Utamu wa Dodo Kunyonya..

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,463
39,930
Utamu wa embe dodo, nawaambia vijana,
Ni embe lisilo nyodo, mfano wake hakuna,
Hamuye ninayo bado, kwa mengine mimi sina,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!

Nilipoona bolibo, nilidhani nimepata,
Nikalipigia chabo, tamaa ikanikuta,
Sikutaka embe robo, lilo zima nikang’ata,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!

Mdomo nikajilamba, bolibo nikisifiya,
Na wimbo nikauimba, utamu nikisikiya,
Na mguno kama komba, mtini akirukiya,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!

Harufu nikanusiya, embe dodo li mtini
Hamu ikaniingiya, bolibo sikutamani,
Haraka nikakimbiya, nisiingizwe mjini,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!

Mwili ukinitetema, nikashika mkononi,
Huku miye ninahema, dodo embe la thamani,
Nikaliminya kupima, jinsi lilivyo laini,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!

Kwa upole nikamenya, dodo nililotungua,
Na kidole kikapenya, nikaanza kutumbua,
Bolibo sikuyasanya, madodo nikachukua,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!

Kufurahia utamu, ni kufyonza kokwa lake,
Dodo litakupa hamu, mengine usiyatake,
Mimi leo ni mwalimu, mengine yana makeke,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!

Beti zangu nazifunga, embe langu najinoma,
Madodo hasa ya Tanga, hakika hayana noma,
Mdudu hatanivunga, na wala sitamtema,
Nimekula embe dodo, bolibo sitaki tena!!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
 
Mahenga wa kaskazi, umerudi kujitia
Kundini kuweka wazi, mambo yakuburudia
Ila mimi nina kazi, ya wewe kufaidia
Dodo hilo limeoshwa, au walifakamia?

Ashakum si matusi, bora ni kuhabarisha
Dodo ukinyonya kusi, kaskazi waharisha
Domo kufanya chunusi, jaribu kama wabisha
Dodo hilo limeoshwa, au walifakamia?

Ama walifakamia, dodo hilo limeoshwa?
Kulitoa kwa gunia, gengeni halitatoswa
Nyani wangejivunia, mwembeni wasingekosa
Dodo hilo limeoshwa, au walifakamia?

Kula dodo lina yule, mdudu kifaurongo
Ukimnyonya tawire, takufa hata ubongo
Hutofika hata Bwire, tutakuweka udongo
Dodo hilo limeoshwa, au walifakamia?

Pundit (Mjini Shule)
 
Embe dodo embe dodo, wanivutia miye dogo,
Zangu toka soko, narudi nimejawa mikoko,
Tele ni majigambo, yangu leo uhondo,
Menya yajipe mambo, napigwa ganda la kisogo,
Langu embe dodo, limejawa nyodo.​

Nyodo zimejaa, kwenye langu dodo,
Utashi si masikhara, nikalimbembeleza kidogo,
Ukubwa ni jalala, nikaushitukia unoko,
Langu embe dodo, limejawa nyodo.​

Nyodo zaliandama, langu embe dodo,
Uwele si mtama, kulichambulia ubongo,
Bariadi mpaka Kahama, kujirudi miye usongo,
Langu embe dodo, limejawa nyodo.​

Nyodo zitaliponza, sifa bado kemkem,
Mwanga si Mwanza, libishi kama Sisiem,
Kuangamia nikakuwaza, ahueni kulitosa sehemu,
Langu embe dodo, tele limejawa nyodo.​

Kokwa sitanyonya, mchangani nimelidondosha,
Siupendi umatonya, mkakamavu ng'wanangosha,
Baadhi walinitonya, yangu majuto kuepusha,
Langu embe dodo, tele limejaa nyodo.​

SteveD. (Mwangwi wa Handaki)​
 
duh... naona embe "limezua" mambo... kapinga ushindwe mwenyewe, Pundit once again..you amazes me.. Steve... I like the free style!! keep up..
 
Embe dodo lasifiwa, shairi likitungiwa
Kwa mbwembwe likiimbiwa,na malenga wenye kujua
Kwa wengine lasifiwa, kwa wengine limevundwa
Malenga naomba juvwa, Ni nini hili embe dodo?

Malenga naomba juvwa, embe dodo hili ni nini
Ni lile lililovundikwa, au liloiva mtini
Mwanakijiji hebu fumbuwa, umesifia kwa yanini
Malenga naomba juvwa, Ni nini hili embe dodo?

Pundit watia shaka, juu usafi wa embe dodo
Mwanakijiji kafamika, na uchafu wa embe dodo?
Steve D achefuka, na embe dodo lenye nyodo
Malenga naomba juvwa, Ni nini hili embe dodo?
 
Si lazima liwe tamu hilo unalosifia
Ulikuwa tu na hamu na njaa ilovilia
Maembe ni mengi humu tena yalo asilia
Si lazima liwe dodo laweza kuwa ng'ong'o

Utamu hutegemea ni vipi unalilamba
Jinsi ganii wahemea embe lako kulikomba
Vile we utavyokemea jirani wakikuomba
Si lazima liwe dodo laweza kuwa ng'ong'o

Kula embe ni ujuzi ili upate utamu
Kunahitaji miluzi kuzidisha yako hamu
Ukifanya upuuzi hutopata yake tamu
Si lazima liwe dodo laweza kuwa ng'ong'o

Waweza pia kuruka kuimba au kucheka
Waweza kulipapasa kabla hata hujalishika
Hauhitaja haraka kwani laweza kasirika
Si lazima liwe dodo laweza kuwa ng'ong'o

Embe likate kwa ufundi katu usiwe na haraka
Lisiliwe kwa makundi peke yako we hangaika
Uwe ni wako ushindi wa kulipata kwa hakika
Si lazima liwe dodo laweza kuwa ng'ong'o

Namaliza kwa kusema sichague aina ya tunda
Mengi ni matamu hima kama tu utayapenda
Ulipe wako mtima sithubutu kulitenda
Utamu wa embe ni wewe, jinsi gani walitenda



Kinyau original​
 
pundit, you made my day. Nice work, nice challenge to all those wanting to eat embe unwashed.
SteveD, Mwanakijiji, ndege ya uchumi,kapinga and mbarikiwa Good work and keep it up.
 
Hii inanikumbusha akia mzee Andanenga, mnamkumbuka huyu mzee? Yuko wapi sasa hivi
 
Bolibo tena hutaki, bayana umeyanena,
Dodo umelimiliki, hutaki tena ya jana,
Kwa dodo huambiliki, mengine hujayaona,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.

Samaki ulimleta, JF uwanjani,
Na sifaze ukateta, harufu iso kifani,
Hatimaye ukajuta, ulimleta kwanini,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.

Kijijini wanicheka, na wengine wanong"ona,
Na hamu imenitoka, njaa bado ninaona,
Kipande kimedondoka, miye simtaki tena,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?

Ulisema humtaki, kumbe ajenda ya siri,
Ukatutia mikiki, vishindo kikiri kikiri,
Oooh, huyu samaki, kwa harufu kakithiri,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.

Njaa imenizidia, ubishoo nauvua,
Samaki aniitia, mwenzenu nimeamua,
Nitamla naapia, magwiji nimeng'amua,
Maji nimeyavulia, sina budi kuyaoga.

Pamoja na uvundowe, umesema utamla,
Jibu tena usipewe, umefunga mjadala,
Umeshikwa na kiwewe, umeishiwa na hila,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.

Sasa ni zamu ya dodo, yu wapi yule samaki,
Umeuacha mpodo, umeshika msuaki,
Ana ana anado, utakosa tahamaki,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.

Mzee sinichukie, najifunza hapa hapa,
Mazuri uyachukue, mabaya waachie papa,
Nami usiniachie, pale nilokwenda kapa,
Dodo na yule samaki, kipi kitamu sana.
 
Dodo limezidi hamu, samaki sitaki tena,
Dodo hili tamutamu, vya bahari hamu sina,
Dodo nalikiri humu, ngisi pweza nawakana,
Dodo la leo adhimu, vilosusa ni vya jana,
Dodoe langu ni tamu, ni tamu kama sukari!

Dodo langu nalimenya, vidoleni nalishika,
Dodo hilo nalipenya, kwa kisu cha uhakika,
Dodo ninalimumunya, ulimini lalambika,
Dodo linanitekenya, akili zimeniruka,
Dodoe langu ni tamu, ni tamu kama sukari!

Dodo nimelisafisha, silili lililo chafu,
Dodo natanaibisha, ndilo embe maarufu,
Dodo msitake bisha, napenda yake harufu,
Dodo roho lanikosha, hapa nawataarifu,
Dodoe langu ni tamu, ni tamu kama sukari!

Dodo si kama bolibo, si ng'ong'o nakuambia!
Dodo siite ni bibo, ni onyo nakuusia,
Dodo silili kwa robo, jizima nafakamia,
Dodo hatui ndorobo, tunda langu nalindia,
Dodoe langu ni tamu, ni tamu kama sukari!

Dodo peke sitamani, mawili nashikilia,
Dodo moja li kinywani, jingine nakumbatia,
Dodo hilo ulimini, kiufundi nang'atia,
Dodo naapa yamini, kamwe siyaachia,
Dodoe langu ni tamu, ni tamu kama sukari!

Dodo nimelisifia, mwenzenu sasa nayeya,
Dodo nalifurahia, silili tena kwa puya,
Dodo nimeliwazia, kama awazavyo yaya,
Dodo nawatangazia, nakwenda kama napweya,
Dodoe langu ni tamu, ni tamu kama sukari!
 
Hii inanikumbusha akia mzee Andanenga, mnamkumbuka huyu mzee? Yuko wapi sasa hivi

Ustaadh Amiri Sudi Andanenga "Sauti Ya Kiza" Mzee wa Kinondoni Shamba ameandika kitabu "Diwani ya Ustadh Andanenga".Yuko involved katika shughuli za the visually impaired na mambo ya jumuiya ya wazazi CCM.
 
Mzee huyu kwa kweli ni kioo cha ushairi na ushauri... mojawapo ya mashairi yake niyapendayo sana ni lile lisemalo "Nyege ni kunyegezana".. watu walidhani anatukana!
 
Dodo halinyonywi, dodo linaliwa. Zinyonywazo ni boribo na sindano.
 
Nautambua uwepo, wenu wanamalenga.
Mimi kwenye embe sipo, haswa yakutoka Tanga.
Mwenzenu napenda epo, ninalila kwa kuringa.
Embe hata liwe zuri, ndaniye kunamdudu.

Siwezi fata upepo, kusifu bila kupinga.
Tena epo likiwepo, kwangu dodo huwa chunga.
Nasema nitamanipo, epo ndio yangu kinga.
Embe hata liwe zuri, ndaniye kunamdudu.

Nimesha kula kiapo, kwa epo nimejifunga.
Kwenye trei mahalipo, dodo ni lakwenye tenga.
Sitaki kuwa popompo, vyamaradhi kuvimanga.
Embe hata liwe zuri, ndaniye kuna mdudu.
 
5 Reactions
Reply
Back
Top Bottom