Ni Muhimu kwa Kila Kampuni na Shirika Kuwa na Mkakati wa Kustahimili Changamoto za Teknolojia ya Digitali

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
603
1,760
Ustahimilivu wa Digitali kwa Mashirika na Makampuni.jpg

Tunaishi katika ulimwengu wa kidigitali unaozidi kukua kwa kasi, lakini makampuni na mashirika mengi bado hayafahamu ni kwa kiwango gani yanategemea teknolojia ya digitali na changamoto ambazo wanaweza kukumbana nazo. Tunapoelekea katika siku zijazo ambazo tunazidi kuwa tegemezi kwa teknolojia ya digitali, hitaji la ustahimilivu kwa makampuni na mashirika nalo linazidi kuwa kubwa.

Ustahimilivu wa digitali (digital resilience/resilience in the digital era) ni uwezo wa kampuni au taasisi kufanya kazi wakati changamoto zinapotokea. Huwezesha makampuni na mashirika kusalia katika utendaji, kupunguza au kuondoa madhara kwa wateja/wadau, kupunguza au kuondoa kabisa uharibifu wa sifa ya kampuni/taasisi, na kuepuka hasara za kifedha wakati wa changamoto hizo.

Ustahimilivu ni mojawapo ya sifa muhimu zaidi kwa shirika au kampuni. Hii inamaanisha uwezo wake wa kukua na kuishi (survive) katika mazingira yanayobadilika kwa kutekeleza kwa ufanisi mikakati ya ulinzi wa taarifa na mifumo, kukuza ujuzi endelevu kwa wafanyakazi na wadau, na utatuzi wa changamoto zozote zinazoweza kujitokeza. Makampuni na mashirika yenye ustahimilivu ni yale ambayo yamejitayarisha vyema kukabiliana na changamoto zilizo mbele yao.

Katika mazingira ya kidigitali yanayoendelea kubadilika, ni lazima mashirika na makampuni yawe na uwezo wa kusonga mbele kwa haraka na kwa urahisi kwa kutumia masuluhisho mapya (updated solutions) ya teknolojia ya digitali.

Taasisi hujenga uaminifu wa kweli kwa wateja/wadau wake kwa kuhakikisha usalama wa taarifa zao na huduma zilizo bora. Katika makala iliyochapishwa hivi karibuni na Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) inasema kuwa "…ustahimilivu wa digitali ni nyenzo muhimu sana katika kupata na kudumisha imani ya watu kwa kila taasisi duniani."

Kuunda mkakati wa kujiimarisha kidigitali katika kampuni au shirika ili kuongeza uthabiti kunahitaji viongozi kutambua na kuwa na kipaumbele cha kutengeneza mpango wa kupunguza au kuondoa athari zinazoweza kuletwa na changamoto za teknolojia ya digitali. Kwa mfano, taasisi ambazo zilikuwa na mkakati bora wa masuala ya digitali ziliathiriwa kidogo sana na janga la UVIKO-19; zile ambazo hazikujiandaa zilijikuta zikitetereka kiutendaji.

Mkakati wa kustahimili changamoto za kidigitali wenye mafanikio unapaswa kulenga kuimarisha uwezo wa watu, na si tu zana, intaneti au programu wanazotumia.

Kwa hivyo, ustahimilivu unaweza kupatikana kwa kuwa na wafanyakazi walio na motisha ambao wanawezeshwa kupata ujuzi mpya ili kukabiliana na changamoto mpya. Kwa kutoa mafunzo na kuweka mipango ya kuongeza ujuzi, kampuni au shirika linajiweka katika nafasi nzuri ya kukabiliana na changamoto zozote za kidigitali zinazoweza kutokea.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom