Zitto Kabwe ni mwenyekiti mstaafu wa chama cha
ACT- Wazalendo aliyehudumu nafasi hiyo kwa muongo mmoja. Zitto alihamia ACT- Wazalendo mwaka 2015 baada ya
kuvuliwa uanachama ndani ya
CHADEMA kutokana na kilichoelezwa kukiuka katiba ya chama hicho kwa kupeleka mahakamani migogoro ambayo ilitakiwa kushughulikiwa ndani ya chama kwa mujibu wa katiba.
Kupitia tiketi ya CHADEMA Zitto aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini mwaka 2005 mpaka 2015. Akiwa kiongozi mstaafu ndani ya ACT- Wazalendo ameendelea kuwa mwanachama muhimu ndani ya chama hicho kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika siasa za Tanzania.
Video iliyochapishwa Facebook ikimuhusisha Zitto Kabwe.
Mtumiaji mmoja wa mtandao wa
Facebook alichapisha video inayomuonesha Mtangazaji wa Crown FM Salim Kikeke akiwa na Zitto Kabwe wakipigia chapuo wanachokiita jukwaa la uwekezaji la serikali na kuwashawishi watu kwenda kuwekeza pesa ili wapate faida.
Je, ni upi uhalisia wa video hiyo?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu (Key word search) umejiridhisha kuwa video hiyo imepotoshwa kutoka kwenye
video halisi ambayo ni sehemu ya matangazo mbashara ya kipindi cha 'Kasri la Kikeke' cha Crown FM kilichofanyika mwezi Septemba 03, 2024 na kuchapishwa katika mtandao wa
YouTube Septemba 04, 2024.
Video imepotoshwa kwa kuwekewa sauti tofauti na iliyokuwepo awali katika video halisi hivyo kupotosha uhalisia. Sauti hiyo imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili Unde. Hata hivyo video pia inaonesha kuwa na madhaifu ikiwemo kuchezacheza kwamdomo ukionekana kuungana na kinasa sauti (microphone) jambo ambalo si la kawaida na halionekani katika video halisi.
Katika video halisi Salim Kikeke anaonekana akimuuliza Zitto Kabwe kwamba kwanini aliamua kupisha nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo katika chama chake. katika sehemu ya majibu yake Zitto alisema,
“Nimestaafu uongozi ndani ya chama kwasababu Katiba ya Chama chetu ina ukomo wa uongozi ndani ya Chama, unakuwa kiongozi kwa mihula isiyozidi miwili”