Uzinduzi wa Zakka Zanzibar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uzinduzi wa Zakka Zanzibar

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by abdulahsaf, Jun 23, 2012.

 1. a

  abdulahsaf JF-Expert Member

  #1
  Jun 23, 2012
  Joined: Aug 31, 2010
  Messages: 859
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  [h=1][/h]Posted on June 23, 2012 by zanzibaryetu
  [​IMG]Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein,akizindua Shuhuli za Zakka Zanzibar katika Ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Zanzibar leo,(kushoto) ni Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,na (kulia) Kaimu Waziri wa Katiba na Sheria na Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Alhaj Nassor Ahmed Mazrui.

  Napenda kutoa wito kwa kila mmoja wetu kuitumia fursa ya kutoa zaka na kuuchangia Mfuko wa Zaka ili kutekeleza wajibu wetu kwa Mola wetu na kuzingatia manufaa mengine yaliyokwishaelezwa. Vigezo vya namna ambayo mfuko kama huu unaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuinua maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi yanaonekana katika mataifa mbali mbali duniani zikiwemo Sudan, Afrika Kusini, Uturuki na nchi nyingi nyenginezo. Wahenga walisema: “Matukio ya mwenzako ni mafunzo kwako”. Kwa hivyo, tuna fursa ya kutumia mbinu bora zinazowasaidia wenzetu kama ni mafunzo mema kwa upande wetu.
  HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
  LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
  KATIKA HAFLA YA UZINDUZI WA MFUKO WA ZAKA
  ZANZIBAR, TAREHE 23 JUNI, 2012 HOTELI YA BWAWANI
  Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
  Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria,
  Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi,
  Mheshimiwa Jaji Mkuu,
  Mheshimiwa Mufti Mkuu wa Zanzibar,
  Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri,
  Ndugu Viongozi mbali mbali wa Dini,
  Ndugu Wananchi,
  Mabibi na Mabwana,
  Assalaam Aleykum Warahmatullah Wabarakatuh
  Awali ya yote tuna wajibu wa kumshukuru Mola wetu (SW) Mwingi wa Rehma na Utukufu, Muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake kwa kutujaalia neema ya uhai na uzima tukaweza kukutana hapa asubuhi hii tukiwa katika hali ya amani na utulivu.
  Sala na salamu zimshukuie mbora wa viumbe na mtukufu wa daraja ambaye ndiye kigezo chetu cha uongofu, Mtume wetu Muhammad (SAW) pamoja na wafuasi wake waliofuata njia yake na kuahidiwa malipo mema hapa duniani na kesho akhera tuendako. Tumuombe Mwenyezi Mungu nasi tuwe pamoja nao.
  Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
  Leo ni siku muhimu sana katika historia ya nchi yetu. Ni jambo la kumshukuru sana Mola wetu kwa kutuwezesha hatimae kutimiza ndoto yetu ya muda mrefu ya kuzindua rasmi shughuli za Mfuko wa Zaka hapa Zanzibar. Maelezo ya Katibu Mtendaji wa Wakfu yameelezea jitihada mbali mbali zilizofanyika hadi leo tumefikia hatua hii ya kufanya uzinduzi rasmi wa shughuli hizi. Tumuombe Mwenyezi Mungu awalipe kila la kheri duniani na akhera watu wote waliochangia kwa namna mbali mbali katika kulifanikisha jambo hili na kwa pamoja atupe uwezo wa kuyatimiza malengo yake kwa ufanisi na katika njia anazoziridhia Yeye.
  Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
  Mafundisho ya dini yetu ya Kiislamu yanabainisha kuwa Zaka ni nguzo katika Uislamu sawa na nguzo nyengine zikiwemo Shahada, Swala, Saumu na Hija. Zaka inakuja ngazi ya tatu baada ya sala. Kwa hivyo, miongoni mwa mambo ya msingi katika hadhara hii ni hatua ya kukumbushana juu ya wajibu wetu huu. Mola wetu ametutaka waumini tukumbushane katika kutenda mema katika aya mbali mbali za kitabu chetu kitukufu cha Kurani. Mwenyezi Mungu anatutanabahisha katika Kurani aya 55 ya Surat Adh-Dhaariyaat kwa kusema:
  “Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa waumini”.
  Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
  Sote ni mashahidi kuwa pamoja na uzito mkubwa ambao Zaka imepewa lakini bado nguzo hii ya Kiislamu haijapata uzito unaostahiki katika jamii yetu. Mafundisho ya dini yanabainisha kuwa Zaka imefaradhishwa kwa kila Muislamu mwenye uwezo na ina faida nyingi kama tunavyoelezwa na maulamaa na mashekhe wetu kuwa mbali ya kuwa ni ibada yenye malipo bora mbele ya Mwenyezi Mungu, hujenga uhusiano bora wa watu katika jamii, husafisha mali tunazozichuma na huleta ustawi wa jamii na kupunguza tofauti ya pato miongoni mwa watu. Kadhalika, kutoa zaka ni namna bora ya kuzishukuru neema za Mwenyezi Mungu anazotupa kwa kuzitumia neema hizo katika njia anazoridhia Yeye ili tupate kurehemewa zaidi kama alivyoatuahidi katika kitabu chake cha Kuran Aya ya 7 ya Suratu Ibrahim kwa kusema:
  “Mkinishukuru nitakuzidishieni …….”.
  Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
  Serikali inatambua hali ya maisha ya wananchi na imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali katika kutekeleza jukumu lake la kuwawezesha wananchi kuinua hali zao za maisha na kupunguza umaskini. Kuna mipango mingi ambayo tumejipangia na tayari imeanza kuonesha matokeo mazuri katika utekelezaji wa malengo ya MKUZA na DIRA 2020. Pamoja na utekelezaji huo, Serikali inaendelea kutafuta mbinu mbali mbali ambazo zinaweza kusaidia na kutoa mchango muhimu katika azma yetu kuu ya kuinua kipato cha wananchi wetu na kuwapunguzia ukali wa maisha.
  Kwa mnasaba huu, Serikali imedhamiria kwa dhati kuitumia fursa ya utoaji wa zaka kuwa ni mojawapo ya vianzio vya kuwajengea uwezo wananchi katika jitihada za kuongeza mapato yao na kuwapunguzia umaskini. Tarekh ya Kiislamu inatufunza kuwa utoaji wa zaka katika jamii una mchango mkubwa katika kuinua hali ya maisha ya watu. Tunaelezwa kuwa katika zama za Ukhalifa wa Sayyidna Umar bin Abdulazizi bin Marwan, waumini walihamasika kutoa zaka mpaka ikawa wanakosekana watu wa kupewa katika jamii ile, kwani Mwenyezi Mungu ameshayabainisha makundi yanayostahiki kupewa zaka katika Suratu Tawba aya ya 60 kwa kusema:
  “Hakika zaka hupewa mafakiri na maskini na wanaozitumikia, na wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislamu) na katika kukomboa watumwa, na katika kuwasaidia wenye madeni, na katika njia ya Mwenyezi Mungu na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na ni mjuzi na mwenye hekima”.
  Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
  Napenda kutumia fursa hii kuwaeleza wananchi kuwa tayari Serikali imeshajitayarisha na utekelezaji wa azma hii. Kama ilivyokwishaelezwa na Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana kuwa uzinduzi wa shughuli hii leo ni hatua ya utekelezaji wa kuelekea malengo yetu ya muda mrefu ambayo kwa taufik ya Mwenyezi Mungu leo tupo katika hatua hii ya uzinduzi na Inshaallah iwe ni ngazi ya kuelekea katika hatua nyengine. Nimeelezwa kuwa hivi sasa chombo maalum cha kuratibu shughuli za zaka Zanzibar kimeshaanzishwa na kitaendesha shughuli zake chini ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana.
  Sina shaka na umahiri, uaminifu na uadilifu wa watendaji wake na pia nafarijika sana na wasimamizi wa chombo hiki kwani wana uzoefu mkubwa wa kubeba dhamana nzito kama hizi. Lakini ilivyokuwa wao ni wanaadamu wanaweza kuwa na upungufu, kwa sababu hakuna aliyekamilika, bali Aliyekamilika ni Yeye peke yake, Subhana. Naamini kuwa watashirikiana vyema na taasisi nyengine zote ambazo zitahusishwa katika utendaji wa majukumu yao ili lengo la kuanzishwa kwa shughuli hizi liweze kufanikiwa.
  Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
  Napenda kutoa wito kwa kila mmoja wetu kuitumia fursa ya kutoa zaka na kuuchangia Mfuko wa Zaka ili kutekeleza wajibu wetu kwa Mola wetu na kuzingatia manufaa mengine yaliyokwishaelezwa. Vigezo vya namna ambayo mfuko kama huu unaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuinua maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi yanaonekana katika mataifa mbali mbali duniani zikiwemo Sudan, Afrika Kusini, Uturuki na nchi nyingi nyenginezo. Wahenga walisema: “Matukio ya mwenzako ni mafunzo kwako”. Kwa hivyo, tuna fursa ya kutumia mbinu bora zinazowasaidia wenzetu kama ni mafunzo mema kwa upande wetu.
  Inaridhisha kusikia kuwa tayari kuna kiasi cha fedha ambazo zimeshachangwa na watu mbali mbali kwa ajili ya Mfuko huu na mipango imeshatayarishwa juu ya namna bora ya kuzihifadhi amana hizi, kuzitumia kwa utaratibu na maelekezo maalum na pia kuwepo kwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa Mfuko wa Zaka Zanzibar unakuwa endelevu. Ni wajibu wetu kuziunga mkono jitihada hizi iwe kwa kuchangia, kusimamia na wale watakaopewa zaka hii waitumie katika malengo yanayomridhisha Mwenyezi Mungu na ufike wakati na wao wanaopewa waanze kupata uwezo wa kuwapa wengine kama lengo kuu la Mfuko huo linavyokusudiwa.
  Katika hotuba yake ya kuaga, Mtume Muhammad (SAW) aliwataka waumini kila aliyekuwepo amfikishie habari asiekuwepo. Nami ninatowa wito kuwa ujumbe huu tuufikishe kwa wasiokuwepo. Tumepewa vitabu vya Muongozo wa Zaka na tumeahidiwa kuwa Muongozo wa Sadakatul Jariiya yaani wakfu nao uko njiani, hivyo tuzitumie vizuri nyenzo hizi muhimu na kwa yule anaetaka kuchapisha nakla nyingi zaidi kwa lengo la kuvigawa kwa watu mbali mbali basi awasiliane na Kamisheni ya Wakfu.
  Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
  Kwa kumalizia nasaha zangu hizi, kwa mara nyengine tena naushukuru uongozi wa Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar na Wizara ya Katiba na Sheria kwa jitihada zao katika kuifanikisha hatua hii ya kuzinduliwa rasmi kwa shughuli za Zaka Zanzibar. Nawahakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo pamoja nanyi katika utekelezaji wa shughuli hizi na wakati wote tupo tayari kupokea ushauri wa namna bora ya kuziendeleza shughuli hizi kwa manufaa ya wananchi na taifa letu kwa jumla.
  Napenda kukutieni shime muendelee na jitihada zenu hizi na kuwanasihi tena wananchi, taasisi na makundi mbali mbali kuuchangia mfuko wa Zaka wa Zanzibar huku nikiamini kuwa taratibu bora za kurahisisha watu kuchangia kutoka popote walipo zimekwishaandaliwa.
  Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa shughuli za Zaka Zanzibar zimezinduliwa rasmi. Wabillahi Tawfiq.
  Ahsanteni kwa kunisikiliza.
   
Loading...