The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,801
Ustahimilivu wa Digitali.jpg

Kadiri muda unavyokwenda teknolojia za kidigitali zinaendelea kuyafikia maeneo mengi ya maisha ya watu. Sasa hivi watu huchangamana na kufanya kazi katika mazingira ya kidigitali.

Kutokana na ukweli huo, watu wanakumbana na wataendelea kukumbana na mabadiliko na misukosuko wakati wa shughuli zao na haiwezekani kuwakinga kabisa dhidi ya changamoto wakati wa kutumia zana za kidigitali. Hata hivyo, kujifunza kuwa mstahimilivu kwa hali ngumu ni sehemu muhimu ya maendeleo ya mtu binafsi.

Ustahimilivu wa digitali (digital resilience/resilience in the digital era) ni uwezo wa kujikwamua kutoka nyakati ngumu anazopitia mtu mtandaoni kama vile kuonewa, kutukanwa, kubaguliwa n.k. Ustahimilivu pia unaweza kuwa ni hali ya kukubali na kujifunza kutumia mapinduzi ya kidigitali kwa kujiamini.

Ustahimilivu huu unajumuisha kuwa na uwezo wa kuelewa unapokuwa hatarini mtandaoni, kujua la kufanya ikiwa utakutana na mabadiliko usiyoyatarajia, kujua la kufanya ikiwa jambo lolote haliendi vizuri, kujifunza kutokana na unachopitia, na kuweza kupona kutokana na misukosuko.

Kwa hivyo, ni lazima kila mtu akuze ustahimilivu wa digitali— yaani ufahamu, ujuzi, wepesi, na ujasiri unaohitajika ili kuwawezesha watumiaji kushiriki kikamilifu katika jamii, na kukabiliana na mahitaji yanayobadilika kila mara.

Watu ambao watajifunza ustahimilivu wa digitali wataweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa kisasa ambao unazaidi kuwa wa kidijitali kila siku. Ustahimilivu huu hukua kupitia matumizi, uzoefu (experience) na kujifunza – kamwe hauwezi kuendelezwa kwa kuepuka matumizi ya digitali.

Kwa mfano, hauwasaidii watoto wako kustahimili changamoto za digitali kwa kuwaweka mbali na mtandao. Ni lazima kuwafundisha namna ya kupambana nazo kwa njia sahihi kwani kumkataza ni kumnyima haki yake ya msingi.

Unaweza kuwasaidia kwa kuwarahisishia kuzungumza nawe kuhusu changamoto zao, kuhakikisha kwamba wanajua mahali pa kupata usaidizi ikiwa wana uhitaji, na kutambua ikiwa wanapitia changamoto fulani ili uweze kuingilia kati na kuwasaidia kupata usaidizi.

Ili kuhakikisha watu wanapata ustahimilivu huu, ni lazima kuwepo na programu ambazo zitamsaidia kila mmoja kupata elimu itakayomuwezesha kufurahia maisha katika zama hizi. Kushindwa au kutotumia nyenzo na fursa za kidigitali ni kunyimwa/kujinyima haki ya msingi.
 
Back
Top Bottom