Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,880
- 3,168
Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kuacha kusubiri Serikali itangaze miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), badala yake waibue fursa na kuwasilisha mapendekezo yao kwa Serikali.
Kafulila ametoa kauli hiyo leo, Septemba 25, 2026, wakati wa Kongamano la Fursa na Uwekezaji kuhusu PPP lililofanyika Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania kujenga uchumi wa dola trilioni moja, akisisitiza kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufikia lengo hilo.
“Wawekezaji mjiandae, mtambue maeneo yenye fursa, mshirikiane na mamlaka za Serikali na mweleze nia yenu ya kuwekeza, bila kusubiri Serikali iandae mradi na kuutangaza,” amesema.
Kafulila amesema Tanzania ina uwezo wa kufikia uchumi wa kiwango hicho, ambacho kimefikiwa na nchi 21 pekee duniani, lakini akasisitiza umuhimu wa kubadili mtazamo na namna Serikali na sekta binafsi zinavyoshirikiana katika kukuza uchumi.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 si mpango wa Serikali au Rais Samia Suluhu Hassan pekee, bali ni dira ya Watanzania wote, huku sekta binafsi ikiwa mhimili muhimu katika utekelezaji wake.
“Kazi ya Mkurugenzi wa Halmashauri au Mkuu wa Wilaya si kutawala watu tu. Ni kuwa-engage na kuwashirikisha katika biashara na uchumi,” amesema.
Ametaja Mkoa wa Pwani kuwa eneo la kimkakati kwa uwekezaji kutokana na fursa zilizopo, akiwataka wafanyabiashara na wawekezaji kuzitumia kwa kushirikiana na Serikali ili kuchochea utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katika kongamano hilo, wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani pia wameeleza umuhimu wa kutumia maeneo ya kimkakati yaliyopo Mkoa wa Pwani katika kukuza biashara na uwekezaji kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.