SoC02 Utafiti na Maendeleo Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

Njokaki

New Member
Aug 24, 2022
1
0
Utafiti na Maendeleo Tanzania

A
ndiko hili limejikita katika kuangazia sekta ya utafiti nchini hasa kwa kuonesha changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kuchukua hatua dhidi ya changamoto hizo. Utafiti ni moja ya kichocheo kilichochangia maendeleo ya dunia. Hii ni kutokana na mchango wake mkubwa katika nyanja mbalimbali kama; elimu, afya, kilimo, uchumi na teknolojia.

Utafiti umetumika katika kubaini matatizo na kupendekeza suluhu ya matatizo hayo. Pia utafiti umetumika kutabiri matokeo mbalimbali yanayoweza kujitokeza kwa wakati ujao. Nchi nyingi zilizoendelea zimewekeza katika utafiti na matokeo yake yamekuwa chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi hizo.

Nchi hizo ziliweza kuwekeza sehemu kubwa ya pato lao la taifa wa ajili ya maendeleo. Ripoti ya benki ya dunia ya mwaka 2018 inaonesha Switzerland, Korea Kusini na Israel kama nchi zinazoongoza kwa kutenga zaidi ya asilimia moja ya pato lake kwa ajili ya utafiti na maendeleo. Na ripoti hiyo inaonesha nchi hizo zimeweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na uwekezaji wake mkubwa katika utafiti. Wakati nchi mbalimbali barani Ulaya na Asia zikionekana kuwekeza katika utafiti kwa kiasi kikubwa, nchi za bara la Afrika bado uwekezaji wake ni wa kiwango cha chini.

Pamoja na makubaliano ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2006 yaliyofanyika Khartoum,Sudan ya nchi wanachama kutenga asilimia moja ya pato la taifa kwa ajili ya utafiti na maendeleo, ni nchi chache tu ambazo zimeweza kuwekeza kwa zaidi ya nusu ya makubaliano hayo. Kwa mujibu wa ripoti ya UNESCO ya mwaka 2021, nchi hizo ni Kenya iliyowekeza kwa 0.8 %, Afrika Kusini kwa 0.75% na Misri kwa 0.6% na nchi nyingine zilizobaki bado ziko chini ukilinganisha na nchi nne zinazoongoza.


1661779674493.png

Picha kwa hisani ya mtandao wa heritage.org

Tanzania kama nchi nyingine duniani ilitambua umuhimu wa utafiti katika sera yake ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996. Katika sera hiyo, moja ya malengo ya sera hiyo ni kuwekeza kwenye utafiti kwa asilimia moja ya pato la taifa. Ili kuweza kufikia malengo yake, Tanzania iliweza kuanzisha taasisi mbalimbali za utafiti nchini katika sekta mbalimbali. Na uwepo wa taasisi hizo umekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi kwa kutatua matatizo mbalimbali kupitia tafiti ambazo zimekuwa zikifanyika na kutoa mwongozo au ushauri kwa masuala mbalimbali nchini. Kwa mfano, Taasisi ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ni baadhi ya taasisi zilizoanzishwa na serikali na taasisi hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya na kilimo.

Pamoja na jitihada za serikali za kuanzisha taasisi mbalimbali za utafiti na mchango mkubwa ambao umekuwa ukitolewa na taasisi hizo kwa maendeleo ya taifa bado uwekezaji katika sekta ya utafiti ni mdogo ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika ambazo zimeweza kuvuka nusu ya 1%. Kwa mujibu wa UNESCO Tanzania imewekeza 0.5% ya makubaliano ya Umoja wa Afrika ambayo ni kuwekeza 1% ya pato la taifa. Pamoja na kiasi hicho cha uwekezaji, sekta ya utafiti bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Kwa mujibu wa ripoti ya SRIA-Programme ya mwaka 2019 iliyofanya tathmini juu ya mahitaji ya mfumo wa utafiti Tanzania, ripoti hiyo iliweza kubaini changamoto mbalimbali.

Kwanza ni kutokuwepo kwa mfumo kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa ndani wa utafiti. Serikali haijaweka mazingira wezeshi kwa ajili ya mfumo wa ndani wa shughuli za utafiti na badala yake shughuli hizo zimekuwa zikifanywa na wafadhili kutoka nje. Pili, kutokuwepo kwa miundombinu inayotosheleza kwa ajili ya shughuli za utafiti. Mazingira ya kufanyia utafiti sio rafiki kwa sababu ya uhaba wa miundombinu mbalimbali ambayo ni muhimu katika kufanya shughuli hizo.

Changamoto nyingine ni uwezo mdogo wa kufadhili shughuli za utafiti. Kutokana na kiwango kidogo cha fedha kinachotengwa na serikali kwa ajili ya shughuli za utafiti, kiwango hicho kimekuwa hakitoshelezi mahitaji. Wakati mwingine taasisi za utafiti zinashindwa kutekeleza majukumu yake au kutegemea ufadhili kutoka nje. Ripoti ya SRIA Programme ya mwaka 2019, inaonesha Tanzania imekuwa ikifadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA) na Benki ya Dunia.

Mbali na hiyo changamoto, bado uwezo wa kuwajengea uwezo watafiti ni mdogo. Watafiti hawapati mafunzo mbalimbali yakutosha ya kujengewa uwezo ili kuimarisha uwezo wao katika kufanya shughuli zao za utafiti.

Pamoja na jitihada za serikali kutambua umuhimu wa utafiti na kuanzisha taasisi mbalimbali za utafiti, sekta ya utafiti inakabiliwa na uhaba wa watafiti. Kwa mujibu wa ripoti ya SRIA- Programme 2019, Tanzania inakadiliwa kuwa na watafiti 18.3 kwa watu milioni moja. Kwa mujibu wa viwango vya UNESCO, hiki ni kiwango kidogo kwa nchi kwani kwa Afrika inatakiwa kuwa na wastani wa watafiti 95.1 kwa watu milioni moja.

Pia tafiti zinazofanyika bado hazifanyiwi kazi. Inaonekana pamoja na taasisi nyingi kujitahidi kufanya tafiti katika sekta mbalimbali lakini matokeo ya tafiti hizo yamekuwa hayafanyiwi kazi kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika nchini na kubainisha changamoto kwenye ripoti mbalimbali, basi serikali inalo jukumu kuhahikisha inafanyia kazi changamoto hizo zilizoibuliwa kwenye ripoti mbalimbali. Kuna ushahidi wa wazi kuwa kuna mahusiano makubwa kati ya utafiti na maendeleo. Utafiti uliofanyika mwaka 2003 kwa baadhi ya nchi za bara la Asia (Asian Tiger Countries) ulionesha katika matokeo yake kuwa uwekezaji katika utafiti umekua kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika nchi hizo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID) ya mwaka 2014.

Vilevile katika sayansi ya sera za umma kuna ushahidi kuwa utafiti ni nguzo muhimu katika kutunga sera ambazo zinaweza kuwa na matokeo chanya kwa taifa. Kwa ushahidi huu basi serikali haina budi kulichukulia suala hili kwa uzito zaidi ili kuweza kupiga hatua kwenye sekta mbalimbali.

Kwa kuhitimisha, andiko hili linapendekeza serikali kuendelea kuwekeza katika sekta ya utafiti kwa kutenga kiasi cha fedha cha kutosha kwa ajili ya utafiti na maendeleo kama makubaliano ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2006 yanavyoelekeza, kuweka mfumo na kuuimarisha kwa ajili ya shughuli za ndani za utafiti, kuboresha miundombinu kwa ajili ya shughuli za utafiti, kuwajengea uwezo watafiti wa ndani mara kwa mara, kuanzisha mfuko maalum wa fedha kwa ajili ya utafiti, kufanyia kazi kwa kiasi kikubwa matokeo yanayotokana na tafiti zinazofanyika na kuendelea kuajiri watafiti.

Imeandikwa na,

Njokaki, ambaye anapatikana katika mtandao wa Twitter kwa jina la @Chagulanishabie
 
Back
Top Bottom