Unapo mdumaza mtoto

fellali

Member
Aug 14, 2013
17
2
UNAPOMDUMAZA MTOTO
Na Felix Lugeiyamu.



Juzi juzi tu katika safari zangu nilikutana na rafiki yangu ambaye tulipotezana kwa muda wa miaka kumi na moja iliyopita. Katika maongezi yetu akanigusia hili, kuwa ameoa na ana mtoto mmoja ambaye ana umri wa miaka kumi na moja (11) tangu azaliwe na akanipa sifa zake lukuki kama vile ana akili nyingi za kuzaliwa kwa maana ya kwamba anaouwezo wa kupambanua mambo kwa undani kama mtu mzima, mdadisi, anapenda sana kuchangia hoja katika mikutano ya pale nyumbani kwake na kuwa hoja zake nyingi zinasaidia katika kuleta maendeleo ya familia yake n.k. Ki-ujumla alimsifia sana, ndipo nikapata fursa ya kumuuliza hili “anasoma darasa la ngapi?” majibu yake yalikuwa ya kutatanisha kidogo maana alisema amemuanzisha chekechea na akamuachia hapo tu. Nilishangaa sana maana kwa sifa alizonipa haikuwa na haja ya elimu ya Phd kumshauri kumwendeleza kielimu zaidi ya hapo alipomwachishia. “Nikamuuliza na hili: kwanini usimwendeleze zaidi na una kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya masomo yake? Mfano una rasilimali za kutosha kumlipia ada na vifaa vyote vya shule!” majibu yake yakawa ni haya “ nina hofu kama ntaweza kumwezesha hadi afikie yale malengo anayohitaji” nikamuuliza kivipi? Akajibu “sitaki aanze shule halafu aishie katikati kwa kukosa mahitaji muhimu”. Ki-ukweli alinishangaza sana.
Mtazamo wake niliulinganisha na ule wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)-Lushoto. Wote tutakumbuka kuwa Chuo hiki kilianza kutoa rasmi huduma zake mnamo tarehe 23 october, 2000 na kilizinduliwa tarehe 3 Agosti 2001 na aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin Wiliam Mkapa
Kuanzishwa kwa Chuo hiki, ilikuwa ni utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Utoaji wa Haki ya mwaka 1977 maarufu kama Tume ya Msekwa, Tume ya Rais ya uanzishwaji wa Demokrasia ya vyama vingi vya siasa ya mwaka 1993 (hii ni tume ya Nyalali) na Tume ya kuboresha sekta ya sheria ya mwaka 1996 (Tume ya Bomani).`
Pamoja na hiyo sababu, pia kulionekana upungufu wa watumishi wa Mahakama ikiwa ni pamoja na Mahakimu wa Mahakama za mwanzo na maafisa masijala. Tatizo hili likasababisha kuwa na mrundikano wa kesi na ikapelekea ucheleweshwaji wa utoaji haki.
Wazo la haraka la kukabiliana na tatizo hilo, likawa ni kuanzisha Chuo ambacho sio tu kitatoa elimu endelevu kwa maafisa wa Mahakama bali kiandae wahitimu ambao wangepata sifa za kuajiriwa kama mahakimu na maafisa masijala. Ndo hapo Chuo cha Uongozi wa mahakama (IJA)-Lushoto kilipozaliwa.
Wazo likanunuliwa na wadau wengi na mwikitikio ukawa unatia moyo. Wanafunzi wengi wakawa wanajitokeza kupata mafunzo ya kimahakama na sheria kwa ujumla. Jina likakua ndani na nje ya nchi kwa ujumla. Hadi leo ukizungumzia IJA-Lushoto katika taifa letu ni sawa na kuzungumzia Mahakimu, Mawakili, maafisa masijala, Wahadhiri wa Vyuo mbalimbali, lakini pia hata washauri wa masuala ya kisheria katika vitengo mbalimbali vya Kiserikali na visivyo vya kiserikali mfano Magereza, Polisi n.k.
Chuo kikajitahidi kuajiri wahadhiri waliobobea katika tasnia ya sheria ambao kwa kiasi kikubwa walijitahidi kutengeneza jina la Chuo na kukifanya kuwa Chuo cha aina yake kitaaluma na kimaadili. Mwanafunzi anayesomea IJA kweli anapikwa na kupikika haijalishi ni kwa Ngazi ya Astashahada au ngazi ya Stashahada. Wadau wa kisheria na jamii ya Watanzania, tunakubaliana katika hili.
Kwa kiasi fulani tatizo la mrundikando wa mashauri ya kusikilizwa ukapungua; Vuguvugu la wafungwa wa maabusu wanaochukua muda mrefu pasipo kusikilizwa mashauri yao ukapungua pia. Kuona hivyo, Mahakama ikakipongeza Chuo na Serikali pia kwa ujumla. Kiujumla ni Chuo ambacho kimekaa kikazi (vijana wanasema).
Sifa hizi zikailewesha IJA-Lushoto, wakajisahau kwamba wanapaswa kuendelea zaidi ya hapo walipofikia, wakaendelea kutoa Stashahada na Astashahada tu kwa kipindi chote hicho cha kuanzishwa kwake. Wakajisahau kuwa ngazi hizo za elimu ilikuwa ni kwa ajili ya muundo wa utumishi wa mahakama namba 22 wa mwaka 2002 uliokuwa unaonesha kuwa ili kuaijiriwa kwa kada ya Uhakimu wa mahakama za Mwanzo ni muhimu uwe na stashahada ya sheria na ili uwe Afisa masijala ulipaswa kuwa na Astashahada ya sheria.
Juzi juzi tena tatizo la upungufu wa mahakimu wa mahakama za mwanzo na maafisa masijala limeibuka tena kwa upya na kwa kasi kubwa zaidi. Wananchi wa kitanzania wenye mashauri ya kusikilizwa katika mahakama za mwanzo wamerudia msoto ule ule wa mashauri yao kutumia muda mrefu bila kusikilizwa katika mahakama za mwanzo huku idadi kubwa ya wafungwa( mahabusu) nayo ikizidi kuongezeka.
Tatizo hili limetokana na sababu kuwa, wale walioajiriwa kama mahakimu wa mahakama za mwanzo enzi hizo wakiwa na Stashahada wamejiendeleza kimasomo na wanapomaliza wanapandishwa vyeo kuwa Mahakimu wa Mahakama za Wilaya, na hivyo kuacha nafasi zao za mwanzo zikiwa wazi.
Katika miaka ya 2010 na 2011 kulivuma taarifa kuwa Mahakama ilibadilisha Muundo wa Utumishi wa Mahakama kwa kada ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo. Sifa za kuajiriwa kuwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo zilibadilishwa kutoka Stashahada ya Sheria kuwa Shahada ya Sheria. Na kweli wahitimu wengi wa miaka hiyo miwili hawajapata ajira hadi leo wapo mtaani wanasuburi nafasi za kazi ndani ya Mahakama huku wakiwa wamekata tamaa.
Ndio hapo nikazinduka nakujiuliza “si, kuna Chuo Cha Uongozi wa Mahakama?”na je, lengo la kuanzisha Chuo hicho si kutoa elimu endelevu kwa watumishi wa kada zote za Mahakama an kuaandaa watumishi wa kada zote za mahakama?” kwanini kisitumike kuwaandaa watu hawa wanaohitajika kwa kufuata sera mpya utumishi wa mahakama? Kwani mahakama inakosa kitu gani hadi washindwe kuanzisha “shahada ya sheria na mambo ya utawala wa kimahakama” kama wanavyohitaji? Au Chuo na mahakama wamefumba jicho moja na hivyo kutoliona tatizo la ukosefu wa mahakimu, maafisa masijala na watenda kazi wengine wa kimahakama na tasnia ya Sheria? Au kwamba tatizo hili haliwahusu? Na kama haliwahusu kwanini wasitoe msaada kwa jamii ya kitanzania? Au nao wanasubiri msukumo wa umma?
Ukilifikiria kwa undani suala hili unaweza kupata maswali mengi ambayo wa kuyajibu ni mahakama na Chuo chenyewe yaani IJA-Lushoto.
Inawezekana Mahakama haina takwimu sahihi za waadhiri na ngazi ya elimu walizo nazo. Kwa utafiti wangu nilioufanya hivi karibuni, nimegundua kuwa Chuo hiki, kina jumla ya wahadhiri therathini na watano (35). Kati ya hao “mmoja ana Shahada ya uzamivu ya sheria” na mwingine anamalizia masomo yake ya “shahada ya uzamivu” pia ya sheria. Mwingine mmoja ana” shahada ya uzamivu ya lugha na mawasiliano”; jumla yao wenye shahada ya uzamivu ni watatu (3).
Kumi na nane (18) wana shahada ya uzamili ya sheria, wanne (4) wana shahada ya uzamili ya lugha na mawasiliano na wawili (2) wana shahada ya uzamili ya Kompyuta. Wanne (4) wana shahada ya uzamili ya Utunzaji nyaraka na Kumbukumbu. Pia watatu (3) wana shahada ya kwanza ya Sheria na wawili wana shahada ya kompyuta. Hiyo ndiyo kambi ya wahadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto; Inatia moyo?
Hivi kwa wahadhiri hawa, Mahakama haioni umuhimu wa kuanzisha programu ya shahada ya sheria katika mambo ya utawala wa kimahakama ili kupunguza tatizo lililopo la upungufu wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo? Na kama inaona umuhimu huo, inangoja nini kuanzisha Programu ya shahada ya sheria katika Chuo hiki? Au inasubiri Chuo kipeleke wazo hilo? Na je, chuo kinasuburi nini? Ingelikuwa ni mimi ningeanzisha Dokezo la pendekezo hili haraka sana.
Naamini mtajiuliza kwanini nimeamua kuandika IJA-Lushoto, na sio Chuo kingine cha Umma? Ukweli ni kuwa mimi ni mmoja wapo wa wanafunzi wa Chuo hiki wa mwanzo niliyefaidi matunda ya Chuo hiki. Ninajua ubora wa mafunzo yanayotolewa na Chuo hiki maana kinatoa elimu bora na siyo bora elimu. Na huu ni ukweli ninao amini unaungwa mkono na Watanzania.
Ninaweza kusema IJA-Lushoto, ni mtoto aliye dumazwa na baba yake Mahakama, tusitegemee asaidiwe na mtu yeyote ila ni Mahakama yenyewe. Nafikiri ni wakati muafaka sasa Mahakama kuona tatizo linalo ikabili na kuona kwamba IJA ni mtoto aliyedumazwa na sasa anapaswa kuendelezwa kwa ajili ya maendeleo ya familia (nchi) ya sasa na ya baadae.
Kila la kheri Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto!
Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki IJA-LUSHOTO.
Kwa maoni zaidi nitumie kwenye email: flugeiyamu@yahoo.com; flugeiyamu@gmail.com
 
Back
Top Bottom