Ni lini inabidi tuseme ndoa hii sasa basi............?
Hakuna kipimo hasa kwa sababu kila mmoja anaguswa kwa namna tofauti na jambo fulani, lakini kila mmoja wetu ana kiwango tofauti cha kuwavumilia na hata kuwasamehe wengine. Watu wengi huwa wanajiuliza wanapokosewa na wenzao kwenye ndoa, ‘sijui nimwache au nimpe tena nafasi?'
Dini zinasisitiza kusameheana, elimu ya utambuzi hivyo hivyo na hata mila na desturi zetu. Lakini kusisitizwa na kutenda ni vitu au mambo mawili tofauti. Bado dini hizo hizo kuna makosa ya kindoa ambayo zinayatazama kama makosa yenye kusameheka, lakini ambayo hayaruhusu au kutoa nafasi kubwa kwa ndoa kuendelea.
Moja ya makosa hayo ni uzinzi, yaani kutoka nje ya ndoa. Kutoka nje ya ndoa ni kosa ambalo limechangia katika kuvunja ndoa nyingi sana. Hata hivyo, kwa bahati mbaya imetokea kuvunja ndoa pale ambapo zaidi anayefumaniwa ni mwanamke. Mtu anapozini tunasema hampendi mwenzake. Hii ina ukweli kidogo kwa sababu kuzini kunafanywa kwa sababu ambazo ni tofauti kutoka moja hadi nyingine.
Kwa hiyo inashauriwa kwamba ndoa inaweza kuvunjwa au ni vizuri ikavunjwa kama inahusisha kuzini. Hata hivyo kama ni kuzini ambako kumetokea mara moja, inabidi mtu atafute sababu kwa nini kulitokea. Kama atathibitisha kwamba mazingira yaliyopelekea kuzini huko yalikuwa na ugumu katika kuepukwa, mume au mke wa huyo aliyefumania inabidi ajaribu kutoa nafasi kwa mwenzake.
Kama kuzini ni mara kwa mara, haishauriwi ndoa kuendelea kuwepo.Mtu anapoishi kwenye ndoa ambayo imegubikwa na uzinzi, anajiweka kwenye hatari nyingi sana. Kwa siku hizi, hatari ya kwanza ni maradhi. Lakini kuna hatari nyingine kadhaa. Kuishi na mzinzi ni kuishi katika kero kihisia. Wenye wake au waume ambao ni walevi, mara nyingi pia wanakabiliwa na maradhi yasiyoonekana hospitalini kwa sababu ya kujiumiza kihisia.