LICHA ya wabunge waliomaliza muda wao baada ya Bunge kuvunjwa kulipwa kiinua mgongo kipatacho Sh milioni 43 kila mmoja na baadhi yao kuacha kutetea nafasi hiyo, imebainika bado wamekuwa wakiendelea kulipwa mshahara na posho kila mwezi.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, alithibitisha jana kuwa wabunge hao wanaendelea kulipwa mishahara na posho mbalimbali na wanastahili kulipwa wakati huu ambao Bunge limevunjwa na Rais.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanadai kuwa kitendo cha mbunge kulipwa mshahara na posho hizo, kinaweza kumfanya akazitumia fedha hizo kuwalaghai wapiga kura wakati wapinzani wake hawana uwezo wa kufanya hivyo kutokana na ufinyu wa rasilimali uliopo.
Dk. Kashilillah alipotakiwa kueleza kwa kina kwa nini wabunge wanastahili kulipwa wakati tayari Bunge limeshavunjwa alisema, wanaowalipa wabunge ni Hazina kwa hiyo ndio wenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo.
Alisisitiza kuwa kama ni masuala ya sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ndiye yuko kwenye nafasi nzuri ya kuyafafanua na kuongeza, nakushauri uwasiliane na AG atakufafanulia vizuri.
Rais Jakaya Kikwete kupitia gazeti la Serikali toleo namba 272 la Julai 28, alitoa tamko la kulivunja Bunge kuanzia Agosti mosi siku chache kabla ya uteuzi wa wagombea udiwani, ubunge na urais kufanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Baada ya tangazo hilo, majimbo yote yalikuwa wazi hivyo kutoa fursa ya Watanzania wenye sifa kujitokeza kugombea ubunge kupitia vyama mbalimbali vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu.
Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema alipoulizwa alisema Katiba ya nchi inatamka kuwa uhai wa Bunge ni miezi 60 hivyo wabunge wanastahili kulipwa mishahara kwa kipindi hicho kilichotajwa kwenye Katiba.
Mishahara kwa wabunge ni lazima iendelee kulipwa na huu sio ufisadi, alisema Jaji Werema na kuongeza kuwa, Wanalipwa kwa vile bado wanafanya kazi katika maeneo yao.
Alipoulizwa kwa nini walipwe mishahara wakati tayari shughuli za Bunge zimeshakoma alisema,hiyo ni advantage (faida) kwao kwani malipo hayo yanatambulika kisheria.
Unakuta watu wanalalamika eti kwa nini Rais anatumia magari ya Serikali, ni lazima atumie kwa kuwa yuko madarakani na hiyo ndio advantage yake, alisema Jaji Werema.
Aliongeza kuwa sheria nyingine inayowafanya wabunge waendelea kulipwa mishahara ni Sheria ya Maslahi ya Wabunge ambayo inaeleza kuwa ubunge unakoma baada ya kulitumikia Bunge kwa miezi 60.
Mwanasheria huyo alisema kibaya ni kwa Wabunge hao kutumia mishahara hiyo kuwarubuni wapiga kura ili wamchague tena.
Kama kuna wabunge wanaofanya hivyo tutaarifuni kwa kuwa watakuwa wanakiuka sheria.
Mbunge mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alikiri kuwa wanaendelea kupokea mshahara wao kila mwezi wa Sh milioni mbili na Sh milioni tano ambazo wanalipwa kama posho za jimbo.
Licha ya malipo hayo, mbunge huyo alisema wabunge pia hulipwa posho za mafuta ambayo ni lita 70 kila wiki.
Kutokana na wabunge kupata mishahara na marupurupu, kazi hiyo imevutia watu wengi wakiwemo wasomi wanaofundisha katika vyuo vikuu ambao mara nyingi wamekuwa tayari kuacha kazi zao na kugombea ubunge.
Kabla ya Rais kulivunja Bunge, Hazina iliwalipa wabunge hao mafao yasiyopungua Sh milioni 43 kila mbunge ikiwa ni asilimia 40 ya mshahara wa mbunge huyo aliyelitumikia Bunge kwa miaka mitano.
Source: Habari Leo