Utafiti: Wanawake wanaongoza kwa utegemezi Tanzania

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,119
1689220376547.png

Wakati jitihada mbalimbali zikifanywa na Serikali na sekta binafsi katika kuwainua wanawake kiuchumi nchini, ripoti mpya ya Wizara ya Fedha inaonyesha jinsia hiyo bado inaongoza kwa utegemezi.

Ripoti hiyo inayohusisha ujumuishi wa masuala ya kifedha kwa wananchi inayoitwa Finscope 2023 imeonyesha idadi kubwa ya watu tegemezi na wasio na shughuli inayowaingizia kipato nchini ni wanawake.

“Katika Watanzania 10 tegemezi, saba ni wanawake (waliofikia umri wa kufanya kazi),” imesema ripoti hiyo inayotolewa kila mwaka.

Aidha, kwa ujumla ripoti hiyo inaonyesha kiwango cha Watanzania tegemezi kimeongezeka kwa asilimia tano ikilinganishwa na mwaka 2017.

“Kiwango cha Watanzania tegemezi (wasio na shughuli zinazowaingizia kipato) kimeongezeka ndani ya miaka sita, kutoka asilimia 18 mwaka 2017 hadi asilimia 23 mwaka 2023,” imeeleza ripoti hiyo.

Wakati utegemezi ukizidi kuongezeka kadri miaka inavyokwenda, pia shughuli ya kilimo na uvuvi ambayo iliajiri vijana wengi nayo imezidi kupoteza mvuto kwa kundi hilo ambapo idadi ya waliojiajiri huko imepungua kwa asilimia 13.

“Mwaka 2017, asilimia 41 ya Watanzania walikuwa wanapata kipato chao kupitia kilimo na uvuvi, idadi hiyo imepungua hadi asilimia 28 mwaka 2023,” sehemu ya ripoti hiyo imesema.

Kwa upande wake, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema mfumo wa maisha ndio unamfanya mwanamke aonekane tegemezi.

“Utegemezi wa wanawake katika uchumi unategemea na muktadha, mara nyingi tunawaona ni tegemezi kwasababu shughuli wanazofanya nyingi hatuzibadilishi kuwa fedha na huo ndio udhaifu wa kipimo hicho,” amesema.

“Japokuwa kweli utofauti upo na wanawake wengi hawana kipato lakini je, siku tukiamua kuwalipa fedha kwa kazi za nyumbani wanazozifanya hawatakuwa na tija?” Amehoji Kinyondo.

Kuhusu suala la Watanzania wengi kuhama kutoka kutegemea kipato katika sekta ya kilimo na kuhamia sekta nyingine, Profesa Kinyondo amesema itakuwa na tija endapo sehemu wanazokimbilia zina ahueni ya kiuchumi.

“Kitaalamu inaitwa mapinduzi ya uchumi (economic transformation) ambapo watu wanatoka katika shughuli moja ya kuingiza kipato kwenda nyingine. Hii inaleta tija kama sehemu ambayo unahamia ina mzunguko mzuri zaidi wa kiuchumi,” amesema.

Pia, Profesa Kinyondo ameongeza kuwa bado katika nchi nyingi zinazoendelea kuna ‘pre-mature economic transformation’ ambapo mtu anahama shughuli moja kwenda shughuli nyingine ambayo bado haimpatii kipato kizuri, jambo alilolitaja kuwa na athari katika uchumi.

Hoja ya wanawake kuwa tegemezi imeangaliwa kiutofauti na Mwanaharakati wa haki za wanawake, Naima Hussein ambaye amesema bado hakuna fursa sawa za kiuchumi ndio maana kundi hilo linakuwa tegemezi.

“Huwezi kutegemea mwanamke aache kuwa tegemezi wakati bado kuna fursa za muhimu ananyimwa ikiwemo elimu kutokana na mila na tamaduni ya baadhi ya maeneo,” amesema Naima.

Aidha, ameshauri Serikali kuendelea kutoa fursa za kiuchumi na kisiasa kwa wanawake ili kufikia azma ya kuwa 50 kwa 50 katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Utafiti huu wa Finscope 2023 umehusisha watu 9,915 ambao kati yao asilimia 52 ni wanawake na asilimia 48 ni wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 16.

MWANANCHI
 
Kuna uzi humu unasema 90% ya wanawake Tanzania ni omba omba.. naona sasa umekuwa backed up na research.
Shida hata wale wanaofanya kazi bado ni tegemezi,na kama % za utegemezi zinazidi kuongezeka kujikwamua na umaskini itabaki kuwa ndoto.
Tanzania watu wachache sana wanafanya kazi ili wengi wanufaike,unakuta mtu mmoja nyuma yako una msusuru wa watu wanakupiga mizinga nonstop.
Dawa ni kukata mirija tu kwa watu waliofikia umri wa kufanya kazi, tutapiga hatua kama taifa kila mtu akifanya kazi,na sio kwa hali ya sasa ilivyo.
 
Back
Top Bottom