UVCCM acheni kuhadaa Watanzania; hatudanganyiki! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

UVCCM acheni kuhadaa Watanzania; hatudanganyiki!

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, Oct 11, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Oct 11, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,580
  Likes Received: 5,762
  Trophy Points: 280
  UVCCM acheni kuhadaa Watanzania

  [​IMG]
  MWANAFALSAFA wa Kigiriki Socrates alishawahi kusema kuwa ukimpa somo mtu yeyote, kitu hiki ni sumu, na hiki ni chakula, halafu ukampa nafasi ya kuchagua kitu cha kula na katika uchaguzi wake akachagua kitu ambacho ni sumu, basi ujue huyo mtu alikuwa hajakuelewa.
  Niliwahi kushangaa siku za nyuma baadhi ya matamko mbalimbali, au kauli zinazotolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa.
  Kiuchumi na kijamii ndani ya taifa hili. Suala langu la kushangaa huwa ni kujadili hivi huyu ametafakari anachosema? Au anasema anachotafakari?
  Najiuliza, je, viongozi hawa hufikiri vema yote wanayoyasema au wanasema yote wanayofikiiri? Sipati jibu katika maswahi haya.
  Viongozi wa CCM wameshaonywa na Watanzania mbalimbali katika mikutano, au katika maswali ya mahojiano ya wazi, au kwa maandishi kama ambavyo wanaopenda kusema ukweli wamekuwa wakitumia nafasi za kuandika katika makala, lakini wapi?
  Nazidi kutafakari, kuna msemo ambao si maarufu sana husema kuwa “Mwenye pesa anaweza kununua kila kitu isipokuwa ufalme wa Mungu.”
  Hiyo inaweza kuwa ni sawa, sasa hawa viongozi wa CCM wenye pesa wameshindwa kweli kununua mtu mwenye mawazo ya kuwashauri ili matamko wanayotamka yasiwe yanawarudi wao? Angalau kama wao hawajui basi watafute mtu anayeweza kuwasaidia sema hiki hapa, hiki pale, na hiki huku.
  Hii itawawezesha kuwaona angalau wana nafuu.
  Ninatafakari zaidi wazo linalotekelezwa sasa hivi na UVCCM, yaani matembezi ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
  Kwa watu ambao si Watanzania wakisikia hili wazo linavyotekelezwa wanaweza wakapongeza sana kuwa kweli tunawaheshimu wahenga wetu, hasa huyu muasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere.
  Nimejiuliza sana, nikaona je, niamini haya yanayofanywa na UVCCM kuwa wanamuenzi Baba wa Taifa? Nimegundua kila ninalotafakari haliingii akilini, hata kwa Watanzania wengi, isipokuwa wachache wanaoweza kurubuniwa na mawazo mepesi, au hoja ambazo zinaweza kusemwa vijiweni tu, lakini si na watu walio tulia.
  Akiwahutubia wananchi wa Nyagunge, mkoani Mwanza, wakiwa safarini kwa miguu kuelekea Butiama, Katibu Mkuu wa UVCCM anawaasa wananchi kuwa: “Tumuenzi Baba wa Taifa, kwa kila kitu alichokianzisha, umoja, mshikamano, na kila alichokianzisha, ikiwamo CCM.”
  Falsafa yangu imeibuka na maswali mengi yakiwamo haya. Hivi kumuenzi Baba wa Taifa kunafanywa na vijana wa CCM tu? Kama wengine wa vyama pinzani wangealikwa wangekataa? Au Baba wa Taifa huyu wanayetaka tumuenzi ni wa CCM pekee? Je, Nyerere anamilikiwa na CCM?
  Huenda vijana wa vyama vingine wangekataa, je, UVCCM haioni kuwa ingewachukua na vijana wale wasio na vyama ingejipatia umaarufu kwa kuonyesha kuwajali Watanzania wote?
  Nikaenda mbele zaidi, nikakumbuka kuwa wanasisitiza mshikamano kwa Watanzania, hapo ndo nilishikwa na butwaa, hivi hawa vijana wana umri gani? Kweli hawaelewi maneno wanayotusimulia? Wanazungumzia umoja, umoja wanaouzungumzia ni upi, wa vyama vya upinzani?
  Au wa Watanzania wengine, maana Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi hivi majuzi amekiri kuwa hata wabunge wa chama hicho hawaamiani hata kuachiana soda katika meza? Kama katika CCM hakuna umoja, wanatufundisha mambo ambayo hata wao hawayatekelezi?
  Ningetegemea kusikia kuwa mshikamano unaohubiriwa na wana CCM hawa vijana ungehubiriwa vema katika chama ili sisi tuige mfano toka kwao, yaani wana CCM hawa wangeonyesha umoja. Mfano, Ole Sendeka na Ole Milya, waonyeshe mshikamano, Dk. Harrison Mwakeyembe na Rostam Aziz watoe tofauti zao, Edward Lowassa na Nape Nauye, wahutubie mkutano wa pamoja, Amos Makalla na Jaji Joseph Warioba waseme wana mshikamano, na kadhalika.
  Hayo nilitegemea kuyasikia kutoka CCM, sasa wao wanatoka katika nyumba chafu wanakuja kuzungumzia usafi nje ya nyumba na kuwasisitiza majirani kuwa usafi ni tabia njema. Waanze wao.
  Kama hiyo haitoshi, Katibu Mkuu wa UVCCM, akasema kwa kuwa Baba wa Taifa alikianzisha Chama Cha Mapinduzi, basi nacho tukienzi. Hapa nilisisimkwa na damu, nikajiuliza hivi huyu kijana hata historia ya Tanzania haijui, hajui kuwa Nyerere alikuwa ni mmoja wa viongozi walioridhia mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, bado anafikiri kuwa Nyerere ni wa CCM tu, sasa huyu ndiye kiongozi anajua mpaka hapo, je, wale ambao anawaongoza wanajua hadi wapi? Hili tuendelee kujiuliza wote.
  Wazo la kumuenzi Baba wa Taifa kwa matembezi ya mshikamano kutoka Mwanza hadi Butiama, wazo kama wazo ni zuri, lakini hofu yangu limeanzishwa katika utengano, je, Kitu kilichoanzishwa katika utengano kinaweza kutumika kuhubiri kuleta Muungano?
  Waliofikiria wazo hilo walianza na U-CCM badala ya utaifa, wakiongozwa na wazo kuwa Nyerere ni wa CCM na si Baba wa Taifa kama Watanzania wengi wanavyosadiki.
  Wangeanza na utaifa wangesema vijana mbalimbali nchini wajitokeze kumuenzi Mwalimu Nyerere, kwa matembezi ya mshikamano, bila kujali itikadi za vyama, ili kuhamasisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa vijana wote.
  Hapa katika wazo hili tungeweza kuwapata vijana wazalendo, wenye upendo na mshikamano wa kweli kwa taifa, wanaomuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo, bila kujali wamekula au hawajala, si hawa wa UVCCM ambao wametumia pesa nyingi kutengeneza mavazi rasmi eti ya kumuenzi Baba wa Taifa.
  Leo na kesho wakaondoka vijana wa CUF wanaanzia maandamano yao Buguruni, Dar es Salaam kwenda Butiama, kesho kutwa wa CHADEMA wakaamua kuanzia Kigoma kuelekea Butiama, mtondo wakajitokeza wa TLP kutoka Tanga wanaenda Butiama, mtondogoo wakajitokeza wa UDP kutoka Bariadi kwenda Butiama. Hawa wote ni wale wanaomchukulia Mwalimu Nyerere kuwa ni Baba wa Taifa, wala hajamilikiwa na CCM kama wengine mnavyosadiki, je, tutakuwa tunahubiri umoja na mshikamano wa kitaifa?
  Kinachofanyika, kinakaribiana sana na maigizo, japo katika maana halisi nimeshindwa kujua niyataje kwa jina lipi matembezi hayo.
  Sana sana yametufanya kuibua maswali kuwauliza UVCCM kuwa wanamuenzi Nyerere katika lipi? Wanamuenzi katika mavazi? Wanamuenzi katika mshikamano, je, ni mshikamano upi wanaouhubiri ambao wao katika chama hawana na wanatangaza hadharani?
  Nyerere alipotembea kwa miguu alikuwa akihamasisha siasa ya ujamaa na kujitegemea, sasa katika matabaka yaliyopo ndani ya CCM yenyewe, na ndani ya Tanzania, je, inawezekana tukahubiri umoja?
  Tayari kuna mawazo tofauti ya kitabaka, wapo wa juu na wa chini, ambao mawazo yao hayapo pamoja, mwingine ni mnyonyaji, mwingine ni mnyonywaji, tutasema kuwa hapa tuhamasishe umoja?
  Mpanda ngazi na mshuka ngazi watashikana mkono? Tuna safari ndefu ya kufikiri namna ya kumuenzi Baba wa Taifa, lakini tutafakari tunamuenzi katika lipi? Na tunamuenzi vipi? Vinginevyo tutakuwa tunawahadaa Watanzania na kutumia vibaya rasilimali zetu kuwa tunamuenzi Nyerere kumbe ni ulaghai mtupu kama inavyofanywa na UVCCM. Na kama hawa bado hawajitambui kuwa wanahadaa Watanzania, basi bado hawajui maana ya kumuenzi Baba wa Taifa ina faa wafundishwe, wajue wanachosema ili wote kama taifa tuzungumzie mshikamano na umoja huo ambao ni wa dhati aliouanzisha Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake.
   
 2. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #2
  Oct 11, 2009
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
  Angekuwa bado hai baba wa taifa angewaambia hao vijana kwanza waache unafiki.
  Pili, angewaambia wasafishe chama chao, na tatu angewauliza ni juhudi gani walizochukua kupambana na ufisadi ndani ya chama chao.
   
 3. Limbani

  Limbani JF-Expert Member

  #3
  Oct 12, 2009
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 1,441
  Likes Received: 92
  Trophy Points: 145
  Hiyo ni moja ya sehemu ya ufisadi CCM, hao vijana wanafanya hivyo kusubiri posho tu na si vinginevyo
   
Loading...