Ndege ya Serikali aina ya Boeing 787-8 Dreamliner imeanza safari ya kwanza leo Julai 29, 2018 tangu ilipowasili nchini Julai 8.
Ndege hiyo inayoelekea Mwanza kupitia Kilimanjaro (Kia) iliondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam saa 12:35 asubuhi badala ya saa kumi na mbili asubuhi.
Kabla ya ndege kuondoka abiria walihesabiwa na baadaye wahudumu walitoa matangazo ya usalama.
Tofauti na ndege nyingine za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier, matangazo ya usalama katika ndege ya Dreamliner yanatolewa kwa njia ya video kupitia skrini iliyo mbele ya kila kiti.
Ukaguzi wa abiria
Awali, eneo la ukaguzi wa abiria wa safari za ndani lilijaa hivyo mtu alitakiwa kusubiri kwa takriban dakika 20 ili kukaguliwa jambo lililosababisha muda wa abiria kuingia kwenye ndege kuchelewa.
Idadi ya abiria kwenye chumba cha kusubiri kupanda ndege kilikuwa na watu wengi.
Awali, ilipangwa muda wa abiria kuingia kwenye ndege uwe saa 11:20 asubuhi lakini kutokana na wingi wa watu, walianza kuingia saa 11:35 asubuhi wakitangulia viongozi kadhaa waliokuwapo na waandishi wa habari.
Ndani ya ndege kulikuwa na wahudumu takriban 10 waliotoa huduma kwa abiria kwa ukarimu.
Miongoni mwa abiria waliokuwapo ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi.
Abiria aliyeingia na bendera ndogo tatu za CCM, alimkabidhi moja Polepole aliyekuwa amevaa sare za chama hicho.
Polepole aliyekuwa akipiga picha na baadhi ya abiria alisema, “Magufuli hoyee.”
Baadhi ya abiria aliokuwa amekaa nao karibu waliitikia, “Hoyee.”
Rais John Magufuli aliahidi kuifufua ATCL kwa kuipatia ndege mpya, Dreamliner ikiwa ni utekelezaji wa ahadi hiyo.
Abiria mwingine alisema ndege hiyo inatokana na kodi za wananchi.
Polepole aliijibu kwa kusema, "Ni kweli kabisa hizi ni kodi za wananchi lakini matumizi mazuri yanapangwa na Serikali."
Ilivyokuwa Kia
Ndege hiyo ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) saa 1:17 asubuhi.
Baada ya kutua Kia ikiwa ni mara ya kwanza, ndege hiyo ilipokewa kwa kumwagiwa maji.
Baadhi ya wananchi waliokuwapo uwanjani na wafanyakazi wa Kia walitumia simu zao za mkononi kupiga picha tukio hilo.
Abiria walioshuka uwanjani hapo walikabidhiwa maua.
Katika uwanja wa ndege wa Kia ndege ilikaa kwa dakika 40 kabla ya kuruka kuelekea Mwanza