Kumekuwa na mitazamo tofauti toka sakata la mjadala wa mavazi kwa wabunge hususani kwa wabunge wa jinsia ya kike kuibuliwa bungeni. Kila upande umekuwa ukitengeneza hoja ili kujenga uhalali. Kwa muono mpana, hili jambo halitakaa liishe leo wala kesho, litaendelea kuibuka kila mara.
Kwa mtazamo wangu, suluhisho sahihi na kamili ni wabunge kuvalishwa mavazi rasmi yenye kufanana (uniform), na kwa hilo ninapendekeza majoho mahususi yashonwe na wabunge wavalishwe kila wanapoingia kwenye vikao vya bunge na kamati. Suala la vazi gani avae mbunge akitaka kuingia bungeni liwe ni jukumu la bunge na sio jukumu la mbunge!
Na sababu zangu ni hizi.
1. Huwezi ukawafuatilia kwa haki na kuwadhibiti wabunge zaidi ya mia tatu kimavazi kila wanapoingia bungeni ikiwa kila mbunge anaweza kuvaa chochote wakati wowote akiingia bungeni.
2. Huwezi kuwa na viwango (standard) zenye kuweza kuwaridhisha wabunge zaidi ya mia tatu kila wanapotaka kuingia bungeni ikiwa kila mmoja ana uhuru wa kuvaa chochote anachokitaka.
3. Tafsiri ya mavazi yenye staha dhidi ya mavazi yasiyo na staha haina maana yoyote katika jamii yenye mitazamo mchanganyiko kuhusu imani, mila, tamaduni, jinsia, rika na mitindo ya kimaisha.