Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,997
Kashfa karibu zote ambazo zimetokea Tanzania na ambazo zitaendelea kutokea zinahusiana moja kwa moja na matumizi mabaya ya madaraka (abuse of power). Na tatizo kubwa pia ni kuwa hao ambao wanatumia madaraka yao vibaya hawaamini wanatumia madaraka hayo vibaya; hutumia kila aina ya kisingizio na udhuru kujaribu kutuelewesha kuwa kwanini walichofanya ni sahihi.
Na wanakuwa wa mwisho kuona jinsi gani wametumia madaraka vibaya. Ni kama mtu mlevi; mtu mlevi ni wa mwisho kabisa duniani kujua kuwa ana tatizo la ulevi (alcoholism). Wakati familia, jamii na hata marafiki tayari wameshamuona ana tatizo la kinywaji a.k.a ulabu yeye mwenyewe haamini kuwa ana tatizo hilo na anaweza kuonesha kuwa yuko timamu. Na anaweza kusema kuwa wakati wowote akiamua kuacha anaweza kuacha. Mlevi wa madaraka naye yuko hivyo hivyo; anaamini kabisa yuko sawa na hana tatizo.
Matokeo yake walevi wa madaraka wana hatari kubwa zaidi kwa sababu wakati mlevi anaweza kuwa tatizo kubwa kwa familia yake au watu anaokutana nao moja kwa moja (kama katika ajali hivi) mlevi wa madaraka ana matokeo makubwa zaidi kwani maamuzi yake yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu na kwa jamii. Mtu anayetumia madaraka vibaya anaweza kuwa chanzo na kichocheo cha umaskini katika jamii - wakati yeye anafurahia utajiri (kama mlevi anavyotumia pombe).
Mfano wa Anna Tibaijuka na viongozi wengine ambao wamepigwa upofu na fedha, umaarufu, na madaraka (blinded by money, fame and power) ni kuwa wanaamini watu wote hawako sahihi; hawawezi kujiangalia wao wenyewe kwani wanaamini wanaangaliwa kwa jicho la wivu.
Ndio maana watu kama Werema wanazile dalili za ulevi huu. Werema anapojiuzulu anatuambia ati wote hatukuelewa ushauri wake. Kwamba alichokishauri ni kitu cha juu sana kiasi kwamba akili zetu kama taifa haziwezi kuelewa na hivyo ni makosa yetu kutokuelewa na siyo kosa lake kushauri. Na wala hawezi kuamini kuwa yeye ndiye haelewi hasira ya taifa ni nini kuhusiana na hili. Naye kama Tibaijuka anajionesha kuwa ni mlevi.
Walevi wote wa madaraka kama walivyo walevi wengine hawawezi kuacha kwa kutaka wenyewe. Ulevi huu unanguvu mno za kulevya (intoxicating power); na mtu hawezi kuacha bila kuwa na dalili kali za kukosa kileo (withdrawal symptoms). Watu kama hawa wakati mwingine wanahitaji kusaidiwa kwa watu wasio na ulevi huu kuingilia kati (intervention).
Kuingilia huku inaweza kuwa kwa kuwatimua kazi, kuwatia pingu, kuwanyang'anya mali zote haramu na kuhakikisha wanapigwa marufuku kusimamia fedha za umma mahali popote na kwa wale ambao ulevi huu ni mkali kwao basi kupigwa marufuku kabisa kushika nafasi yoyote ya umma. Kuwaambia tu walevi wa madaraka wajiuzulu au kuwahamisha haitoshi; watatafuta kileo kingine tu... mlevi haachi mwenyewe.
Ndio njia pekee ya kuwasaidia.