunzi vinashuka pamoja na shule za sekondori za serikali zimekuwa zikipata matokeo mabaya kulinganisha na za binafsi.

Kwa nini tusimchape viboko Mkuu wa Baraza la mitihani la Taifa kwa mitihani kuvuja kabla ya kufanywa, lakini pia tusiache kuwachapa viboko na watendaji wa baraza hilo kwa kutengeneza vyeti bandia na kuziuza kwa gharama ndogo? Hawa si ndiyo wanoshusha kiwango cha elimu? Kwa nini tusiwachape watendaji wa wizara ya elimu kwa kuanzisha mafunzo ya muda mfupi kwa walimu ‘Voda Vasta' ambao tuna uhakika hata ufundishaji wao si bora.

Binafsi nafurahia mfumo wa kuanza kuchapana viboko lakini ni vema ukaanzia katika ngazi za juu ambako ndiko kwenye maafa zaidi kuliko ngazi za chini ambazo kwa kiasi kikubwa huathiriwa na mfumo mbaya wa uongozi wa juu.

Tungeweza kuwachapa viboko kina Lowassa, Hosea, Karamagi na Msabaha kwa kuiingiza nchi katika mkataba wa Richmond ambao ulilifanya taifa kulipa sh milioni 152 kwa siku hapo ningefurahi, tungeweza kumchapa Mramba kwa kununua ndege ya rais yenye thamani ya bil 40 huku wananchi wakifa na njaa tena kwa kuwalazimisha wale majani hapo ningeunga mkono uchapaji viboko.

Nani atayeweza kufanya kazi kama hajui atakaa wapi, familia yake itakula nini, ataishi vipi na huduma nyinginezo za muhimu? Viongozi wana uhakika na maisha yao, kwani wanakaa kwenye nyumba nzuri, marupurupu mazuri, wanasomesha watoto zao shule za kimataifa na wengine wanawapeleka nje ya nchi, wanatibiwa nje ya nchi sasa kwa nini washindwe kufanya kazi vizuri hasa kwa kutimiza ahadi walizozitoa? Nani asiyejua hivi sasa uongozi ni biashara?

Mbunge anayekaa madarakani kwa muda wa miaka mitano hupata sh milioni 30, gari na posho nono za kila kikao anashindwaje kuisimamia serikali kuwapelekea wananchi maendeleo?

Hawa ndiyo wa kuchapwa viboko kwani wana ‘maisha bora', lakini hawana moyo wa kufanya kazi, walimu wana moyo wa kufanya kazi lakini hawana maisha bora watawezaje kutekeleza wajibu wao kwa taifa?


Tatizo la nchi hii ni viongozi kutokuwa makini na kusimamia wajibu wao, inawezekanje sekta ya elimu isipewe kipaumbele kinachotakiwa na badala yake fedha nyingi zinaishia kwa wajanja wachache kwa kununua magari ya kifahari pamoja na kuandaa warsha za ujanjauujanja?

Kama tusipokuwa makini ipo siku tutaanza kupigana risasi hadharani kwa kushindwa kutimiza wajibu, kwani itafika wakati tutaona viboko havifai.
 
Back
Top Bottom