SoC03 Utawala bora ndio umebeba mustakabali wa maisha

Stories of Change - 2023 Competition

Heavenlight Boman

New Member
May 4, 2023
3
2
Utangulizi
TANZANIA
ni miongoni mwa nchi inayoendelea barani Afrika, huku ikipambana kujikwamua kiuchumi kwa kupigana na umasikini, ujinga, maradhi pamoja na rushwa.

Licha ya kuwepo mapambano hayo lakini bado suala la utawala bora limekuwa changamoto kubwa bila kujua ndiyo limebeba msingi na mustakabali wa Taifa.

Utekelezaji wa dhana ya utawala bora ni muhimu sana kwa taifa lolote lililojiwekea malengo thabiti ya maendeleo kwa vizazi vijavyo, hususani kwa nchi zinazopatikana barani Afrika.

Dhana ya utawala bora tangu uhuru hadi sasa, hali ikooje?

Tukiangazia kwa ufupi dhana ya utawala bora tangu nchi ilipopata uhuru wake mnamo mwaka 1961 mpaka sasa, ni takribani vipindi vitano vya uongozi kwa awamu vimepita, na sasa ikiwa ni awamu ya Sita. Ambapo kila awamu imeweza kutekeleza dhana hii kwa namna yake.

Awamu ya kwanza na Julius Kambalage Nyerere( Uhuru na Kazi)
Katika awamu hii iliyoongozwa na Muasisi wa taifa hili Hayati Julius Nyerere iliweza kutekeleza dhana ya utawala bora hususani katika upande wa uhuru.

Kwa maana ya uhuru wa serikali itokanayo na watu,inayolinda uhuru wa watu kutoa maoni yakiwemo maoni yasiyoifurahisha serikali.

Awamu ya pili na Ali Hassan Mwinyi( Ruksa Tu)
Pia, awamu ya pili iliweza kutekeleza dhana ya utawala bora kwa kuweza kuanzisha mfumo wa vyama vingi, hali iliyosaidia kuwepo ushindani wa kisiasa na kuongeza wigo wa demokrasia kwa jamii.
Pia, hapa ndipo tumie ya uchaguzi ilipoundwa.

Awamu ya tatu na Benjamiin William Mkapa( Uwazi na Ukweli)
Awamu hii iliyoongozwa na Mwanadiplomasia, Hayati Benjamin Mkapa ilitekeleza dhana ya utawala bora kupitia kauli mbiu yake ya ukweli na uwazi katika siasa, uchumi na jamii.
Katika awamu hii ndipo Mamlaka ya Mapato (TRA) ilianzishwa, pamoja na utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa.

Awamu ya nne na Jakaya Mrisho Kikwete(Maisha Bora kwa kila Mtanzania)
Awamu hii ilitekeleza dhana ya utawala bora hususani katika kuimarisha, kuendeleza na kudumisha misingi yake, hali iliyosababisha Rais Jakaya Kikwete kutunikiwa tuzo ya utawala bora barani Afrika mwaka 2015.

Awamu ya Tano na John Pombe Magufuli(Hapa Kazi Tu)
Katika awamu ya Tano iliyoongozwa na Hayati John Magufuli,dhana ya utawala bora ilitekelezwa hasa katika uwajibikaji(kazi) viongozi wanapaswa kuwajibika bila kutanguliza maslahi yao mbele na badala yake wawajibike kwa wananchi ili kuchochea maendeleo katika taifa.

Awamu ya Sita na Samia Sulluhu Hassan(Kazi Iendelee)
Hii ndiyo awamu iliyopo madarakani wengi wakiitafsiri kama awamu iliyotekeleza dhana ya utawala bora katika masuala ya kujenga Tanzania moja yenye mshikamano(umoja kwa taifa) hasa kwa kutokuwa na ubaguzi wa misingi ya vyama vya siasa.

Hivyo, ni baadhii ya vipengele vilivyoashiria kutekelezwa kwa dhana ya utawala bora katika awamu Tano za uongozi zilizopita na awamu ya Sita ambayo kwasasa ipo madarakani.

Je,Utawala bora ni nini?
Utawala bora, ni matumizi mazuri ya mamlaka kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ambapo misingi yake ni pamoja na uwazi, haki, uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi, usawa na kufuata utawala wa sheria.

Kuna manufaa makubwa kwa taifa endapo litatekeleza dhana ya utawala bora ikiwa ni pamoja na mtumizi mazuri ya rasilimali za nchi, maendeleo endelevu, kutokomea kwa rushwa,kuheshimu haki za binadamu na kuwepo kwa huduma bora za jamii.

Nini kifanyike Taifa kuzingatia utawala bora?
Kuundwa sera toshelevu kuhusu utawala bora, nchi imejiwekea azma yake ya maendeleo lakini, bila kuwa na sera toshelevu zinazo husianani na utawala bora ni kumpigia mbuzi gitaa.

Sera toshelevu ndizo zitakazo amua yupi ndiyo kiongozi bora kwa taifa au bora kiongozi.

Kuboresha mifumo ya kiutendaji, Mifumo hii ya kiutendaji inajumuisha wajibu(uwajibikaji) wa kiongozi anawajibika vipi kuchochea maendeleo katika jamii inayomzunguka.

Viongozi walio wengi wanawajibika kutetea maslahi yao binafsi na siyo kuwatumikia wananchi, kuboreshwa kwa mifumo hii kutasaidia vingozi kutambua wajibu wao kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Utekelezaji wa misingi ya demokrasia, mfumo ambao wananchi wanashiriki katika kufanya maamuzi ya maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii ndio mfumo unaoheshimu dhana ya utawala bora.

Viongozi walio wengi wamekuwa wakitumia mabavu kutoa maamuzi katika jamii na kusahau kuwa dhamana yao ipo mikononi mwa wananchi. Utekelezaji wa misingi ya demokrasia ndio utasaidia Taifa kufikia malengo yake.

Hitimisho
Vita vya wenyewe kwa wenyewe, migogoro ya kikatiba, haki za binadamu kukandimizwa ndiyo miongoni mwa athari kubwa sana zitazokumba taifa iwapo litatupilia mbali dhana ya utawala bora.

Hata hivyo, taifa lijifunze kupitia makosa kwa kutazama mataifa mengine yenye migogoro mbalimbali, "ukicheka na nyani utavuna mabua" kwanini tuvune mabua?,ili hali tuna nafasi ya kusimama tena kama taifa kujenga misingi ya utawala bora kwa vizazi bora vijavyo.
 
Back
Top Bottom