Wakuu Salaam.
Nikiri wazi, nimelazimika kuandika huu uzi baada ya mabishano makali kati ya roho yangu na kichwa changu; roho ikiniambia usiandike, na kichwa kikinilizamisha kuandika, hatimaye nimeamua kukipa kichwa ushindi hivyo kuamua kuandika.
Taarifa za viongozi wa Chadema kupigwa jana wakati walipokwenda kumchukua kiongozi wa chama Mh. Freeman Mbowe baada ya yeye kukamilisha taratibu za kulipiwa faini hazijanifurahisha, bado sijajua ni kwanini askari magereza waliamua kuwa "too harsh" kiasi cha kuwasababishia maumivu na majeraha katika miili yao.
Inaripotiwa kwamba, baada ya viongozi wa Chadema kufika maeneo ya gereza palitokea mabishano kati yao na askari magereza yaliyosababisha askari aliekuwa zamu kupiga filimbi ya kuashiria hali ya hatari, iliyosababisha askari wengine kufika eneo la hatari ili kuongeza nguvu kwa mwenzao, hili lilisababisha baadhi ya viongozi wa Chadema kupigwa na kuumizwa, ambapo sasa inaripotiwa wapo kituo cha polisi Stakishari.
Nikiri wazi, bado nasisitiza nguvu iliyotumika kuwatawanya viongozi wa Chadema na wapenzi wao ilikuwa kubwa kupitiliza, hasa ukizingatia waliotuhumiwa kufanya vurugu hawakuwa na silaha yoyote ambayo ingesababisha kuhatarisha hali ya amani kwa kiwango kikubwa, hivyo askari magereza walichokifanya hakika hakijampendeza mpenda haki yeyote, wapunguze matumizi ya nguvu kupitiliza.
Lakini pia nalazimika kuwashauri viongozi wa Chadema wawe makini hasa wanapofika maeneo nyeti kiusalama nchini, hasa wanapokwenda kuwachukua au kuwatembelea viongozi wao, gerezani in particular.
Sote tunafahamu unyeti wa maeneo ya magereza nchini, yanahitaji ulinzi na utulivu wa uhakika kwa muda wote wa masaa ishirini na nne kwa siku (24 hours a day). Hivyo nakuwa mgumu kuamini kwamba viongozi wa Chadema walipigwa tu punde baada ya kufika Segerea pasipo kupewa maelekezo yoyote ambayo naamini kwa namna moja au nyingine walikuwa wagumu kuyafuata, hali iliyosababisha wao kupatwa na majanga yaliyowafika.
Naamini kwamba, kama wangeonesha ushirikiano toka mwanzo kwa kutii maagizo na maelekezo waliyopewa, hali hii isingefikia hapa ilipofika ambapo tunaambiwa Mh. Esther Bulaya alipigwa mpaka kuzimia.
Hili lililowapata linasononesha mioyo ya wazazi, ndugu, jamaa, na marafiki wote wa viongozi wa Chadema nchini, hakuna anayependa kuona wakifikwa na madhila kama hayo yaliyowapata hapo jana, hivyo ni vyema kwa mtazamo wangu, viongozi wa Chadema wao binafsi, wawe wa kwanza kuchukua tahadhari kulinda usalama wao, badala ya kuacha kila jambo litokee bila kujali athari za kile kitachoweza kuwapata baadae.
Bado ninaamini, walikuwa na uwezo wa kumpokea Mbowe popote hata kilomita moja mbali na gereza, kwasababu kwanza alishaachiwa, pili nae alikuwa anaelekea maeneo ya makao makuu ya chama, hivyo kumuona Mbowe hiyo jana kwao ilikuwa ni lazima, bila kuathiri utulivu wa eneo la gereza kwa namna yoyote.
Ni vyema kila mtu achukue tahadhari kwa upande wake, kila mmoja popote alipo ajue anawajibika kulinda usalama wa mwingine bila kusababisha maumivu kwa yeyote.
Asanteni.
Sent using
Jamii Forums mobile app