Bolibo tena hutaki, bayana umeyanena,
Dodo umelimiliki, hutaki tena ya jana,
Kwa dodo huambiliki, mengine hujayaona,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.
Samaki ulimleta, JF uwanjani,
Na sifaze ukateta, harufu iso kifani,
Hatimaye ukajuta, ulimleta kwanini,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.
Kijijini wanicheka, na wengine wanong"ona,
Na hamu imenitoka, njaa bado ninaona,
Kipande kimedondoka, miye simtaki tena,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
Ulisema humtaki, kumbe ajenda ya siri,
Ukatutia mikiki, vishindo kikiri kikiri,
Oooh, huyu samaki, kwa harufu kakithiri,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.
Njaa imenizidia, ubishoo nauvua,
Samaki aniitia, mwenzenu nimeamua,
Nitamla naapia, magwiji nimeng'amua,
Maji nimeyavulia, sina budi kuyaoga.
Pamoja na uvundowe, umesema utamla,
Jibu tena usipewe, umefunga mjadala,
Umeshikwa na kiwewe, umeishiwa na hila,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.
Sasa ni zamu ya dodo, yu wapi yule samaki,
Umeuacha mpodo, umeshika msuaki,
Ana ana anado, utakosa tahamaki,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.
Mzee sinichukie, najifunza hapa hapa,
Mazuri uyachukue, mabaya waachie papa,
Nami usiniachie, pale nilokwenda kapa,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.