Utafiti wa tamwa Zanzibar wabaini kasoro, ufanisi mahakama maalum ya udhalilishaji zanzibar

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
ZAYNA.JPG
ZANZIBAR

SERIKALI imeshauriwa kukarabati na kuboresha miundombinu ya Mahakama maalum ya udhalilishaji Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwezesha matumizi ya ushahidi wa kielektroniki hasa kwa kesi zinazohusu watoto ili kuwa rafiki kwa wanaotumia mahakama hizo na kuwezesha upatikanaji wa haki katika mazingira bora.

Wito huo umetolewa na wadau wa kupinga udhalilishaji Zanzibar wakati wa mkutano wa kuwasilisha ripoti ya ufanisi wa Mahkama Maalum katika kushughulikia kesi za Udhalilishaji tangu kuanzishwa kwake ulioandaliwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Foundation For Civil Society (FCS) na Ubalozi wa Norway uliolenga kujadili mstakabali wa watoto kulindwa dhidi ya vitendo hivyo.

Kwa mjibu wa ripoti hiyo, imeelezwa kuwa licha ya mahakama hiyo kuonesha mafanikio makubwa ya usikilizaji wa kesi tangu kuanzishwa kwake lakini bado miundombinu haitoshi kutokana na kukosekana kwa vyombo vya kisasa vya usikilizaji wa kesi, ikiwemo mifumo ya kidigitali (video conference) na ukosefu wa vyumba maalum vya kuwaweka watoto walioathirika na vitendo hivyo.

Hawra Shamte, ambaye ni mtafiti wa utafiti huo uliofanywa na TAMWA ZNZ kati ya Juni 16 na Julai 16, 2023 kwa kuzihusisha Shehia 57 Unguja na Pemba alisema, “ukosefu wa vifaa katika mahakama na miundombinu duni bado ni changamoto, mfano majengo ya Mahakama ya Vuga, Mahonda, Mkoani na Wete Pemba ni ya zamani na karibu kupitwa na wakati wakati jambo linalopelekea ugumu katika uendeshaji wa kesi hizo.”

Aidha alieleza utafiti umebaini miongoni mwa mafanikio ya uwepo wa mahakama hiyo ni pamoja na kuongeza kasi ya usikilizwaji wa kesi za Udhalilishaji katika mahakama hizo.

"Wahojiwa walisema mahakama hii maalum ya Udhalilishaji inaonesha siku hizi kesi za aina hii zinachukuliwa kwa uzito mkubwa na hata hukumu zinazotolewa si ndogo kama ilivyokuwa awali, siku hizi utasikia mtu anapewa kutoka kifungo cha miaka 20 hadi miaka 30 na pia wapo waliopewa kifungo cha maisha," alieleza Hawra.

Kutokana utafiti kubaini miongoni mwa changamoto zinazozuia ufanisi wa mahakama hizo ni kesi nyingi zinazowahusisha vijana wenye umri wa kuanzia miaka 14 hadi 18, waathiriwa kushindwa kutoa ushirikiano katika kutoa ushahidi, utafiti umeshauri serikali kuongeza vifaa vya upelelezi ili kuwezesha uchunguzi kukamilika mapema kuepukana na mashahidi vigeugeu.

“Tunapendekeza serikali kutoa vifaa vya kutosha kwa idara ya polisi ili kuwawezesha ufanisi katika kufanya uchunguzi bila kuchelewa ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuwezesha matumizi ya ushahidi wa kielektroniki kwenye kesi hizi,” alisisitiza mtafiti huyo.

Mratibu wa miradi ya kupinga udhalilishaji TAMWA ZNZ, Zaina Salum, alieleza TAMWA ZNZ katika kuendelea na kampeni ya kupaza sauti ya Haki za Watoto dhidi ya matukio ya ukatili kinafanya tafiti mbalimbali ili kukuza uchechemzi wenye kuchochea mabadiliko chanya kwenye masuala hayo.

Zaina alieleza, “TAMWA ZNZ tumekuwa tukifanya uchechemzi wa masuala mbalimbali yanayohusu vitendo vya udhalilishaji kupitia tafiti na kuzifikisha kwa taasisi na wadau husika kuzifanyia kazi ili kuisaidia jamii kuondokana na tatizo hili.”

Mapema mwenyekiti wa TAMWA ZNZ, Asha Abdi, alishauri jamii kuwapa nafasi watoto kuchangamana na watoto wenzao kupitia majukwaa mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa uthubutu na ujasiri wa kuzungumza changamoto na fursa zinazowakabili na kuwalinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

Alisema iwapo watoto watapewa fursa sawa na wazazi kushiriki kamilifu katika majukwaa yao ikiwemo mabaraza ya watoto kuanzia ngazi ya shehia itawajenga kukua katika misingi ya ujasiri na kukuza uwezo wa kukabiliana na vikwazo mbalimbali vinavyo kandamiza haki zao.

Alitaja watoto wa kike wanakosa haki zao ikiwemo haki ya uongozi kutokana na kukosa misingi ya kushirikishwa katika majukwaa yao kuanzia ngazi ya awali yanayowajenga kutambua fursa na haki zao muhimu.

“Wazazi tuwaruhusu watoto wetu hasa wa kike wachangamane na watoto wenzao kupitia mabaraza ya watoto ili wapate fursa ya kuzungumzia mambo yao yanayowahusu na hii itawasaidia kuwajengea ujasiri wa kuzungumza kwa uwazi changamoto zao,” alieleza mwenyekiti huyo.

Wilfred Ezra, ambaye ni afisa uchunguzi kutoka Tume ya Haki za Binaadam na Utawala Bora alishauri jamii kuendelea kutoa taarifa za matukio ya udhalilishaji yanapotokea ili kusadidia kuwalinda watoto na kuwadhibiti watekelezaji wa vitendo hivyo.

Nae Thuwaiba Ali, mmoja wa wanafunzi walioshiriki mkutano huo aliomba serikali kuongeza adhabu kali kwa watekelezaji wa vitendo vya ukatili ili adhabu hizo ziwe onyo na tishio kwa wenye tabia hizo zinazokiuka haki za binaadam.

"Serikali iweke adhabu kali kwa wanaofanya vitendo vya udhalilishaji ili kuwatisha wengine kuendelea kufanya vitendo hivyo kasababu wengi wanaendelea kutufanyia udhalilishaji kutokana wanajua hata wakifungwa wataachiwa kwasababu hakuna adhabu kali," alieleza mwanafunzi huyo.

Ayoub Nassor Sharif kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka alipongeza TAMWA ZNZ kwa kuendelea kuwaunganisha wadau kupaza sauti dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na kushauri kuendelea kutoa elimu kwa jamii kutambua umuhimu wa kuwenda kutoa ushahidi mahakamani ili watuhumiwa wachukuliwe hatua kisheria.

Aliomba, “TAMWA iendelee kuhamasisha jamii kuja kutoa ushahidi mahakamani pale wanapohitajika kwani ni kweli kesi nyingi zinafutwa kutokana na kukosa ushahidi na kama ambavyo tunafahamu hakuna kesi bila ushahidi.”

Mkutano huo ambao umeandaliwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Foundation For Civil Society (FCS) na Ubalozi wa Norway umewashirikisha wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali na kiraia wakiwemo mahakimu, waendesha mashtaka, viongozi wa dini, walimu, wanamtandao wa kupinga udhalilishaji na maafisa ustawi wa jamii ambapo nimwendelezo wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike.
 
Back
Top Bottom