Unajua nimekuja kuhitimisha kuwa sisi Watanzania tuko ‘soft’ sana, hususan nyakati hizi.
Unakuta mtu ana likitambi lake likubwa tu halafu eti analalamika vyuma vimekaza.
Watu wanakula bata kila kona huku wanalalamika vyuma vimekaza.
Wakati mwingine huwa nikiwaangalia naishia kucheka na kuwaambia ‘mnacheza nyie’.
Wahenga wenzangu watakubaliana nami kuwa kuna kipindi nchi hii vyuma vilikaza kweli kweli.
Enzi za miaka ya 80, hususan mwanzoni hadi katikati.
Enzi za maduka ya ugawaji. Watu mnajipanga mstari kusubiri kununua bidhaa kama sukari, unga, mafuta, mchele, miche ya sabuni, na vitu vinginevyo.
Bidhaa hizo za kila siku zilikuwa adimu. Sabuni za kuogea kama vile Imperial Lather na Palmolive zilikuwa hazipatikani kirahisi nchini. Kuzipata ilibidi mtu aende nje ya nchi kama Kenya au Ulaya huko. Watu tulikuwa tunaogea sabuni za Mbuni. Sabuni hiyo hiyo unaoshea vyombo, hiyo hiyo unaogea na hiyo hiyo unafulia nguo.
Hata dawa za mswaki zilikuwa adimu. Kunywa hata soda lilikuwa ni jambo la anasa. Watu mnaweza kupitisha hata miezi sita hamjanywa soda. Hata kula mkate wa siha ilikuwa nadra.
Kula pilau nako hivyo hivyo. Kula kuku pia.
Kunywa bia ndo kabisa! Kukaza huko kwa vyuma kulifanya pombe za kienyeji zipande chati, hususan wanzuki na kangala.
Sasa leo nikiona hivi vitoto vya miaka ya 90 vikijiliza liza eti vyuma vimekaza huku majumbani kwao kuna DSTV, maduka yamejaa kila aina ya bidhaa, vikienda baa vinakunywa Smirnoff, Savanna nini sijui, Hennessy V nini sijui, vinavaa nguo za madizaina [hata kama ni feki], yaani starehe mwanzo mwisho!
Nikiona hivyo huwa najiuliza sana...kama sasa hivi vyuma vimekaza...enzi zile vilikuwa vimefanya nini sasa!
Nani humu kaenda dukani akakosa Colgate, kwa mfano?
Nani hajanywa soda mwaka mzima? Nani hajanywa Fursana au Mo Orange kisa kashindwa kununua kwa sababu vyuma vimekaza?
Nani kaenda dukani kununua Rinju akakosa?
Tumekuwa watu walaini mno sisi. Watu wa kudekadeka tu.
Vyuma vilikaza miaka hiyo. Hakuna vyuma vilivyokaza miaka hii.
Acheni usleki mayai.