Sehemu ya 130
Ndege ilipotua, watu wakateremka, jeneza likashushwa, watu wakaanza kulia kwa sauti, kila mmoja alitaka kuligusa jeneza hilo ambalo lilipakizwa na kuanza kupelekwa katika uwanja wa taifa ambapo huko watu walitakiwa kuaga na kisha kuelekea kanisani, kufanyiwa ibada na kwenda kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni.
Kila kitu kilichotakiwa kufanywa, kilifanywa na ilipofika majira ya saa kumi jioni, tayari msafara ukaanza kuelekea katika makaburi hayo na hivyo mapacha hao kuzikwa huko.
Ilikuwa ni huzuni, mapacha waliokuwa wameipatia Tanzania umaarufu walifariki, kila mmoja alihuzunika, japokuwa walikuwa wameondoka lakini kwenye akaunti yao waliacha utajiri mkubwa ambao wazazi wao wakaamua kutumia asilimia kumi ya utajiri huo kwa ajili ya kuwasaidia watoto waliokuwa kwenye matatizo mbalimbali.
Kwa msichana Patricia, aliendelea kuwa kwenye hali hiyohiyo kwa muda wa miaka mitano. Alikuwa akitibiwa kwa nguvu zote, pingili za mgongo wake ambazo ziliachia zikaanza kurudi na miaka miwili mbele, akafanikiwa kusimama na kuanza kutembea ila kumbukumbu zake hazikuweza kurudi tena.
Ubongo wake ulikuwa kama umeathiriwa, hakujua kilichotokea, hakujua kama aliwahi kuwa na mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa moyo wake wote. Wazazi walijitahidi kumpeleka katika hospitali mbalimbali lakini kote huko waliambiwa kwamba binti yao asingeweza kukumbuka kitu chochote mpaka kifo chake.
Maisha yake yakaanza upya, akaanza kutengeneza urafiki na watu wengine, hata alipokuwa akiziona picha za Walter na Walker hakuwa akikumbuka kitu chochote kile, kwake, watu hao walionekana kuwa wageni kabisa ambao aliwaona mara kadhaa walipokuwa wakimfuata hospitalini kumuona.
Naseku hakuwa na furaha, alikuwa mtu wa huzuni, kila alipokuwa akiziona picha za watoto wake, alikuwa akilia, machozi yalitiririka mashavuni mwake na kuyafuta kwa kutumia viganja vyake.
Hakikubadilika kitu, kwa mtoto mmoja waliyekuwa naye, Esta, wakaendelea kumlea na baada ya miaka minne, akaolewa na kufanikiwa kujifungua watoto mapacha wa kiume ambao kwa kuwaenzi ndugu zake, akaamua kuwaita Walter na Walker.
MWISHO.