Ukomavu wa Uongozi: Tabia au Cheo?

Ukomavu wa Uongozi: Tabia au Cheo?

Zack Abdul

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2026
Posts
560
Reaction score
519
✍️Kuna jambo moja ambalo vijana tunapaswa kujifunza kwa umakini sana katika safari ya uongozi si kila mtu anayetamani kuwa mkubwa ana uwezo wa kubeba ukubwa huo.

Kuwa na ndoto kubwa ni jambo jema kuwa ambitious ni jambo jema kutaka kufika mbali ni jambo jema

lakini tatizo huanza pale ambition inapopoteza mipaka ya nidhamu heshima subira na uadilifu.


Uongozi unatupa mifano mingi ya watu ambao walikuwa na uwezo walikuwa na nafasi walikuwa wameaminiwa lakini walishindwa kwa sababu walitaka kufika kwenye kilele kabla hawajajifunza maana ya kubeba mamlaka.

Hapo ndipo tunapaswa kujiuliza Je tunataka uongozi kwa sababu tunataka kutumikia au tunataka uongozi kwa sababu tunataka kutawala?


Kuna tofauti kubwa sana kati ya mtu anayesema “Nataka siku moja niwe kiongozi mkuu ili niweze kufanya makubwa” na yule anayesema “ Kwa nini yeye awe mkuu wakati mimi nina uwezo kuliko yeye?”

✍️Wa kwanza ana ndoto wa pili ameanza kuingia kwenye mtego wa entitlement yaani kujiona kwamba nafasi fulani ni haki yake.


Tatizo hili linaweza kuanza kwa kitu kidogo sana.

Unaweza kuteuliwa kuwa msaidizi wa mtu ukapewa dhamana ya kumsaidia katika majukumu yake.

✍️Badala ya kuona nafasi hiyo kama shule ya kujifunza uongozi unaanza kuitazama kama ngazi ya kumpita aliyekuteua🙌.

Unaacha kujiuliza Ninawezaje kumsaidia huyu kiongozi afanikiwe?

na kuanza kujiuliza Nitawezaje kumfanya aonekane hafai ili mimi nichukue nafasi yake?


Hapo ndipo ambition inapogeuka kuwa tamaa ya madaraka .



Msaidizi anayefanya kazi kwa bidii ili mkuu wake afanikiwe si dhaifu huyo anaonyesha ukomavu.

Kwa sababu ameelewa kwamba mafanikio ya taasisi ni muhimu kuliko ukubwa wa jina lake.


Lakini msaidizi anayeanza kuhujumu kazi ya mkuu wake ili ajionyeshe yeye ndiye mwenye uwezo zaidi hata kama ana akili nyingi kiasi gani bado hajakomaa kiuongozi.


Tunapaswa kuelewa kwamba kupewa nafasi ni ishara ya kuaminiwa lakini si uthibitisho kwamba umefika mwisho wa safari yako.

Mtu anaweza kuaminiwa leo kama mkurugenzi msaidizi kesho akawa mkurugenzi.

Anaweza kuwa mkuu wa wilaya leo kesho akapewa nafasi kubwa zaidi.

Anaweza kuwa mbunge leo kesho akawa waziri.


Lakini kila hatua inahitaji mtu ajifunze kubeba dhamana ya wakati wake bila kuharibu nafasi ya mwingine.


Ndiyo maana si busara kuishi maisha ya kulinganisha nafsi yako na kila aliyepandishwa juu yako.

Mafanikio ya mwenzako si ushahidi wa kushindwa kwako.


Wakati mwingine mtu mwingine anaweza kupewa nafasi ambayo wewe uliitamani lakini hilo halimaanishi kwamba Mungu amekusahau.


Inaweza kuwa bado unaandaliwa au nafasi yako ipo sehemu nyingine au unatakiwa kwanza kujifunza kitu ambacho hujajifunza.


Hapa ndipo imani na uongozi vinapokutana.

Kama tunakubali kwamba Mungu ndiye anayejua kesho yetu basi hatupaswi kuishi kwa hofu kwamba tusipopata cheo leo basi tumepoteza maisha.

Cheo kinaweza kuchelewa lakini kuchelewa siyo kukataliwa.

Wakati mwingine kinachotakiwa kwanza si kupata mamlaka zaidi bali kujenga uwezo wa kuitumia mamlaka hiyo bila kuharibu wengine.

Tukitazama historia ya siasa duniani tunaona mara nyingi kwamba tamaa ya madaraka inapovuka mipaka mtu anaweza kuanza kumwona hata aliyemsaidia kufika hapo kama kikwazo.

Hapo ndipo utii unapoanza kupungua makundi yanaanza kujengwa maneno ya chinichini yanaanza kusambaa na mtu anaanza kutengeneza mazingira ya kuonekana yeye ndiye suluhisho la matatizo ambayo wakati mwingine yeye mwenyewe ameyachochea.


✍️ Hili ni somo muhimu sana kwa vijana wanaoingia kwenye siasa taasisi michezo dini na uongozi wa kijamii.


Usijenge safari yako kwa kumwangusha mwingine.

Kwa sababu unaweza kumwangusha leo lakini tabia hiyo hiyo inaweza kukurudia kesho pale utakapokuwa juu.


Kiongozi mwenye ukomavu anajua kwamba mamlaka ni ya muda.

Leo unaweza kuwa juu kesho mwingine akawa juu yako.

Leo unaweza kuwa mteuzi kesho ukawa mteuliwa.

Leo unaweza kuwa mkuu kesho ukawa mshauri.

Kwa hiyo heshima unayowapa wengine leo ndiyo aina ya uongozi utakayostahili kesho.


Na hapa ndipo tunapopaswa kutofautisha kati ya uaminifu na unafiki.


Kuheshimu mamlaka hakumaanishi kukubaliana na kila kitu bila kufikiri.

Msaidizi anaweza kuwa na maoni tofauti na mkuu wake.

Anaweza kumpa ushauri mgumu.

Anaweza kusema jambo fulani si sahihi Lakini tofauti ya kiongozi mkomavu na mwenye tamaa ni kwamba mmoja anapinga hoja kwa nia ya kulinda taasisi mwingine anapinga mtu kwa nia ya kuchukua nafasi yake.


Hii ni tofauti ndogo kwa maneno lakini kubwa sana katika uongozi.


Usikatae mtu kwa sababu unataka nafasi yake pinga wazo kwa sababu unaamini linaweza kuiumiza taasisi.


Vijana tunapaswa kujifunza pia kwamba si kila anayekusifia anaamini katika uongozi wako.

Wengine wanaweza kukusifia kwa sababu wanataka kutumia tamaa yako ya madaraka.

Wanaweza kukuambia Wewe ndiye unayestahili “Wewe una uwezo kuliko huyo” “Kwa nini usiwe wewe?” Ukianza kuamini kila kauli kama hiyo unaweza kujikuta unaingia kwenye vita ambavyo hukuvianzisha kwa hekima bali ulivianzisha kwa ego.


Ndiyo maana kiongozi lazima awe na watu wanaoweza kumwambia ukweli si watu wanaomwambia kila anachotaka kusikia.


Mtu anayekupinga kwa hoja anaweza kuwa anakujenga zaidi kuliko anayekusifia kwa maslahi.


Kwa hiyo tunapozungumzia leadership maturity hatuzungumzii umri pekee.


Tunazungumzia uwezo wa kudhibiti ego kuvumilia kusikiliza kujifunza kuheshimu mamlaka kukubali kushindwa kumpongeza aliyeshinda na kuendelea kujenga bila chuki.


Hapo ndipo uongozi wa kweli unapojengwa.


Kwa sababu ukweli ni kwamba mtu anayeshindwa kujitawala mwenyewe hawezi kuaminika kutawala wengine.

Kama tamaa zako zinakutawala cheo kikubwa kinaweza kukufanya kuwa hatari zaidi kuliko ulivyokuwa kabla ya kukipata.


✍️Ndiyo maana vijana tusikimbilie tu kuuliza Nitapata lini nafasi?


Tuulize pia
Nikipata nafasi hiyo nitakuwa mtu wa aina gani?


Je, nitakuwa kiongozi anayejenga watu au anayewaogopa wenye uwezo?

Je, nitatafuta mafanikio ya taasisi au nitatafuta sifa yangu binafsi?

Je, nitamwinua anayenifuata au nitamzuia kwa sababu naona anaweza kunipita?


Je, nitaheshimu mamlaka nikiwa chini kama ninavyotaka kuheshimiwa nikiwa juu?

Na zaidi ya yote nikikosa nafasi niliyoitamani nitaendelea kuwa mwaminifu au nitageuka kuwa mpinzani wa yule aliyepewa?


Haya ndiyo maswali yanayotenganisha mwenye ndoto za uongozi na mwenye maandalizi ya uongozi.


Kwa hiyo tusikatae ambition Tuiweke kwenye nidhamu Tusikatae ndoto Tuzijenge kwa subira.

Tusikatae kutaka madaraka Tujifunze kwanza maana ya dhamana.

Na tusikatae kutaka kuwa viongozi wakubwa lakini tujue kwamba ukubwa wa cheo hauwezi kuzidi ukubwa wa tabia.


Mwisho wa yote historia haitakumbuka tu ulifika kwenye nafasi gani itakumbuka ulivyotumia nafasi hiyo uliwatendeaje waliokuwa chini yako uliwaheshimuje waliokuwa juu yako na ulifanya nini pale ulipokuwa na nafasi ya kumwangusha mwingine lakini ukachagua kumjenga.


Huo ndiyo ukomavu wa uongozi.


Na kwa vijana tunaotamani kuwa viongozi kesho somo ni moja
Usikimbilie kiti. Jenga tabia ya kukalia kiti bila kubadilika kuwa mtu mwingine.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom