Josh Michael
JF-Expert Member
- Jun 12, 2009
- 2,523
- 77
Walter Sawe
TANGU Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani (2005), nimekuwa nikifuatilia staili ya Chama tawala Cha Mapinduzi (CCM), kinavyotumia njia mbalimbali kujisafisha.
Hakuna ubishi kwamba CCM ina mbinu nyingi katika kujisafisha na baadhi ya njia inazotumia, zinavutia, zinachekesha, zinashangaza na kutafakarisha.
Ni staili ambayo inazua maswali yasiyo na majibu au yenye majibu yasiyoridhisha kwa umma wa Watanzania kama ilivyotokea hivi karibuni mjini Dodoma.
Binafsi safari hii nimejiuliza maswali kadhaa kwamba CCM inajisafisha na nini? Ni uchafu gani inaojaribu kujisafisha? Uchafu huo umeingiaje? Na umeingizwa na nani?
Ikumbukwe kuwa tangu tuhuma dhidi ya viongozi wa CCM zitolewe pale Mwembe Yanga, Temeke, Septemba 15 mwaka juzi na viongozi wa upinzani, ikiwahusisha na ufisadi wa aina mbalimbali, kuanzia ule wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na nyumba za serikali.
Katika utawala wao wa miaka minne tu, ufisadi umekithiri serikalini, huku rais na mawaziri wake, wakiutetea waziwazi hata kwa kutumia mamilioni ya fedha za umma kuzunguka mikoani kuhadaa wananchi.
Wananchi maskini na wanaharakati wamekuwa wakipuuzwa, huku baadhi ya viongozi wakitoa kejeli mbalimbali kwamba kelele za mlango hazimnyimi mwenye nyumba usingizi.
Ndani ya miaka minne ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, viongozi wametumia madaraka yao vibaya kuliko miaka kumi ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Kutokana na hali hiyo, wapo wana CCM wanaosema bila woga kutaka Rais Kikwete asiongezewe muda kwa madai kuwa ameshindwa kuchukua maamuzi magumu dhidi ya mafisadi ndani ya serikali yake.
Naipongeza ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe na kusababisha Lowassa na mawaziri wengine wawili kuachia ngazi.
Je, kuondoka kwa Lowassa, Kikwete atapona? Umma wa Watanzania tuliliangalia suala la Richmond kwa haraka na kummwagia tuhuma zote Lowassa kana kwamba yeye alikuwa peke yake!
Kwanza, Lowassa alikuwa mtumishi na mteule wa rais na mtekelezaji wa maagizo ya Rais. Kwa mujibu wa Katiba yetu, waziri mkuu hawezi kutekeleza suala lolote kitaifa ambalo hajaagizwa na rais, halafu rais asimfukuze kazi.
Sawa, Richmond imeonyesha maagizo ya Lowassa na shinikizo lakini Lowassa angekuwa kajituma tu bila kutekeleza agizo au makubaliano angefukuzwa kazi na Rais? Haya na mengine mengi ukweli unabaki palepale kwamba usafi wa Lowassa ndio uchafu wa CCM.
Namalizia makala yangu hii kwa kuwaeleza umma wa Watanzania kuwa kuna mambo ndani ya Serikali ya Awamu ya Nne mazuri ambayo wanajivunia ni matunda ya Lowassa.
Mara zote ndani ya serikali na ndani ya chama, Lowassa alikuwa mtendaji, msimamiaji na mtekelezaji. Mwanzo wa makala yangu nilisema usafi wa Lowassa ni uchafu wa CCM.
Napenda Watanzania wenzangu wapenda haki tuelewe kwamba Lowassa kama kiongozi alikuwa habanwi kwa ufisadi bali kwa uwajibikaji wa pamoja kama msimamizi mkuu wa shughuli za serikali, Watanzania tumekuwa wepesi wa kusahau mambo.
Wakazi wa Shinyanga na Kahama watamkumbuka Lowassa akiwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo alidiriki kuwa tofauti na Wamisri na kuwapatia maji kutoka Ziwa Victoria na yapo hadi leo. Hiyo ni kazi ya Lowassa.
Ni Lowassa huyuhuyu alifuta umiliki wa viwanja vya tajiri mmoja, ambapo leo ndipo yamejengwa majengo ya PPF, International House, ni Lowassa aliwafukuza nchini City Water mwaka 2005, baada ya kushindwa masharti na kuilipa serikali sh bilioni 15.
Ni Lowassa huyuhuyu aliyesimamia shule za kata, hata kama walimu hakuna.
Ni Lowassa huyuhuyu aliyesimamia chakula cha njaa kikasambazwa kila tarafa, kata hadi kijijini.
Ni Lowassa huyuhuyu aliyepunguza foleni jijini Dar kwa utaratibu wa njia tatu hadi leo upo na nyingine zikapanuliwa kwa maelekezo yake.
Lowassa ameonyesha uungwana wa hali ya juu. Yeye ameamua kujiuzulu wadhifa aliokuwanao. Ingawa jamii imekwisha kuamini hayo yaliyosemwa sana juu yake, bado anayo nafasi.
Nimalizie makala hii kwa kuchavusha fikra zetu. Rais Kikwete aliwahi kusema yaliyomkuta Lowassa ni ajali ya kisiasa. Naamini Lowassa alipokuwa akifanya maamuzi mengi kati ya niliyoyataja hapo juu, tulimshangilia na kumsifia kana kwamba kiongozi shupavu. Nauliza, je, utamaduni huu wa kumalizana utatupeleka wapi?