Jerry Nashon alikulia katika kijiji kiitwacho Kigera kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma jirani na shule ya Sekondari Mara. Jerry alianza kujifunza gitaa akiwa Musoma Catholic Mission club ambayo leo ni Mwembeni secondary School. Alikuwa ana mazoea ya kwenda kwenye hiyo social club ya kanisa iliyofanya kazi nzuri sana ya kuwaunganisha vijana wenye vipaji mbalimbali. Alijiunga katika bendi ya Special Baruti Band iliyokuwa na Rashid Ruyembe mwaka 1980. Jerry alianza kuendelezwa na Charles Koya ambaye wakati huo alikuwa mpiga rhythm wa bendi hiyo. Alikuwa mwanafunzi mzuri na baada ya muda mfupi alikuwa mpigaji mahiri na akaweza kurekodi na bendi yake hiyo katika studio za Tanzania Film Company, RTD na hatimaye katika studio mbalimbali nchini Kenya. Jerry na Special Baruti Band walifanya maonyesho mengi katika jiji la Nairobi , katika kumbi na club mbalimbali kama vile Bombax Hotel, Kaka Night Club, Rwadhia Night Club na nje ya Jiji katika mikoa takribani yote ya Kenya kasoro Mombasa na Kisumu. Katika kumwona kiongozi wa bendi hiyo, ambaye ndiye alikuwa mtunzi na mwimbaji akipata umaarufu mkubwa nae akaona heri ahame kutoka upigaji wa rhythm na kuwa mwimbaji mtunzi. Taratibu alianza kujifunza na juhudi zake zikaonekana na Jeshi la Magereza Musoma nalo likamchukua akajiunge na Magereza Jazz Band. Baada ya miaka miwili na nusu hivi akiwa na Special Baruti Band Jerry alihamia Dar es Salaam. Wakati huo mji wa Musoma ulikuwa na bendi nyingine, kulikuweko na Musoma Jazz Band waliopiga kwa mtindo wao wa Segese, Mara Jazz Band maarufu kwa mtindo wao wa Sensera, pia ilikuwepo bendi iliyomilikiwa na Seminary ya Kikatoliki ya Makoko, hii iliitwa Juja Jazz band , haikuwa na mtizamo wa kibiashara hivyo haikuwa na umaarufu kama zilizotajwa hapo juu. Jerry alidumu kwa muda Magereza Jazz band kasha akahamia Bima Orchestra nahatimae Vijana Jazz Band mpaka mauti yake.