SoC01 Utoaji wa dawa na vifaa tiba kwa mfumo wa OTT hospitalini

Stories of Change - 2021 Competition

eam6476

New Member
Aug 24, 2021
2
1
Dawa na vifaa tiba ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa waliolazwa mahospitalini na kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na kustawi katika afya bora. Hospitalini ambapo dawa na vifaa tiba ni nyenzo muhimu katika uwezeshaji wa utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa, lakini sekta hii ya afya mara nyingi imekumbwa na uhaba wa dawa na vifaa tiba jambo ambalo linasababisha ugumu wa utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa hususani waliolazwa wodini licha ya kuwa serikali imeongeza bajeti yake katika wizara ya afya kwa lengo la kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana.

Naipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Wizara ya Afya kwa jitihada na juhudi mbalimbali zinazofanywa kuhakikisha kuna uwepo wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya licha ya uhaba huu uliochangiwa na ugonjwa wa virusi vya UVIKO-19 unaosababisha uhaba wa vitendea kazi. Hivyo kutokana na changamoto zilizopo za uhaba wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya, ni vyema tukaanza kufikiria njia nzuri zaidi ya kuzitumia rasilimali zilizopo ili kuhakikisha tunaokoa maisha ya ndugu zetu wagonjwa waliopo hospitalini. Moja ya njia hizi ni utoaji wa dawa na vifaa tiba kwa mfumo wa OTT.

OTT ni nini? OTT kwa kirefu chake ni “One Tme Taking”. Ni mfumo ambao dawa na vifaa tiba hutolewa kwa mara moja na kwa siku husika. Mfumo huu wa OTT utamsaidia mgonjwa kupata dawa zake za siku hiyo atakapokuwa wodini na kwa wakati unaofaa atumie dawa alizoandikiwa na daktari. Pia mfumo huu utawasaidia wauguzi kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi zaidi kwa wagonjwa kwa kuwa utawawezesha kupata vifaa tiba vinavyohitajika kuwahudumia wagonjwa waliolazwa wodini.

Mfumo huu wa OTT una faida mbalimbali kwa wagonjwa na hata kwa wahudumu wa afya mahospitalini na kwa serikali kwa ujumla iwapo mfumo huu utatumiwa kwa umakini. Hizi ni baadhi tu ya faida za kututumia mfumo wa OTT.

Utasaidia kupungua kwa gharama za matibabu kwa wagonjwa waliolazwa hopitalini. Mara nyingi wagonjwa waliolazwa hospitalini huwa wanakabiliwa na gharama kubwa za kulipia kutokana na huduma za afya wanazozipata pindi wanapotibiwa katika vituo ya afya. Sehemu kubwa ya gharama hizo huwa ni gharama za dawa na vifaa tiba wanavyovitumia wanapokuwa wakiuguzwa. Kwa kutumia mfumo wa OTT, utapunguza gharama za matibabu zinazotokana na dawa na vifaa tiba kwa sababu mgonjwa atapatiwa dawa na atahudumiwa kwa vifaa tiba sawa na idadi ya siku atakazokuwa amelazwa hospitalini. Kwa mfumo wa OTT utamsaidia mgonjwa kupata dawa alizoandikiwa na daktari na muda sahihi wa kupatiwa hizo dawa. Yaani dawa za kutumia asubuhi, za mchana, za jioni pamoja na dawa za usiku. Hivyo mgonjwa atalipia gharama za idadi ya vidonge au dawa za sindano atakazokuwa ametumia kwa siku husika na hiyo kumfanya awe na weledi wa gharama za matibabu anazozilipia.

Utapunguza mlundikano wa dawa na vifaa tiba wdini. Kwa kutumia mfumo wa OTT itapunguza mlundikano wa dawa na vifaa tiba visivyokuwa na matumizi wodini na hiyo kufanya mazingira ya kufanyia kazi kwa wauguzi waliopo wodini kuwa mazingira safi, salama na rafiki kwa kuwa watakuwa wanapatiwa vifaa tiba vinayohitajika kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kwa hiyo siku moja husika. Hii pia itasaidia kuhakikisha matumizi sahihi ya malighafi zilizo duni kwa mfano mipira ya mikono yaani ‘gloves’ na vifaa vinine vingi. Hii pia itawasaidia wauguzi kuweka rekodi sahihi ya vifaa tiba pamoja na makadirio sahihi ya vifaa tiba vilivyotumika kwa mgnjwa husika wakati wa kufunga mahesabu ya gharama za matibabu.

Utapunguza upotevu wa dawa wodini. Mfumo wa OTT utasaidia sana katika kupunguza upotevu wa dawa wodini. Upotevu wa dawa wodini unatokea wakati ambapo mgonjwa alikuwa akitumia dawa fulani husika na kabla hajamaliza kutumia dawa hizo, ikamlazimu daktari kubadilisha dawa kutokana na sababu mbalimbali za kitabibu. Kwa hivyo vile vidonge alivyokuwa akivituia mgonjwa hapo awali, vinakuwa havina matumizi tena kwa sababu daktari amebadilishia dawa. Lakini zile dawa zilizobaki bado pia ni rasilimali ambayo ikitunzwa itaweza kumsaidia mgonjwa mwingine na kumtibu. Hii ni hususani kwa dawa za vidonge na sio dawa za sindano.

Utasaidia ufuatiliaji wa karibu wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa wagonjwa. Hili ni jukumu muhimu hasa kwa wafamasia ili kuweza kuisaidia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ‘TMDA’ kuifuatilia dawa husika kwa ukaribu kulingana na madhara yatakayokuwa yametolewa ripoti kuhusu matumizi ya dawa husika kwa waonjwa. Mfumo wa OTT utawasaidia sana wafamasia kufahamu na kuchunguza zaidi madhara yatokanayo na matumizi ya dawa mbalimbali na kuweza kuzuia na kutibu madhara yatokanayo na matuizi ya dawa hizo kwa wagonjwa. Hili litawezekana kwa sababu mgonjwa atapatiwa dawa moja baada ya nyingine kwa nyakati tofauti na hivyo itawezesha kufahamu ni wakati gani amepata madhara kutokana na dawa alizopewa na kuweza kutoa taarifa kwa TMDA kwa kutumia fomu ya njano.

Utasaidia kupunguza mwingiliano kati ya dawa moja na nyingine ‘drug-drug interaction’ na mwingiliano katiya dawa na chakula ‘drug-food interaction’. Kupungua kwa mwingiliano wa dawa zaidi ya moja pamoja na chakula utasaidia dawa kutibu maradhi kwa ufanisi zaidi na kupunguza madhara yanayosababishwa na mwingiliano wa dawa na vyakula. Hii itasaidia kupungua kwa madhara yanayotokana na matumizi ya dawa ikiwemo kutokupona kwa maradhi yanayowasumbua. Hii ni kwa sababu kila dawa itatolewa na mfamasia kwa muda muafaka wa hiyo dawa husika kutumiwa ili kuzuia isilete mwingiliano na dawa nyingine au kupelekea madhara kutokea kwa monjwa.

Utawaleta kwa karibu wafamasia pamoja na wahudumu wengine wa afya katika utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa. Mfumo wa OTT utamfanya mfamasia awe bega kwa bega na madaktari pamoja na wauguzi wakati wa kuwaona wagonjwa wodini na kuweza kushauriana katika matibabu ya mgojwa husika. Hii pia itamsaidia mfamasia kuongeza maarifa zaidi kutoka kwa wataalamu wengine wa afya kama madaktari bingwa na wauguzi na kupanua wigo wa taaluma zilizo bobezi katika kada hii ya Famasia. Pia kwa uwepo wa mfamasia wodini itawasaidia madaktari kufahamu na kutumia dawa zilizopo kwenye taasisi husika na kuepusha gharama za ziada za matibabu kwa mgonjwa kuandikiwa dawa ambayo haipo katika taasisi hiyo anayotibiwa. Pia kwa uwepo wa wafamasia wodini utakuza matumizi sahihi ya dawa za vijiua sumu ‘Antibiotics’ na kuzuia usugu wa dawa utokanao na matumizi holela ya dawa za Antibiotics.

Utaongeza nafasi za ajira kwa wafamasia: Mfumo wa OTT utaiwezesha serikali chini ya wizara ya afya pamoja na hospitali za umma na hospitali binafsi kuongeza nafasi za ajira kwa wafamasia na pia kusogeza huduma za kifamasia karibu zaidi na mgonjwa. Hii itapunguza dhana potofu ya kwamba wafamasia ni watu wa kukaa dirishani na kugawa tu dawa au wezi wa dawa. Hii ni kwa sababu huduma za wafamasia na umahiri wao utaonekana zaidi pale wanapowahudumia wagonjwa mahosptalini katika wodi wanazokuwa wamelazwa. Hiyo kutakuwa na wafamasia wengi zaidi watakaokuwa wanahudumia wagonjwa kwa kuwapatia dawa sahihi kwa matumizi na kwa wakati sahihi kwa mfumo wa OTT, pamoja na kufuatilia kwa ukaribu zaidi maendeleo yao na kuzuia madhara yatokanayo na dawa wanazozitumia wagonjwa wa mahospitalini.

20210905_185528.jpg
Prepared by:
ERICK A. MINJA.
Intern Pharmacist.
Muhimbili National Hospital
Email: minjaerick7@gmail.com
 
Back
Top Bottom