Umeshawahi kukutana na balaa la nyoka?

Satoh Hirosh

JF-Expert Member
Mar 30, 2021
5,950
23,264
Kuna mtu ukimtania "hapo chini Kuna nyoka" ni Kama unatafuta kumuua kwa presha, hawapendi kabisa kuleteana utani wa nyoka. Wengine wakijua ndani, nyumba wanazoishi Kuna nyoka ataikimbia nyumba na kuitelekeza kabisa hadi asikie nyoka ameshauawa.

Sasa, Kuna akina sisi ambao huwa hatuogopi nyoka. Kuna baadhi ya matukio nayakumbuka na mengine najiona mjinga Sana kwa kucheza na mdudu huyu hatari Sana.


====


Enzi hizo nipo kijana mdogo wa darasa la tano, siku moja ilikuwa msimu wa baridi Kali (kipupwe). Kwetu kipindi Cha baridi Hali inakuwa tete kwa sisi tusiopenda maji, inafikia wakati baridi linakuwa Kali Hadi mchanga ukikanyaga bila viatu unahisi umekanyaga barafu. Kipindi hiki swala la kuoga linageuka kuwa Jambo la ufahari.

Sasa siku moja nikiwa nimejiandaa mapema Sana ili niwahi shule kuchukua namba maana mwalimu wa zamu alikuwa mnoko. Kwa sababu ya baridi kuwa kali, nikagahilisha swala la kuoga, nikapiga mswaki Kisha nikanawa uso na kutinga uniform tayari kwenda shule. Sasa njiani Kuna zile nyasi zilizopata umande. Nikijiangalia miguuni naona miguu Kama imepakwa chokaa, habari ya kupaka mafuta usiku kabla ya kulala upo kijijini unaanzia wapi? Nikasema hii miguu hapana kwa kweli, imezido kuchakaa, nikawa nimehama njia na kuanza kupita kwenye nyasi zenye maji (umande) ili kusafisha miguu. Hapo miguuni nimevaa kandambili alafu kitendo Cha kupita kwenye nyasi zenye maji zikawa Safi hadi nikiwa nainua mguu kandambili inaitika waah!! .Watoto wa siku hizi wa gari za njano na wakiamka wanasalimia good morning Dad and mamy hawaelewi hizi mambo za kunawa maji ya umande.

Sasa wakati nimehama njia natembea kwenye nyasi ili kuosha miguu, huku kidumu na fagio vipo mikononi, Ghafla..!! Cobra akiwa amevimbisha shingo huku amejaza mate yenye sumu alikuwa ameshajihami yupo mbele yangu tayari yupo katika mkao wa kushambulia. Wakati nimetaharuki nawaza nini Cha kufanya yeye ndiyo kwanza akasogea barabarani kweupe kabisa. Ni Kama alisogea mbele kuniblock nisiende shule. Nikaangalia nyuma Kama Kuna mtu anakuja nikawa naona ukungu tu, nilikuwa mzee wa kuwahi Sana. Wale wanafunzi wanaowahi sana shule. Nidhamu nyingi. Hata hivyo kwa sababu sikuwa mwoga wa nyoka nikasema leo mbona tutanyooshana tu. Pembeni yangu kulikuwa na mti mrefu kidogo nikauchukua nikatoa vitawi ikabaki fimbo. Nikaanza kumrushia.

Sasa Cobra kwa kukwepa ndiyo mwaliku wao. Kila nikirusha anakwepa alafu ananifokea balaa huku amejaza lundo la mate yenye sumu shingoni. Lakini Cha ajabu Wala harudishi mashambulizi wala kunitemea mate yake yaliyojaa shingoni yenye sumu Kali.

Kumbe nyoka ana akili Sana.

Wakati najiona Kama napambana nae nimuue kumbe mwenzangu ananiona Kama mtoto tu nisiye na hatia akawa ananikwepa pasi na kunidhuru. Ilikuwa Kama anacheza na Mimi maana hata nguvu ya kurusha ule mti ilikuwa dhaifu Sana kwa sababu ya umri wangu.

Alipoona nimetaharuki huku macho yamenitoka Kama tochi nakaribia kulia alafu sina msaada akaamua kuinama chini na kusepa mdogo mdogo na kuishia zake porini. Alipotokomea ndiyo nikakumbuka Kumbe nilibeba kidumu cha maji na fagio, sijui nimevitupa wapi. Nikavitafuta nikakuta nilivitupa kwenye majani, maji yameshamwagika maana kidumu hakikuwa na mfuniko. Nikasepa zangu shule miguu ikiwa haina nguvu kabisa.

Ila sikukoma, niliendelea na tabia yangu ya hovyo na kukutana na balaa la nyoka? Ilikuwaje?
 
Kisa Cha pili.

Nakumbuka ilikuwa nipo kidato cha tatu,siku moja nipo likizo huko kijijini nilkwenda nyumbani kwa rafiki yangu ambae nae kaja likizo. Nyumbani kwa jamaa kumejitenga nje kidogo na kilipo Kijiji. Mzee wake anamiliki eneo kubwa sana la shamba kwa hiyo akaamua kujenga huko huko shambani wakawa wanaishia huko. Kutoka kwao kuja kijijini ni mwendo wa Kama robo saa.

Nilipofika kwao huyo rafiki yangu,tulipiga sana stori. Katikati ya stori akachomekea stori nyingine "Oya Satoh pale shambani kwenye mihogo Kuna 'bonge la chatu' amelala chini ya mti!!"

Sasa jamaa kuongelea nyoka akawa Kama amenitia ndimu maana napenda sana stori za nyoka. Nikamwambia twende tukamwone!! Jamaa akaniambia yupo kwenye shimo huwezi kumuona nyoka wote ila utamwona baadhi ya sehemu tu. Nikamjibu twende tukashuhudie huko huko.

Baada ya Kama dakika 3 tukafika shambani. Lilikuwa shamba la mihogo. Pale shambani Kuna mti mmoja mkubwa sana ambao una mizizi iliyotokeza nje. Inaonyesha kipindi kabla haujakuwa my mkubwa ulitaka kung'oka pengine kwa sababu ya mvua au upepo,kwa hiyo kwenye ile mizizi iliyozama Chini unaweza kupitisha hata bomba kubwa likatokea upande wa pili Kama halitakutana na kizuizi Cha mizizi midogo.

Jamaa akaniambia angalia chini kwanza. Nilipoangalia chini nilistuka kuona mchirizi mnene Kama limepita tairi ya gari ndogo. Akasema hii ndiyo njia yake na anapolala ni hapo kwenye mti,chungulia chini kwenye ule mzizi. Aisee chatu anatisha!! Nilipoinama kuangalia ule mti niliona joka kubwa nene balaa. Nikwambia jamaa tusepe hapa atatuuua huyu.
Rafiki akasema huyu hawezi kung'ata Kama nyoka wadogo,hadi akuwekee mtego,na hapo alipo hata umfanyaje hawezi kurudi nyuma,hadi aende mbele Kisha akutegee mtego,kwa hiyo hapo hawezi fanya chochote. Tulipotosheka kumwangalia tukasepa.

Sasa ukageuka utaratibu wetu kila siku kwenda kufanya utalii wa ndani...Tukaanza kufanya kitu cha hatari zaidi!!

siku nne mfululizo nikifika tu nyumbani kwa jamaa tunaenda kumchezea chatu. Nasema kumchezea kwa sababu baada ya kumzoea tukaanza kumchokonoa na miti tuliyoichonga. Wakati tunamchezea alikuwa anafoka kwa hasira sana.

Mzee wa rafiki yangu Kuna kitu akanotice akaanza kutufutatilia nyendo zetu. Siku ya tano tuliporudi home tu huku tunakimbia baada ya kumchokonoa yule chatu na mti ,tukahisi anataka kutoka ili atukimbize ndiyo tukakutana na mzee anatusubiri. Akatusimamisha na kutuuliza huko shambani huwa mnaenda kufanya nini na kwa nini mnarudi kwa woga huku mnakimbia na kuhema juu juu? Tukamjibu tulikuwa tunachimba mihogo. Akauliza iko wapi hiyo mihogo? Tukaangaliana bila majibu. Akatubananisha tukamwambia ukweli. Mzee alitusema sana kwa jinsi tulivyokuwa tunacheza na kifo maana chatu ni mdudu hatari sana. Akatuambia huyo nyoka mnayemchezea,Simba na ubabe wake wote akikutana na chatu anamgwaya. Hivi hiyo shule inawasaidieni nini humo kichwani? Mzee akageuka Faiza Fox kutuchamba.

Siku walipoweka mtego wa kumuua ndipo tulijua tulikuwa wapumbavu kiasi gani kwa kitendo tulichokuwa tunamfanyia yule chatu...Ni Kama tulikuwa tunabipu kifo. Mtego waliomtegea ili anase Kisha afe aliuvunjavunja vibaya mno. Ingawa wanakijiji walifanikiwa kumuua lakini shamba la mihogo la mzee lilichakaa kwa mbilinge mbilinge za joka na mishale ya wanakijiji. Alikuwa Ni nyoka mkubwa sana.

Chatu ni nyoka mwenye nguvu sana ndiyo nikakumbuka kauli ya mzee siku anatugombeza aliposema Simba mwenyewe na ubabe wake wote akikutana na chatu akili inamkaa sawa.

Kuna kisa kingine Kati ya chatu na dereva wa Dangote...Narudi
 
Chatu na dereva wa gari la Dangote.

Miaka kadhaa iliyopita Kuna Docta mmoja alikuwa anatoka Dar anaelekea Masasi mkoani Mtwara kwa mambo yake binafsi. Alipofika ndani ya viunga vya wilaya ya kilwa mkoani Lindi kwa mbali mbele yake akaoana na gari (roli) ya Dangote ambayo ilikuwa inaelekea Mtwara. Baada ya dakika chache jamaa wa Dangote akapunguza mwendo akapaki kando ya barabara Kisha akashuka akasogea kwa ndani kwenye majani. Ilikuwa mida ya jioni Kama saa kumi na moja. Doctor akalipta lile roli na kuendelea na safari yake.

Kesho yake Doctor alipomaliza mishe zake mjini Masasi akawasha gari na kurudi Dar. Cha ajabu alipofika eneo lile la Jana mahali gari la Dangote limepaki alilikuta lipo vile vile. Na gari halikuwekwa triange kuashiria kwamba limehaeibika. Ilikiwa Kama limepaki kwa muda Kisha safari itaendelea.

Jamaa akapunguza mwendo Kisha akawa anaendesha mdogo mdogo mpaka usawa wa lile roli. Akapaki pembeni Kisha akashuka na kuvuka barabara kwenda upande wa pili kuangalia pengine dereva ana shida au amepata ugonjwa wa ghafla alafu watu/madereva wapita njia wasijue maana gari halikuonekana Kama Lina ishara ya kuharibika na halikuwa na mzigo maana lilikuwa linarudi Mtwara.

Alipofika akapiga hodi kwa mlango wa dereva hakukuwa na response yoyote. Akajaribu kufungua mlango ukafunguka bila shida. Akaangalia ndani hakuona mtu. Wasiwasi ukamwingia akahisi Kuna uwezekano wa tatizo,ile haikuwa hali ya kawaida.

Akasogea barabarani kuangalia magari yanayokuja. Kwa bahati Kuna gari ndogo ikawa inapita akaipungia mkono ikasimama. Wakapita madereva Kama watatu nao wakasimama. Jamaa akawasimulia kilichotokea kuanzia jana. Wakaamua kuingia kwa ndani,ndani ya kamsitu kuangalia Kama wataona chochote.

Kilichotokea....

Kumbe yule dereva ile Jana aliposhuka kwenye gari alienda kujisaidia (tafsida). Huko porini ndiyo akakutana na balaa la chatu. Inavyoonyesha chatu aliweka mtego jamaa akauingia,na kwa kukosa msaada akazidiwa nguvu akauawa Kisha akamezwa.

Pale porini walimkuta chatu amelala hoi kwa kushiba na tumbo lake limejichora alama ya mtu akiwa amelala kwa kunyooka.

Taarifa ikawafikia wenye mamlaka,chatu akauawa na marehemu akatolewa nje ya mwili wa chatu. Picha za yule jamaa zilikuwa zinatisha sana maana alimezwa mzima mzima,yeye,viatu hadi nguo. Alikuwa Kama amemwagiwa mayai au mlenda.

Kama humu ndani Kuna madereva au wahusika wa Dangote wanaweza kukumbuka hiki kisa Cha dereva wao aliyemezwa na chatu Miaka kadhaa iliyopita.

Kuna kisa kingine Cha kishujaa Kati ya chatu na Mamba...

Narudi
 
Visa vipo vingi kwa sababu nimekaa sehemu yenye nyoka nyoka wengi kwa Miaka mingi. Nakumbuka mfano siku moja nimeenda na mzee kukata kuni,wakati nimemaliza kufunga mzigo wangu nikaukalia huku namsubiri mzee afunge wake Kisha nimtwishe maana Mimi ni kijana nilikuwa na nguvu sana,tofauti na yeye mzee,wakati nimezikalia zile kuni nikahisi mtikisiko,nikageuza kuni Kumbe nilikuwa nimeweka mzigo juu ya nyoka aitwaye kifutu. Kwa sababu ya upole wake yule nyoka mzee aliniambia nisimuue kwa sababu Hana kosa na Kama angekuwa ana ubaya angeshaning'ata muda tu alafu poa sisi ndiyo tumemfuata kwenye makazi yake (akimaanisha porini). Kweli sikumfanya chochote tukasepa bila kumuua. Kuanzia siku ile nikaanza kuwaangalia viumbe kwa namna ya upole.

Nitasimulia kisa hiki Cha mwisho.

Taarifa ikafika kijijini,huko mtoni Kuna chatu mkubwa anapambana na Mamba. Wanakijiji wakaanza kutiririka kuelekea mtoni kushuhudia hilo tukio.

Ilikuwaje hadi chatu na mamba kushambuliana kiasi hiki?

Kuna jamaa mmoja mchungaji wa wanyama,ng'ombe,mbuzi na kondoo alikwenda kulisha na kunywesha maji wanyama wake kando kando ya mto. Ilikuwa mida ya jioni Kama saa 11. Kumbe eneo lile la mto kandokando ya maji Kuna chatu mkubwa ameshaweka mtego wake anasubiri mbuzi ajichanganye Kisha ajipatie kitoweo.

Wakati huo huo ndani ya maji karibia eneo lile lile alipo chatu Kuna mamba mkubwa anavizia mnyama atakayekuja kunywa maji ili ajipatie nyama ya jioni.

Ilikuwa bonge la scene.

Wakati mchungaji wa hao wanyama yupo makini kuwachunga wanyama wake na kuwapeleka sehemu yenye kina kidogo ambacho mamba hawezi kufika,Kuna mbuzi mmoja akamsahau kum-monitor...si unajua mbuzi wanavyokuwa na wenge!!? Waliowahi kuchunga mbuzi wanajua mziki wa mbuzi machungani. Mimi nimewahi kuchunga mbuzi wa shule enzi hizo primary. Ilikuwa mshikemshike. Ukifungua banda tu Kuna mbuzi viherehere unawakuta wameshakuacha km mbili kwa uroho wa kukimbilia majani porini.

Pale mtoni,yule mbuzi aliyewaacha wenzie akasogea mbele ghafla akaanza kulia kwa sauti kali meeh meeh!! Sijui nini kilitokea ila mamba na chatu wakajikuta wanamvamia mbuzi kwa pamoja. Isivyo bahati,wote wakakosa kitoweo wakajikuta wamevamiana wenyewe kwa wenyewe. Na hapo ndipo mziki ulipokuwa hadi jamaa wa kuchunga akaja kuita wanakijiji.

Eneo la mto lote nyasi zililala pakawa Kama palipitishwa fyekeo. Mamba alikuwa amefanikiwa kuingiza kichwa Cha chatu mdomoni lakini chatu hakuchagua kuwa mnyonge. Alijiviringisha kwenye mwili wa Mamba na kumbana mbavu ili asipumue.

Mpaka wananchi tunajaa lile eneo,ilikuwa Mamba na chatu wote wameshachoka hoi. Ni Kama wote walikuwa wanakaribia kukata moto maana kila mmoja alikuwa amembananisha mwenzie sehemu mbaya...Mamba amebanwa mbavu hapumui na chatu haonekani kichwa,means kipo kwenye bakuli(mdomo) wa Mamba.

Kufupisha stori,hili tukio hakupatikana mshindi maana wote walikufa na wananchi wenye uchu kujipatia kitoweo Cha mamba na ngozi ya chatu kiulaini kabisa.

Ingekuwa enzi hizi za smartphones Hili tukio lingetrend sana mitandaoni ila ilikuwa zamani kidogo.
 
Sasa cobra na koboko tft si ni lugha au
Hapana mkuu,

Cobra ni nyoka mwingine na koboko ni mwingine pia. Na Kati ya hao wawili hatari zaidi ni koboko,ni nyoka mwenye kisirani na anapenda sifa za kijinga.

Unaweza kwenda kuchunga ng'ombe yet akaamua kukutia hasara akawagonga ng'ombe wote ili wafe tu akutie umasikini. Cobra anavimba Sana kwenye mashavu akiwa na hasira na anatema mate yenye sumu,nakumbuka cobra ameshawahi kumtia upofu ng'ombe wa shule kwa kumtemea mate yenye sumu Kali.
 
Ulivyosema ulikuwa unatumia fimbo kupiga nyoka umenikumbusha tukio moja la miaka ya nyuma.

Wakati niko shambani nalima kuna nyoka akakatiza mbele yangu, nikasema huyu simuachi.

Nikachukua fimbo ndefu nikawa namchapa nayo ila alikuwa yuko fasta kukwepa. Ghafla nilikuta nilivyorusha kumchapa akairukia ile fimbo akawa anatembea juu yake kuja kwangu.

Aisee nilipagawa niliachia ile fimbo nikafanya mara 3 ya kile anachokifanyaga Usain Bolt
 
Sasa cobra na koboko tft si ni lugha au
Cobra sio koboko, ni aina mbili za nyoka tofauti. Cobra nimeshuhudia Mwaka huu mwezi January tulimuua baada ya kuingia kwenye zone yake pasipo kujiua akatuletea utata tukapambana naye.

Cobra anajitanua shingo yake hasa anapokuwa ameudhika.

Koboko (Black/Green mamba) sijawahi kumuona kwa macho yangu ila nimehadithiwa na nimemsikia hasa nyakati za usiku akiwa anawika
 
Cobra sio koboko, ni aina mbili za nyoka tofauti. Cobra nimeshuhudia Mwaka huu mwezi January tulimuua baada ya kuingia kwenye zone yake pasipo kujiua akatuletea utata tukapambana naye.

Cobra anajitanua shingo yake hasa anapokuwa ameudhika.

Koboko (Black/Green mamba) sijawahi kumuona kwa macho yangu ila nimehadithiwa na nimemsikia hasa nyakati za usiku akiwa anawika
Sas kwa nini mlimuua na nyie ndo mliingia kwenye zone yake
 
Hapana mkuu,

Cobra ni nyoka mwingine na koboko ni mwingine pia. Na Kati ya hao wawili hatari zaidi ni koboko,ni nyoka mwenye kisirani na anapenda sifa za kijinga.

Unaweza kwenda kuchunga ng'ombe yet akaamua kukutia hasara akawagonga ng'ombe wote ili wafe tu akutie umasikini. Cobra anavimba Sana kwenye mashavu akiwa na hasira na anatema mate yenye sumu,nakumbuka cobra ameshawahi kumtia upofu ng'ombe wa shule kwa kumtemea mate yenye sumu Kali.
Exactly, Mwaka Juzi kule Uyui Tabora kuna Mzee mmoja ngo'mbe wake wengi waliuliwa na koboko ndani ya dakika chache sana. Niliona habari hii ITV
 
Back
Top Bottom