Umma umechoka kuonewa, kunyonywa

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
Na Lula wa Ndali Mwananzela | 13 Jun 2012

NIMEJARIBU kutafakari kwa nini kuna wimbi la watu kuikataa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nguvu zaidi wakati huu kama ilivyokuwa mwaka 1995.

Miaka mingi imepita lakini wakati mwaka 1995 ilikuwa kwa kiasi kikubwa ni kutumia uhuru wa kujiunga na chama kingine zaidi ya CCM safari hii kuna kitu tofauti kinajionyesha wazi.

Watanzania kwa maelefu – mijini na vijijini, wazee kwa vijana, wake kwa waume – wameamua kuiambia CCM "Bye Bye" na kujiunga kwa mbwembwe kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Nilipotafakari zaidi mang'amuzi haya mapya yanayoendelea nimejikuta nikirudi nyuma zaidi karibu miaka 50 iliyopita.

Vitu vile vile vilivyowafanya Watanganyika na Waafrika kwa ujumla kuukataa ukoloni na serikali yake vimeanza kukataliwa tena na safari hii si dhidi ya ukoloni bali dhidi ya utawala ambao umegeuka na wenyewe na mwelekeo wa ukoloni usiopingika.

Mambo haya matano manne kati yake yanajulikana sana kwani yamekuwepo katika tangazo la Azimio la Arusha la mwaka 1967 na ambalo ukweli wake bado unasimama.

Katika Azimio la Arusha tulitangaza hivi: Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha… Ni unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe, tunyanyaswe na tupuuzwe. Sasa tunataka mapinduzi ili tusionewe, tusinyanyaswe na tusipuuzwe tena!"

Hivyo, mambo manne ya kwanza ambayo Watanzania wanayakataa ni kuonewa, kunyonywa, kunyanyaswa na kupuuzwa.

Tuyaangalie haya kidogo:

Tumeonewa
Watanzania wameamua kukataa kuonewa na watawala wao. Kuonewa huku kunakuja kwa aina nyingi sana lakini kubwa ni ile hisia ya tofauti kati ya watawala na watawaliwa ambapo watawala ambao kutokana na nafasi zao wanajiaminisha kuwa wanaweza kufanya lolote, kwa yeyote aliye chini yao.

Mifano miwili iko wazi sana kuwakilisha hili. Wengi mnakumbuka yule DC aliyemzaba kibao baba wa watu mbele za watu na hakukemewa na kiongozi yeyote.

Wapo watu wengi sana ambao wamejikuta wakionewa na watawala iwe katika ajira, biashara au hata nafasi tu. Matokeo yake Watanzania hawa wamejikuta wakilazimika (sijui kama ni sawa kuita kulazimika au kulazimishwa) wanatafuta kujipendekeza kwa watawala hao ili ‘mambo yao yawanyokee'.

Ni uonevu wa kiutawala ambao unalazimisha wananchi wa kawaida kuwa kama vijakazi mbele ya watawala. Ni uonevu unaowafanya watawala waweze kutoa maagizo yoyote kwa sababu ya utawala wao.

Tumeona watu wetu walivyohamishwa kwa nguvu sehemu mbalimbali ili kupisha ‘wawekezaji'. Tumeona mahali ambapo watu wamenyang'anywa maeneo waliyokuwa wanalima mazao ya chakula ili waje watu kulima mazao ya ‘mafuta'! Sasa Watanzania hawa wameamua kukataa kuonewa tena!

Tumenyonywa
Moja kati ya mambo ambayo Azimio la Arusha lilipambana nayo ni kile Mwalimu alichokiita "exploitation of man by man'. Kwa wanaokumbuka vizuri tatizo kubwa la ubepari mahali pote duniani ni kuwa unatengeneza tabaka la wanaofanya kazi na kuhenyeka na wanaokunja nne na kubweteka wakila matunda ya jasho la wengine.

Unyonyaji huu ambao umesifiwa kuwa ni ‘ubepari" au mfumo wa mtaji (capitalism) umesifiwa sana kwa kuinua maisha ya watu hasa kwa kuongeza ushindani. Lakini utabiri wa Nyerere juu ya mfumo huu umekuwa wa kweli na matokeo yake miaka 50 tangu aandike yale yanatimia. Nashauri watu wasome "A Rational Choice" ambapo Mwalimu anaelezea kwa nini kwa taifa changa kama la kwetu uchaguzi sahihi ulikuwa ni ujamaa na si ubepari.

Lakini ubepari una matokeo mazuri vile vile hasa kwenye ngazi ya ushindani. Lakini ni ushindani wa nani hasa? Nyerere anaelezea kwa kweli si ushindani wa mtu mwenye biashara ndogondogo na kampuni kubwa ya kimataifa! Huwezi kumshindanisha mchimba madini wa Chunya na Barrick au Ango-Ashanti Gold. Huyu mchimba madini hana ubavu!

Huwezi kushindanisha kwa mfano kiwanda kidogo cha kutengeneza baskeli na kiwanda kikubwa cha kutengeneza baskeli cha huko Marekani. Matokeo ya ushindani huu mara zote ni kuwa makampuni makubwa ndiyo yatanufaika na wafanyabiashara ndogo wataendelea kufanya biashara ndogo au – kama Nyerere alivyoonesha kwenye maandishi hayo – yule mkubwa anapoamua kumnunua yule mdogo!

Dunia imetambua hili na miaka kama 10 iliyopita mwamko wa kuupinga ubepari huu wa kimataifa umeibuka katika kampeni ya kupinga utandawazi ambapo ubepari ulivuka mipaka ya nchi na kuanza kuingia kwa nguvu kwenye nchi masikini.

Ni kweli umeleta viwanda vikubwa lakini wakati huo huo kuua kabisa viwanda vya ndani na ushindani mdogo wa ndani. Kumbe unyonyaji ambao umetokea sasa si wa mtu na mtu tena bali ni unyonyaji wa makampuni makubwa ya kimataifa dhidi ya vijimiradi vidogo vya baba, mama na vijana wetu!

Hivyo, Watanzania wanakataa kunyonywa; wanakataa kugeuzwa vijakazi na watumishi wanaovaa suti za kupendeza za makampuni makubwa ya kimataifa ambayo kutokana na sera zilizopo, yanaweza kuzalisha nchini nakuondoa faida yote kwa asilimia 100 kuipeleka kwao.

Yaani, makampuni ambayo yamekuja na kugeuza Tanzania shamba lao. Na hili linatisha zaidi hasa pale ambapo serikali inakubali kampuni ya kigeni kukodi eneo la ardhi na kupanda mazao ya chakula ambayo soko lake kwa asilimia 100 ni kwenda kwenye nchi zao! Kuna uwezekano huko baadaye watu wakawa wanakufa njaa wakati mashamba ya wageni yanazalisha chakula na kupelekwa nje na watu wetu watakapoanza kulalamika wataambiwa "ndivyo mkataba unavyosema!"

Hivyo, wanakataa kuonewa kwa namna yoyote ile kwani wameshaonewa kiasi cha ‘kutosha'!

Tumenyanyaswa
Sasa hili la kunyanyaswa linaendana na hilo la kunyonywa. Wakati hili la kunyonywa linahusiana na mahusiano ya kiuchumi, hili la kunyanyaswa linahusiana na mahusiano ya mtu na mtu katika jamii, na hasa, kati ya wale walionacho na wale wasionacho.

Walionacho wanaweza kujipatia lolote katika jamii wakati wale wenzangu na miye inabidi wajitahidi sana kupata kidogo wanachokipata. Ni unyanyasaji wa kimfumo.

Fikiria kwamba hakuna kiongozi mkubwa wa kitaifa ambaye anata tatizo la umeme au maji! Yeye ameweza kujiwekea posho au utaratibu wa kununua jenereta na mafuta yake (iwe nyumbani au ofisini) na ana uhakika wa usafiri wake (lipo gari la serikali kumpeleka kokote). Mtu wa kawaida anapata shida ya maji na umeme kwa sababu vitu hivyo ni anasa kwake na anapojaribu kuvitafuta ni manyanyaso ya kila namna.

Lakini unyanyasaji mwingine ambao uko wazi – na watu wenye madaraka hauwagusi – ni kutotendewa kwa heshima wanakofanyiwa wananchi wanapotaka huduma mbalimbali.

Majuzi nilikuwa na mjadala mkali kwenye FB yangu na mambo mengi yakawa dhahiri. Mtu anapoondoka nyumbani kwenda kutafuta huduma hasa kwenye taasisi ya serikali anatakiwa ajiandae kihisia na kiakili; kuna kuzungushwa, kuna kucheleweshwa, kunakusumbuliwa kiasi kwamba anaporudi nyumbani anakuwa hoi bin taaban si kwa sababu ya safari bali sababu ya watu aliokutana nao. Ni kunyanyaswa anakofanyiwa mtu duni kulinganisha na heshima anayopewa mtu ‘anayejulikana'. Hili Watanzania wanalikataa.

Tumepuuzwa
Sasa hayo matatu ya kwanza yote yanahusiana moja kwa moja na jinsi mtu anavyotendewa. Lakini hakuna kitu kinachoudhi zaidi kama mtu kupuuzwa.

Unapompuuza mtu kimsingi unamuondolea umuhimu wake alionao na unaondoa hisia yoyote ya kuonekana ana thamani. Kumpuuza mtu ni kumfanya mtu si kitu; anachosema hakina maana, matatizo yake hayana mpango, na malalamiko yake ni ya kijinga. Mfumo unapompuuza mtu unamfanya mtu au raia ajihisi ameondolewa thamani.

Wakoloni walifanikiwa sana katika kumpuuza mtu Mweusi; walimpuuza kiasi kwamba athari zake zilibakia kwa muda mrefu kwenye fikra za watu wetu.

Hata leo hii utakutana na watu ambao wanatafuta kuonekana wana thamani mbele ya Wazungu kuliko inavyoweza kuelezeka kiakili. Mkoloni alimfanya mtu wetu duni kwa mifumo aliyomtengenezea na kwa jinsi alivyomhudumia. Kupuuzwa basi ni jambo ambalo mwanadamu hajaumbwa kuishi nalo. Huwezi kumpuuza mwanadamu kwa muda mrefu kabla mwanadamu huyo hajaamua kuasi.

Hata watumwa walipuuzwa kwa muda mrefu lakini hatimaye kizazi chao kilikuja kuasi. Sasa kupuuzwa huku katika nchi yetu kunaonekana sana katika mambo mawili makubwa (nitaacha wengine wayaongeze).

Kwanza ni katika ubora huduma ambazo serikali inatoa kwa wananchi wake. Ukiangalia vizuri sana utaona kuwa utawala uliopo haujaweka msisitizo katika ubora wa huduma bali wingi wa huduma.

Shule, hospitali, barabara, nishati, n.k vyote vipo na vingi vimeongezwa lakini suala la ubora linaudhi. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) katika ripoti zake mbalimbali amekuwa akigusia hili kwa namna moja au nyingine anapolinganisha fedha iliyotumika na ubora wa kitu kilichonunuliwa au kupatikana (value for money comparison).

Hili la ubora linaonekana sana kwa kukosekana kwa mifumo mizuri ya Quality Assurance (QA) na hivyo taasisi na ofisi nyingi za serikali kukosa usimamizi mzuri wa huduma wanazotoa.

Sasa Watanzania hawataki kuendelea kupuuzwa. Kwani kupuuzwa kunakoudhi zaidi ni kule kwa wao wananchi kuonekana wasumbufu; maswali yao kutupwa pembeni na wanapouliza kujihisi kama wanamuuliza mfalme wa mbinguni. Habari zilizoripotiwa kuhusu Steven Wassira hivi karibuni kwenye jimbo lake kunatudokeza.

Si mara moja kiongozi wa umma anaposimama kuulizwa maswali anaanza kuonyesha kumpuuza mwananchi aliyeuliza swali hilo. Ni nani amesahau jinsi yule mtoto wa shule ya msingi wilayani Ukerewe alivyomuuliza swali Edward Lowassa na akajiletea matatizo?

Ni mara ngapi watu wanaogopa kuuliza maswali kwa sababu watu wa ‘usalama' watawaita pembeni na kuwabana? Hadi waandishi wa habari wanaogopa kuuliza maswali wanapokuwa mbele ya watawala na badala yake wanakuja kama kasuku kutuambia alichoongea mkubwa na kuacha maswali yaendelee kuning'inia au wanakimbilia kuandika maswali kwenye tahariri zao badala ya kumuuliza muhusika na kumbana atoe majibu. Wanaogopa kupuuzwa!

Lakini maelfu wameamua kukataa kuendelea kupuuzwa! Hakuna utawala ulioweza kudumu huku ukipuuza wananachi wake au kundi kubwa la wananchi wake.

Sasa hayo manne yote yanapatikana ndani ya Azimio la Arusha. La tano hata hivyo naweza kusema ndilo linakataliwa zaidi na kizazi cha sasa nalo ni kudanganywa.

Tumedanganywa
Watanzania wamechoka kudanganywa na kuahidiwa mambo yasiyoweza kufanyika. Lakini ni kudanganywa kunakofanyika kiutalamu sana na sasa wananchi wamegundua. Sasa kudanganywa kunakofanywa mara nyingi ni kule kunakotelewa na wenye vyao kwa namna ya ahadi. Watawala wanaposhindwa kutoa majibu ya kueleweka wao hutoa ahadi.

Sasa ahadi zinaficha ukweli wa uzembe na kushindwa kwa watawala. Fikiria pembezoni ya makazi ya polisi pale Msimbazi, Dar es salaam ambapo kwa miaka nenda palikuwa pamerundikana vinyesi na uchafu.

Sasa mahali kama hapo unaweza kuuliza nani au kumuuliza mtu nini akakupa jibu la ukweli zaidi ya kutoa ahadi? Sasa wananchi wameshaanza kugundua kuwa ahadi = uongo wa kinamna.

Kwanini wanakimbilia CHADEMA?
Kwanini ni CHADEMA? Watu wengi wanaanza kujiaminisha kuwa CHADEMA nacho kinayakataa mambo hayo hayo. Wananchi wanakimbilia huko kwa sababu wanaamini kitawaongoza kuelekea "Uhuru wa pili".

Kama wazee wetu walivyokimbilia TANU dhidi ya mkoloni leo wapo watu wanakimbilia CHADEMA kwa sababu wanaanza kuamini kuwa labda nayo itawaongoza katika kujijengea kujitegemea, kujiheshimu na kuthaminiwa.

Hata hivyo, naamini changamoto kubwa zaidi kwa CHADEMA si kufanya maandamano au kuvaa magwanda bali ni jinsi gani itaongoza watu kuanza kujiletea maendeleo.

Ni lini kwa mfano tutaona viongozi wake wakifanya kama alivyofanya Nyerere katika ziara yake ya pili ya vijiji vya Tanzania mwanzoni mwa miaka ya sabini ambapo alishiriki kazi za ujenzi wa Taifa.

Kwa mfano, lini tutaona vijana wa CHADEMA wakihamasika kupaka rangi shule, kuleta matofali, kuziba mitaro au hata kujenga kliniki au kuboresha kliniki. Je, inatosha kufanya maandamano na kuhamaisha watu kujivua gamba kama kuvaa gwanda mwisho wake ni kujisikia raha tu lakini si kufanya kitu?

Kumbe Watanzania wanapokataa haya mengine kimsingi wanakubali jambo linalowezekana. Swali ni lipi litawezekana chini ya CHADEMA sasa kabla ya 2015? Historia itaamua.

Vyovyote vile itakavyokuwa Watanzania hawatokubali tena kuonewa, kunyanyaswa, kupuuzwa, kunyonywa na kwa hakika hawatokubali kudanganywa tena. Wanataka vitendo vyenye kuonyesha kuwa watawala na wale wanaotaka kuja kutawala wanawapa thamani wanayostahili, wanawajali na kuwaheshimu kama wananchi.
 
Zanzibar imekuwa kama kupe mgongoni mwa ng’ombe. Haiishi kulalamika kwa nini ng’ombe hali vizuri, kwa nini ng’ombe hatambui uwepo wa kupe, kwa nini ng’ombe damu yake si tamu sana.


Imekuwa ni kupe asiyetosheka na sasa anaamini kuwa kwa kujitoa mgongoni mwa ng’ombe anamkomoa ng’ombe. Ati anadai uhuru wake, ili awe kupe kamili. Tatizo ni kuwa hakuna namna yoyote kupe ataweza kukaa bila kunyonya ng’ombe au mnyama mwingine. Zanzibar haiwezi kukaa bila kutegemea nchi nyingine. Ama itategemea bara au itajaribu kutegemea Uarabuni au nchi nyingine.


Chanzo: Raia Mwema, Toleo na. 250, 18 July 2012
 
Mkuu, kinachofanya bara tung'ang'anie Muungano ni nini? je! Haya matusi yote ni kosa la nani???
 
Well said,hivi vikupe kila siku kazi kubwabwaje.Vinapenda sana kusaidiwa,sasa hvi vinaona waarabu ni waume wazuri kuliko watanganyika.Mi naona bora viende huko hafu baadaye vijutie maamuzi.
 
Mkuu, kinachofanya bara tung'ang'anie Muungano ni nini? je! Haya matusi yote ni kosa la nani???

Zenj ni koloni letu,tukiwaachia utakuwa uwanja wa alshabab,boko haram na alqaeda kwa hiyo hakuna kuwaachia.We umeona ushirikiano wao na iran.Je wakiwa huru kipi kitakachofuata?
 
Hata sisi watanzania tumechokwa kunyonywa na viongozi tunaowapa madaraka wanaotoa maamuzi yanayowafurahisha wao.
 
Kosa ni kuichagua ccm, hakuna Mtanganyika aliwahi ulizwa ktk kuufanya huo muungano, Dawa pekee ni kuipiga chini ccm, watanganyika watakua na nchi yao na znz watakua na kiti chao Un, CCM ni JANGA la kitaifa uwepo wake unaondoa utulivu na ustawi wa watanganyika wote
 
Zenj ni koloni letu,tukiwaachia utakuwa uwanja wa alshabab,boko haram na alqaeda kwa hiyo hakuna kuwaachia.We umeona ushirikiano wao na iran.Je wakiwa huru kipi kitakachofuata?

Utahofu mataifa mengine mpaka lini????????????????????? You Tanganyika, jiimarishe Kijenshi na uache kuwatumia wenzio kama ngao yako ya kinga
 
Hongera kwa uchambuzi mzuri, ila tatizo litakuwa kwa sisi wananchi kubadilika. Kwa maana hata kama itakuja Chadema kama fikra za watu za kubadilika hakuna itakuwa kazi bure. Kama tutaendelea kuwa na watu wanaoamini maendeleo yatakuja kwa kusubiri serikali na sio mtu binafsi au kusubiri serikali ikuambie safisha mazingira yako ili usipate malaria, kama tutaamini kwamba ili kuhudumiwa kwenye ofisi za serikali ni mpaka utoe pesa basi sisi (wananchi) tutakuwa na matatizo.



Kuichukia hali hii ya kuonewa, kudharauliwa, na kupuuzwa inabidi ifanyike sambamba na kujenga nchi ambayo watu wake wapo tayari kukataa uonevu, ubinafsi na pia kujitolea kushiriki pamoja katika shughuli za maendeleo ya nchi, iwe kujenga shule, zahanati, barabara, kufanya usafi kwenye maeneo tunayoishi.
 
Back
Top Bottom