Viwanda vya juisi, pombe ya korosho vyaja

elivina shambuni

JF-Expert Member
May 31, 2018
461
295
1573197806150.png


WAFANYABIASHARA wakubwa wa korosho, wawekezaji na watafi ti 169 kutoka nchi 13 duniani zikiwamo nchi zinazoongoza kwa ununuzi wa korosho, India na Vietnam, wamekubaliana kuzuia uuzwaji wa korosho ghafi kutoka nchini kwenda nje ya nchi.

Badala yake, wametaka korosho iendelezwe hapa hapa nchini na kuuzwa nje ikiwa imeshachakatwa ili malighafi zake ziendeleze viwanda hapa nchini. Wamepanga kuanza maandalizi sasa hivi ili msimu ujao wa mwaka 2020/2021, wasitishe kuuza korosho ghafi nje ya nchi.

Hayo yameridhiwa kwenye mkutano wa siku tatu wa maendeleo ya korosho unaomalizika kesho. Mkutano huo umeitishwa na Shirikisho la Korosho Afrika (ACA), ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana pia kushiriki kikamilifu kusaidia maendeleo ya zao hilo, huku wakiainisha fursa katika zao la korosho nchini.

Katika kikao hicho kilichofunguliwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, wadau hao walionesha nia ya kushirikiana na serikali katika kuwekeza kwenye mikoa 17 inayolima zao hilo, hasa kwa kufunga mashine za kubangua korosho, kulima mashamba makubwa, kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao yatokanayo na korosho pamoja na kufungasha kabla ya kuingiza bidhaa sokoni.

Akizungumzia korosho, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sekta Binafsi ya Korosho kutokea Ghana, nchi ambayo ndio Makao Makuu ya ACA, Mary Adzanyo alibainisha kuwa uwekezaji ukifanyika hapa nchini, utachochea uanzishwaji wa viwanda vingine, vitakavyoendeleza faida za korosho.

Alitoa mfano Tanzania inaweza kuanzisha viwanda vya juisi itokanayo na bibo la korosho, kinywaji ambacho ni maarufu zaidi nchini Ghana. Pia, kwamba Tanzania inaweza kuzalisha pombe kali inayoweza kuuzwa hata katika soko la kimataifa kutokana na korosho Alisema “hii inaweza kuwa ni fursa kubwa kwa kuwa kati ya wawekezaji waliohudhuria mkutano huu wapo wa kimataifa ambao wamewekeza nchi mbalimbali duniani, hivyo uwekezaji kama huu ni uwekezaji mkubwa ambao unaweza kuwa na tija kwa watanzania hasa kutoa ajira na kuzalisha bidhaa nyingine kubwa tu”.


Kwa upande wake, Waziri Hasunga alibainisha kuwa uwekezaji huo, utaiwezesha sekta binafsi nchini kuuza korosho nje ya nchi ikiwa katika hatua ya mwisho ya kuliwa na kuiwezesha korosho ya Tanzania kuwa na thamani zaidi na faida kwa wakulima.

Akizungumzia mkakati wa serikali katika kuliinua zao la korosho ili kuendana na uhitaji wa soko wa kimataifa, serikali imepanga kupanda mikorosho milioni 15 kila mwaka ili ifikapo msimu wa mwaka 2024/25 ivune korosho zaidi ya tani milioni moja.

Mkakati huo unaendana na kuongezwa kwa mikoa ya kulima zao hilo kufikia mikoa 17 huku wakuu wa mikoa, wakiwa wamepewa maelekezo kuhusiana na upandaji huo wa miti. Alisema, Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Naliendele, kinazidi kutafiti mbegu bora za korosho ikiwemo kuwaelimisha wakulima na maofisa ugani wa mikoa namna bora ya kuliendeleza zao hilo.

Alibainisha kuwa kutokana na mazingira ya kijiografia, Tanzania inaanza kuvuna korosho miezi sita kabla ya nchi nyingine, hivyo kuna uwezekano mkubwa kama ikijipanga vema katika soko la korosho, inaweza kutoka kuwa nchi ya nne kwa uzalishaji hadi kuwa nchi ya kwanza.

Alisema uwekezaji huo ukifanyika kikamilifu, kama ambavyo wawekezaji wamepania, utaongeza kiwango cha ubanguaji wa korosho kutoka asilimia 60 kinachofanyiwa kazi hapa nchini hadi kufikia uwezo wa kubangua korosho yote hapa nchini. Aliongeza kuwa serikali imejipanga kwenye msimu ujao wa korosho, kuhakikisha kuwa inapitia upya sera ya kilimo cha korosho na kuweka sera zenye tija zaidi kwa wakulima na kuwavutia wawekezaji.

Alisema wakulima watafundishwa na kuwezeshwa kuingia makubaliano na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ili ardhi yao itumike kwa kilimo hicho, huku akigusia kuhusu namna ambavyo wakulima wameshaanza kunufaika na zao hilo. Kwa msimu huu imeshafanyika minada mitatu, ambapo sera inayotumika ni ya uwazi, kwa kuwauliza wakulima kama wanakubaliana na bei, ambayo mnunuzi anaitaja ambapo hadi sasa bei inayoongoza sokoni ni ya Sh 2,500 hadi 2,660, kiwango ambacho alisema sio cha kuridhisha na kuomba wanunuzi wengine wengi zaidi kujitokeza.

Alisema: “Wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza hapa nchini na uwekezaji wao sio wa kubabaisha wanataka kuwekeza kwenye ubanguaji, uandaaji na hata kuendeleza bidhaa nyingine zitokanazo na korosho, kutakuwa na viwanda vya juisi na hata pombe itokanayo na zao hilo.

Huu ndio uwekezaji mkubwa wenye tija katika korosho, ni lazima faida ya korosho ibakie hapa nchini na tumejipanga kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni kutokea kwenye kiwango cha tani 300,000 ambacho ni kiwango kikubwa kwa mwaka wa 2017/18”.

Nchi ambazo wadau hao wa korosho wanatoka, idadi ya washiriki ikiwa kwenye mabano ni Benin (30), Burkina Faso (34), China (3), Cote de Ivore (14), Ufaransa mmoja, Ujerumani mmoja, Ghana (24), Guinea Bissau (11), Kenya (3), Korea mmoja, Msumbiji (32), Uholanzi( 4), Nigeria (8), Senegal (1), Siera Leone(1) , Afrika Kusini (1), Umoja wa Falme za Kiarabu (12, Tanzania 59, Marekani (5), Uingereza mmoja na Vietnam (3).
 
Aaaaaaa sasa Korosho tena wazalishe pombe kari? Mbona ivyo tena? Juice haitoshi?
 
Good move yasiwe maneno tu..vitendo vichukue nafasi..ila msisahau na kulipa wakulima pesa zao..
 
Back
Top Bottom