SoC01 Vyanzo vipya vya mapato kwa Serikali

Stories of Change - 2021 Competition

KiuyaJibu

JF-Expert Member
Aug 29, 2007
841
175
Utangulizi

Ninasikitishwa sana na utendaji wa Wizara ya fedha katika suala zima la uandaaji wa bajeti kwa Serikali ya Tanzania. Kila mara bajeti inaposomwa Bungeni na Waziri wa fedha pamoja na mambo mengine, huwa inakuwa na ongezeko la kodi/tozo kwenye bidhaa zile zile ambazo zimeguswa na ongezeko la kodi/tozo katika bajeti zilizopita; kwa mfano kwenye mafuta (nishati), mawasiliano, vinywaji vyenye kilevi na visivyo na kilevi, sigara. Sijaona sababu ya msingi ya kuongeza tozo kwenye huduma za simu ukizingatia makampuni ya simu yanailipa kodi serikali; sekta ya mawasiliano na nishati ni vichocheo vikubwa vya ukuaji wa uchumi katika Taifa lolote. Kwa upande wa mawasiliano na nishati inashangaza kuona sekta hizo zikiandamwa na ongezeko la kodi/tozo kama ilivyojitokeza kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2021/2022 hii inaonyesha mtizamo wa Wizara ya Fedha kuwa sekta hizo ni anasa.

Lengo kuu

Ili Serikali iweze kujiendesha na kutekeleza mipango iliyojipangia kwaajili ya kuboresha maisha ya watu wake inahitaji rasimali watu na fedha; hili la fedha ndiyo linalotokana na makusanyo ya kodi/tozo mbalimbali kazi inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ninachojua, hakuna ukomo katika ukusanyaji wa mapato ila kuna ukomo katika matumizi ya mapato yaliyokusanywa. Ukusanyaji wa mapato uzingatie hali halisi ya vipato vya wananchi, ukweli uliopo ni kwamba Watanzania walio wengi ni masikini na nchi pia; japo ina utajiri ambao haujageuzwa kuwa mapato. Kuepuka tatizo, Wizara ya fedha ilitakiwa ifanye upembuzi yakinifu kuhusu uwezo wa Watanzania kama wanaweza kumudu tozo iliyo pendekezwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye miamala ya fedha kwa njia ya simu.


Kwa hali hii, Wizara ya fedha imeonyesha udhaifu katika suala zima la ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato.

Mapendekezo

Kutokana na tozo kuwa kero kwa Watanzania walio wengi; nimefikiria na kupata vyanzo 09 vya mapato ambavyo vinaweza kuipatia Serikali mapato inayostahili kwa lengo la kushughulikia maendeleo ya nchi na kuboresha maisha ya Watanzania. Vyanzo hivyo ni kama ifuatavyo:

  • Kodi kwa madalali wote

  • Hii ni biashara ambayo imekuwa ikifanywa kwa muda mrefu hivi sasa; dalali anaweza kuwa mtu binafsi au kampuni ambaye ana nadi na kuuza bidhaa au huduma kwa niaba ya mwenye mali/mmiliki; wanajishughulisha kwenye biashara tofauti tofauti mfano ardhi; kilimo; mifugo na uvuvi; magari na vipuri; mashine, mitambo na vipuri na biashara ya huduma pia.

  • Kodi kwa Viongozi Wote

  • Yafanyike marekebisho ya sheria kuhakikisha kila kiongozi mwenye cheo cha kisiasa analipa kodi kama wanavyolipa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi.

  • Bandari na Meli za Uvuvi

  • Zinazofanya uvuvi katika maeneo yote ya Tanzania; kwasababu kilichogundulika hapa ni kwamba Serikali inatumia gharama kukusanya mapato kwa wavuvi wadogo na kuwaacha wavuvi wanaovua malaki hadi mamilioni ya samaki kila kukicha; kinachotakiwa kufanyika ni kujenga bandari za uvuvi.

  • Biashara za Mtandaoni (Online Marketing & Sales)
  • Kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia; kumechochea ukuaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari (IT) na TEHAMA (ICT). Pamoja na mambo mengine ambayo Serikali imekwisha yafanyia kazi kwenye eneo hili; ninacho fahamu hadi hivi sasa hakuna sheria inayosimamia biashara hii. Nafikiri imefika wakati sasa ufanyike utaratibu wa kupata sheria itakayoitambua na kudhibiti ili Serikali iweze kupata mapato pia.

  • Haki za Miliki Ubunifu (Intellectual Property Right)

  • Miliki bunifu ni mali (assets) kama ilivyo kiwanja, nyumba au gari; ndani yake ziko nyingi sana kwa mfano ulinzi kwenye Alama za Biashara na Huduma (Trade and Service Marks), Hataza (Patents), Hatimiliki (Copyright), kukuza mimea (Plant breeders), Asili ya bidhaa (Geographical indication), Ubunifu wa bidhaa (Industrial design) ila kwa Tanzania sheria zilizopo zinafanya kazi kwenye eneo la Alama za Biashara na Huduma, Hataza, Hatimiliki pamoja na kukuza mimea ni ukweli usiyopingika Tanzania inafanya sehemu ndogo kwenye eneo hili. Kuna kiasi cha mapato ambacho Serikali inaweza kujipatia kwa kuchukua kodi/tozo kwenye maeneo hayo machache tunayo yafanyia ulinzi wake kulingana na sheria zilizopo. Kwa kuwa ni mali, mmiliki wake anaweza kuuza kwa mtu mwingine au kukodisha pia kwa mikataba na kulipana kiasi cha fedha watakacho kubaliana baina ya pande mbili. Hali ilivyo hivi sasa, kwenye uuzaji na ukodishaji wake ni ada tu ndiyo inayotozwa kwa mujibu wa sheria husika hakuna kodi inayochukuliwa.
  • Maboresho ya sheria za uwekezaji sekta ya madini

  • Chanzo kikubwa ni madini, Wizara ya fedha inachotakiwa kufanya ni kushughulikia tafiti na mapendekezo yaliyotolewa na kamati zilizoundwa kuchunguza mikataba mibovu ya madini iliyosainiwa kipindi cha Serikali ya awamu ya tatu hadi sasa; mojawapo ni mrahaba uongezwe, misamaha ya kodi ifutwe na makampuni yaanze kulipa kodi mara moja kuchangia pato la Taifa kama inavyofanyika kwa wawekezaji wengine.
Katika sekta ya madini nchini Tanzania wanaonufaika zaidi ni wawekezaji na nchi inaambulia kidogo.

Kwa mfano,kwenye kila Tshs 100/= Serikali inapata Tshs 3/= na mwekezaji anapata Tshs 97/=. Hicho kiasi Serikali inachopata kinaitwa mrahaba; kuhusu kodi wamesamehewa (Tax holiday) kwa madai kwamba walisema wanapata hasara na wanafidia gharama za uwekezaji.

Baadaye Serikali ilishituka na kuamua kufanya uchunguzi kama kweli tuhuma za wawekezaji ni sahihi; kampuni iitwayo Stewart kutoka Marekani ilipewa kazi hiyo.

Jibu kwa ufupi likawa,Serikali inaibiwa kiasi cha robo ya bajeti yake kwa mwaka inapotea.

  • Maboresho ya sheria za ubinafsishaji wa mali za Umma

  • Ubinafsishaji wa mali za umma uzingatie ukweli na uhitaji wa kufanya hivyo kiweledi na uadilifu; kwa kutanguliza maslahi ya nchi mbele. Walengwa wa kwanza kupatiwa hizo mali wawe ni Wazalendo au Wazalendo kwa kuingia ubia na wageni au Wazalendo na Serikali.
Mfano, shughuli za uendeshaji uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro, zilibinafsishwa kwa mwekezaji mmoja; ambaye anailipa Serikali kodi ya dola za kimarekani 1000 kwa mwezi. Mwekezaji huyo analipwa na kila shirika la ndege dola za kimarekani 5000 kwa mwezi.

Swali la kutizama mapato, kuna mashirika mangapi ambayo ndege zake zinatua Kilimanjaro International Airport (KIA)? Naamini ni mengi,lakini Serikali imekubali kudhulumiwa wakiwa wanalijua hilo.

Mwingine ni hoteli iliyojengwa hapo awali ikiitwa Sheraton,walipewa msamaha wa kodi wa miaka mitano,baadaye ikaitwa Royal Palm halafu Movenpick na hivi sasa Serena; sijui kama msamaha unaendelea kuwepo! Hii ni kutokana na udhaifu wa sheria za uwekezaji ambapo Serikali inachezewa mchezo na wawekezaji.

Hutuwezi kutegemea fedha ya kodi kutoka katika duka, genge ili kuipatia Serikali mapato ambayo yatafanya bajeti yetu isiwe tegemezi. Tusipo badilika, ni sawa na kuchota maji kisimani kwa lengo la kujaza bahari.

  • Maboresho sheria za uwekezaji

  • Kuwekwe vifungu kwenye sheria vya kuwalazimisha wawekezaji wa kigeni kuingia ubia na Wazalendo, kutumia malighafi zilizopo nchini na wataalam wa ndani; itakuwa vinginevyo endapo itathibitishwa hakuna hapa nchini. Na kuhakikisha akaunti zao za benki zinafunguliwa kwenye benki zilizopo nchini; lengo likiwa kuwawezesha Watanzania kukuza vipato vyao na Taifa kupata mapato inayostahili.
Kwa mfano, Agosti, 2012 gazeti la The Guardian lilichapisha matokeo ya utafiti kuhusu sekta ya utalii; utafiti uliofanywa na Makamu mkuu wa chuo kikuu cha St.Augustine Dk.Charles Kitima.

Kwa mujibu wa utafiti huo, karibu trillioni 1.2 fedha za Kitanzania zinazopatikana kila mwaka kutoka katika sekta hiyo huishia nje ya nchi (capital flight) yanakotoka mashirika makubwa ya kimataifa (multinational companies) yanayomiliki hisa nyingi kwenye biashara ya utalii hapa nchini.

Mwingine, vitalu vya uwindaji 95% vinamilikiwa na wageni na 05% wakiambulia Wazalendo. Hii ni sababu kubwa ya fedha nyingi kwenda nje ya nchi. Ingawa utafiti wa Dk.Kitima uligusa sekta ya utalii pekee, ni imani yangu kuwa hali hiyo ipo katika sekta nyingine. Hali ilivyo inatufanya baadhi yetu tuanze kujiuliza hii ndiyo stahiki yetu kwa kuwaamini na kuwategemea wawekezaji wa kigeni!

Ikumbukwe kwamba wawekezaji wote wa kigeni wanapoingia katika nchi yoyote ambayo ina sheria na sera dhaifu; lengo lao kubwa pekee ni kujitengenezea fedha na kuzipeleka kwao kila mwaka; na ndiyo maana hujiondokea haraka kwa kufunga au kuuza biashara zao wanapoona hawapati tena faida au kipindi cha unafuu wa kodi (tax holiday) walichopewa kimemalizika.

Ninakubaliana na msimamo wa marehemu Robert Mugabe (aliyekuwa Rais wa Zimbabwe); alishinikiza uwepo wa sheria inayowalazimisha wawekezaji wageni kuwa na ubia na Wazalendo. Kupitia tangazo la Serikali Na.280 la mwaka 2012, ambapo kila biashara kubwa nchini humo 49% imilikiwe na wageni na 51% Wazalendo. Ilikuwa hivyo kwenye sekta za madini, utalii, nishati, usafiri, mawasiliano, elimu, na fedha.

Ingawa Bw. Mugabe alishutumiwa sana kwa uamuzi huo uliotafsiriwa kuwa ni wa kidikteta; alilenga kuinufaisha nchi yake. Kuwa fanya Wazalendo wamiliki 51% ya hisa katika kila biashara kubwa, kuna hakikisha angalau mapato ya asilimia hiyo yanabaki nchini Zimbabwe kila mwaka.

Maboresho sheria za Benki na fedha

Kwenye eneo hili ni kuzuia utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na kufanya kuwe na mzunguko mkubwa wa fedha; kwa mfano, ripoti ya utafiti wa utoroshaji wa fedha nchini kwenda kufichwa katika benki za nje ikiwamo Uswisi uliofanywa na shirika la Global Financial Integrity umeonyesha kuwa fedha nyingi kutoka Tanzania zilitoroshwa katika kipindi cha utawala wa awamu ya nne kati ya 2005 na 2009.

Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa katika kipindi cha utawala wa kwanza ulioishia 1985, fedha zilizofichwa nje zilikuwa Dola 3,493.3 milioni (Sh5.5 trilioni) na katika awamu ya tatu kati ya 1995 hadi 2005, zilikuwa Dola 2,108.8 milioni (Sh3.3 trilioni) wakati katika awamu ya pili zilitoroshwa Dola 529.1 milioni (Sh846 bilioni).

Hitimisho

Ili Serikali iweze kupata matokeo chanya kwenye mapendekezo haya kuna haja ya kuwekeza kwenye kutunga sera, sheria na kanuni mpya; kuna ambazo zitatakiwa kufanyiwa marejeo na huenda zingine zikafutwa.
 
Back
Top Bottom