Waandishi binafsi wa Vitabu vya ziada Mashuleni, watakiwa kufuata muongozo

pantheraleo

JF-Expert Member
Jan 5, 2013
691
878
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt Aneth Komba amewaelekeza waandishi binafsi wa machapisho mbalimbali yenye lengo la kutumika shuleni katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari waandike vitabu kwa kufuata mwongozo wa uandishi wa vitabu vya ziada.

Akieleza haya leo mapema katika mkutano wa waandishi binafsi na TET uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TET alisema, waandishi binafsi wanapaswa kuandika machapisho yenye lengo la kutumika shuleni kwa kufuata mwongozo uliotolewa na TET ili kurahisisha na kuharakisha mchakato wa ithibati.

“Lengo la Serikali ni kumpatia mtoto elimu bora, hivyo waandishi wa vitabu mnatakiwa kuandika vitabu vinavyofuata muongozo wa uandishi ulioandaliwa na TET, mlete vitabu vipitiwe na kuweza kupata ithibati ya kutumika shuleni. TET inashirikiana na itaendelea kushirikiana na waandishi binafsi katika kufanya kazi pamoja ili kupata kitabu bora, hivyo waandishi binafsi msijione kama ni maadui wa TET”, alisema.

Awali alisema, TET imeimarisha kitengo cha uthibiti ubora wa machapisho,hivyo waandishi walete machapisho kwenye kitengo na kitengo kitahakikisha kinapitia kwa wakati kwa kufuata hatua zote muhimu za uthibiti ubora.

Aidha waandishi binafsi wameiomba TET kuangalia upya suala la muda katika mchakato wa uthibiti wa machapisho.Walisema, mchakato wa ithibati unakua mrefu na hivyo kusababisha vitabu vya ziada kuchelewa kupata ithibati ya kutumika shuleni.

Pamoja na kutambua juhudi za maboresho zinazofanywa na TET pia waliomba kitengo cha uthibiti ubora kiweze kuwa na muda wa majadiliano ya moja kwa moja ili kuweza kujadiliana na kukubaliana baadhi ya marekebisho ili kurahisisha kazi.

Naye Mwenyekiti wa umoja wa waandishi binafsi Gabriel Kitua alishukuru TET kwa kushirikiana na waandishi binafsi katika kurekebisha kazi zao za uandishi na aliwaomba waandishi walete kazi zao ziweze kupitiwa na kuweza kupata ithibati ya kutumika shuleni.

Imetolewa na ;
Afisa Habari TET
Dorothy Natale
 
Back
Top Bottom