Vijana wengi wako kwenye hatari ya kupata ajali za barabarani zinazochangiwa na uendeshaji wa bodaboda na bajaj

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,501
9,280
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), watoto kuanzia miaka mitano hadi 29, wako katika hatari zaidi kutokana na vijana kujikita katika uendeshaji wa bodaboda na bajaji.

Pia takwimu za WHO zinaonyesha chanzo cha vifo namba nane duniani kinatokana na ajali za barabarani.

Balozi wa usalama barabarani, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Road Safety Ambassador (RSA), Augustus Fungo, alisema hayo mjini Kibaha, mkoani Pwani wakati wa kuhitimisha sehemu ya mradi wa elimu ya usalama barabarani, kwa shule za msingi na sekondari 12 za mkoani humo.

Alisema mradi huo wa miezi nane ulianza Novemba mwaka 2019 na ulikuwa ukitekelezwa katika mikoa ya Pwani na Kilimanjaro.

Alisema takwimu za WHO zinaonyesha watu 1,350,000 wanapoteza maisha huku zaidi ya milioni 50 wakiachwa na ulemavu wa kudumu duniani.

"Kutokana na hali hii tumeanza kutoa elimu na tutaendelea kufanya hivi kuwanusuru vijana ambao wengi wao ni madereva wa bodaboda na bajaji," alisema.

Alisema wanatarajia kutoa elimu hiyo kwa watu wenye ulemavu ili nao watambue sheria za barabarani na kuepuka ajali.

Naye, Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, ASP Africanus Sulle, alisema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza ajali hasa kwa wanafunzi ambao wanatumia barabara kuu kuvuka kwenda shuleni.

Alitoa wito kwa wazazi kuwasaidia kuwavusha watoto barabarani badala ya kuwaacha wavuke peke yao.

Alitaja maeneo ambayo alama za zebra zimefutika watashiriki na wakala wa barabara zichorwe upya ili kuepusha wanafunzi na watu wengine kugongwa wanapovuka barabara.

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kongowe, Nyambura Marwa, alisema elimu hiyo imewasaidia kwa kuwa kwa sasa wanaitumia kuvusha wengine na wamefanikiwa kupunguza ajali ambazo zilikuwa zikitokea awali.


IPPMedia
 
Back
Top Bottom