SoC01 USHAURI: Serikali ijitahidi kuboresha huduma ili kaya maskini zinufaike

Stories of Change - 2021 Competition

Langlang

JF-Expert Member
Jul 29, 2021
256
239
Kuna watu wanatusimanga eti Tanzania ni nchi maskini, na watu wanaamini. Watu wanaishi mbali nje, na saa nyingine hawajawahi onana na wanaoitwa maskini wa Tanzania, lakini wanatusema. Wameweka vigezo waliovitunga wenyewe na kutuhukumu, eti vinatuhusu.

Hebu niambie, unapoambiwa ati wewe ni maskini, kipi kinachokujia akilini?Serikali yetu, kwa kutambua kuwa hakuna nchi isiyo na maskini wake, ilianzisha asasi iitwayo Tanzania Social Action Fund (TASAF) ambayo kazi yake kuu ni kusaidia kupunguza maumivu ya waTanzania maskini.

TASAF hapa nchini inashughulikia hao wanaoitwa kaya maskini na wanawalipa kiasi fulani cha fedha kila baada ya miezi miwili kwa ajili ya mahitaji mbalimbali na ya shule na matibabu kwa ajili ya watoto wao. Idadi ya wahitaji ambao wako TASAF katika eneo ninakoishi imefikia wanakijiji zaidi ya themanini. N

Imeambiwa vigezo vinavyotumikaili kustahili kuitwa kaya maskini ni pamoja na: Nyumba anayoishi isiwe na umeme wala maji. Asiwe anamiliki mifugo wala redioAsiwe na baiskeli wala chochote chenye kuonekana kuwa na thamaniIkiwa TASAF wamefanikiwa kupata watu wenye vigezo tajwa wa idadi hiyo, basi ni wazi kuwa kuna idadi kubwa ya maskini Tanzania kwa sababu ni kweli pia, waliopewa jukumu la kuwapata maskini hao watakuwa hawajasakanya maeneo yote.

Katika mradi huu, wahusika wanalipwa wastani wa Sh. 10,000/- kwa mwezi na tegemezi wasiozidi umri wa miaka 14 wanalipiwa Sh. 200/- kwakila mmoja kwa mategemeo kwamba zitapunguza magumu katika kutatua baadhi ya mahitaji muhimu.

Mwandishi mmoja wa fani ya Menejimenti– Abraham H. Maslow katika nadharia yake kuhusu motisha (A Theory of Human Motivation) aliwahi kuandika kuwa mwanadamu anao mpangilio wa mahitaji ambao anapofanikisha hitaji moja analohitaji linasita kuwa motisha ya maisha na badala yake linajitokeza jingine la juu zaidi.

Katika mpangilio huo yako mahitaji ya chini zaidi yanayomhusu maskini nayoni yale ambayo ni muhimu ili aishi,ikiwa ni pamoja na:Chakula na kinywaji (maji). Kwamba atatumia uwezo wake wote katika kutimiza hitaji lake la wakati, kwamba mtu mwenye njaa anatamani chakula,anaota chakula, anapata njozi za chakula, hadi atakapokipata.

Anapolipata anahangaikia lingine.Usalama. Kwamba anapokamilisha ngazi ya chini ya mahitaji, anakuwa na hitaji la usalama – wa kimwilina hata wa maisha.Kumiliki mali. Hata maskini anahitaji kumiliki mali bila kujali thamani ya mali hiyo – hata kitanda na godoro ni mali kwake.Mahali pa kulala. Kwamba maskini anahitaji maskani. Haijalishi thamani ya maskani hiyo ikoje.Afya. Kwamba anapougua aweze kupata matibabu.

Maskini wengi hupoteza maisha kutokana na kukosa matibabu muafaka.Mengine yanayomhusu mtu maskini ni pamoja naElimu.

Mfumo wetu unawasaidiaje maskini? Mafungu yanayotengwa ni kiasi gani kwa kila mwanafunzi? Tunao viongozi wengi wenye kusomesha watoto kwenye shule za binafsi na hata nje ya nchi.

Jiulize kwanini! Ninaye jamaa yangu mwenye matatizo ya umaskini ambaye mtoto wake alipangiwa shule ya Sekondari iliyoko Kigoma wakati yeye anaishi Arusha. Ikiwa iko database ya wanafunzi huko wizarani, kwanini impangie mtoto mahali mbali na nyumbani wakati upo uwezekano wa kumpangia karibu.

Kuna suala zima la magonjwa kama UKIMWI na sasa UVIKO ni balaa na hayachagui tajiri wala maskini. Yanapomkuta maskini hasa ukizingatia wengi hawana bima za afya, inakuwa jambo la kuhurumia – nani wa kumsaidia!

Nimewahi kutembelea baadhi ya nyumba vijijini nikakutana uso kwa uso na umaskini uliokithiri. Watoto hadi sita wanalelewa na bibi au babu, waliozaliwa na binti anayeishi mjini wakatelekezwa kwake/kwao.

Walezi hao hawana ajira wala kipato cha uhakika, wanalala kwenye godoro moja chini kwenye chumba kidogo cha udongo,Watoto ambao wazazi wao wamepoteza maisha kwa magonjwa (yakiwemo niliyoyataja), waliochukuliwa na jamaa zao ambao pia wanao watoto wao wa kuwazaa wenyewe.

Pia kaya hizi zinahudumiwa na wazazi/walezi ambao hawana ajira au kipato kinachoeleweka. Kitanda kimoja wanalala watoto hadi sita wa jinsi zote na mama mlezi.

Watoto wanaoishi na wazazi au walezi walevi, wasio na ajira wala kipato cha uhakika.Watoto waliozaliwa na mzazi mwenye mtindio wa ubongo au mwenye matatizo ya akili na ambao walezi wao hawana ajira wala kipato cha uhakika.

Wazazi/walezi wasio na kipato wanaoishi na watoto wenye matatizo ya kiafya ya aina mbalimbali.Baadhi ya wazazi/walezi hao ni wazee, walevi na wenye matatizo mengine mengi hata kama pia wanafaidika na mpango mzima wa TASAF. Mahitaji ya fedha ni makubwa.

Ukiangalia kwa juu juu, unaweza kushawishika kuwashutumu walezi/wazazi wa hizo kaya. Chukulia msichana mwenye akili timamu anatoka nyumbani, anabeba mimba anajifungua na kumtelekezea mzazi wake mtoto amlee.

Ukifuatilia utakuta watu hawa hawakomi. Baada ya muda anarudi tena nyumbani na kumwachia mzazi wake kajukuu kengine. Kwa upande mwingine ni kama vile mzazi wake kwa visingizio visivyoeleweka, wanawakubalia watoto wao, jambo linalowatumbukiza zaidi katika lindi la umaskini.

Baadhi yawanawake wanajiliwaza ati, Mungu aliwaambia…”Enendeni mkaijaze dunia…”, hivyo hawawezi kujizuia, hawajitathmini, hawajutii. Ni wazi kwamba masuala haya yanahitaji umakini fulani katika kuyashughulikia.Katika kuutangaza Utalii, Tanzania imetumia mbinu nyingi kuhakikisha watalii wanafurika kwetu.

Ili kufanikisha lengo hili, yapo mazingira ya aina mbalimbali yanayosaidia kufanikisha/au kukwaza juhudi hizo. Kwa mfano, barabara iingiayo katika hifadhi ya Tarangire, ina vumbi kupita kiasi na, bila kujali ni mtalii au mpita njia, kero ya vumbi inakukabili.

Pembeni ya barabara hiyo, unapotoka kutaalii, unakutana na idadi kubwa sana ya watoto wanaochunga mifugo ambao, kila mmoja kwa yake ananyoosha mikono/mkono wake akionyesha ishara ya kuomba na kutoa sauti akisema …”Tupaa…” akiwa anamaanisha urushe nje ya dirisha la gari, chochote – kiwe ni makombo ya chakula, au vinywaji.

Kuna wamama waliotokwa machozi. Ukiwaangalia unaona wazi kuwa wamekabiliwa na umaskini wa kweli. Kisha unajiuliza ikiwa kweli hakuna jinsi ambavyo jambo hilo linaweza shughulikiwa kutuondolea aibu hiyo! Viongozi hawaioni aibu hii?!TASAF wamejijengea jina katika kuhudumia kaya hizo kwa kadri ya uwezo wao, ambao ndio huo nilioueleza hapo juu. Ziko asasi nyingine pia zinazofadhili miradi ya aina hiyo.

Baadhi zinao uwezo zaidi ambapo zinafadhili hadi elimu ya watoto toka kaya maskini kwa kulipia mahitaji mbalimbali ya elimu kwa kadri ya uwezo wa watoto kujiendeleza. Wazazi wanashukuru. Serikali inalionaje hili?

Najaribu kutafakari jinsi ambavyo serikali inavyolishughulikia suala zima la umaskini. Ikiwa TASAF ni chombo cha serikali ni wazi kwamba jinsi wanavyohudumia maskini ndivyo ambavyo uwezo wa serikali unavyoliona suala zima la umaskini hapa nchini.

Kwamba hizo Sh. 20,000/- wanazopewa kila baada ya miezi miwili ndiyo uwezo wa serikali yetu katika kupunguza umaskini… yaani fedha hizo zitumike kwa miezi miwili na zikidhi mahitaji!

Kuna mambo Serikali inayafanya yanayoashiria kwamba serikali inaweza kufanya mambo makubwa zaidi. Kwa mfano:Mfumo wa mishahara ya viongozi unarandana na hali halisi ya nchi yenye umaskini wa kiwango chetu?

Hizo posho wanazojilipa zinazingatia uchumi na hali halisi ya umaskini wetu?Hayo marupurupu wapewayo, na wakati mwingine kuyaweka hadharani, yanawastahili ukizingatia wanaoitwa wanyonge walio na hali ngumu ni wengi wanayaona kila yanapoonyeshwa katika vyombo vya habari?Mipango ya muda mrefu na mfupi ina uelekeo wowote kuelekea kumkomboa maskini?

Tumekuwa tukisisitiziwa kuwa, kila Halmashauri inayo mipango ya kuwakopesha vikundi mbalimbali fedha zisizo na riba ili kupunguza umaskini na kuinua hali ya maisha ya Mtanzania na tumeona ni idadi na watu gani ni walengwa wanufaika.

Ipo Wizara yenye jina linaloashiria kuwa inahusisha masuala ya wazee. Nimeelezea hapo juu jinsi ambavyo wazee wamekuwa wanajihusisha na masuala ya familia mbalimbali wanavyohangaikia maisha ya familia zao vijijini.

Ni kwa jinsi gani wazee wamenufaika kutokana na uwepo wa hiyo wazara?Wakati umefika sasa kwamba, serikali ionyeshe dhamira ya dhati katika suala zima la kushughulikia umaskini, matamko hayatoshi.

Inapozungumzia maskini iwe na takwimu sahihi. Inapotoa mikopo kwa makundi mbalimbali, iwe na uhakika na inachotangaza, inapotoa misaada kama hiyo ya TASAF, misaada iwe na tija. Napendekeza pia, matumizi mbalimbali ya serikali hususan kwa baadhi ya watumishi wake isionekane kama kufuru.

Nimetoa mfano wa Tarangire kuhusu hao watoto ombaomba wanaorushiwa makombo ya vyakula wanavyokula watalii ambao, kwa kiwango kikubwa hawaonyeshi taswira nzuri kwa nchi yenye jina kubwa kama Tanzania.

Naamini inawezekana wako wengine wa aina moja au nyingine wa aina hiyo na kwa eneo tofauti. Wengi watakuwa wanaishi maeneo karibu na ambapo nchi yetu inapata mapato makubwa kutokana na miradi, uwekezaji na/au maliasili mbalimbali.

Itapendeza ikiwa maeneo hayo yataendelezwa – kwanza kwa sababu za kibiashara kama kuzitangaza lakini pia kuficha aibu yetu. Kurekebisha au kuboresha barabara iingiayo kwenye kivutio cha watalii, kuna faida kwa wakazi majirani na biashara yako pia.

Kwani kwa wanaonufaika na huduma hizo tutoazo, wako wanaokerwa na wanachokiona, kwamba baada ya kufurahishwa na kilichowaleta, wanakutana na hali inayoashiria kuwa fedha wanazolipia huduma husika haziwanufaishi wanaoishi katika maisha magumu kwa ujumla wao.

“Social Responsibility”ni dhana inayojulikana kuwa ni kama kurudisha fadhila na shukrani kwa walengwa fulani katika mazingira unayoyafanyia kazi. Faida mojawapo ni kule kuwafanya wahusika kujiona kama wadau muhimu katika mradi huo.

Serikali haina budi kujidhihirishia uhusiano wa karibu na wahusika wote kama wadau muhimu. Mafanikio yana gharama zake lakini pia ikiwa ni gharama zenye mafanikio na zenye kuongeza furaha kwa wananchi, ndilo lengo lenyewe.

Na bila kusahau tumekuwa tukisimangwa kuwa ni mojawapo wa nchi 10 maskini kuliko zote duniani kwa muda mrefu, kuna kila sababu kwa viongozi wetu kuona aibu kila wanapozungumzia utajiri na fursa tulizonazo wakati wanajua kuna maskini wanakufa kwa kukosa huduma muafaka zilizo kwenye uwezo wao kuzifanyia kazi.

Najua na ninaamini kuwa viongozi wetu wanao uwepo wa Mungu ndani yao, watafanya. Mungu awape nguvu ya kutenda mema kwa wahitaji wote nchini kwetu.

LANGLANG
 
Back
Top Bottom