Ukomavu wa Kihisia: Nguvu ya Usikivu

Ukomavu wa Kihisia: Nguvu ya Usikivu

Zack Abdul

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2026
Posts
1,088
Reaction score
865
Kama kuna kiashiria kimoja kizuri cha ukomavu wako kihisia ni uwezo wa kumsikiliza mtu hasa yule usiyejua hulazimiki kumsikiliza. Ukomavu huo unakuchochea kutamani kuelewa ‘ulimwengu’ wa mwenzako—anafikiri nini, anaona nini, anaamini nini, anataka kufanya nini—bila kuteka uzoefu wake wala simulizi lake na kulipima kwa mizania ya misimamo na matarajio yako.

Usikivu wako unapimika vizuri kwa namna unavyoweza kusikia kisichoweza kusemwa kwa maneno. Unasikiliza sauti inayobeba hisia zilizo nyuma ya maneno anayochagua mwenzako. Unasikiliza ujumbe unaobebwa na uso wa mtu. Unasikiliza kuelewa maana ya kimya cha mtu bila kumhukumu na kumshinikiza kukuamini. Unasikiliza kuelewa kinachomgusa zaidi, kinachobeba matumaini yake, kinachomtia ujasiri, kinachobeba fahari yake na kumfanya ajione muhimu miongoni mwa binadamu wenzake.

Kadhalika, usikivu wako huambatana na ule upendo wa dhati unaojaribu kuuelewa woga wa mwenzako, kuelewa ilikojificha aibu yake, ukurasa upi wa maisha yake asingependa kuusoma kwa sauti na kubaini swali lipi asingependa uulize maana linaweza kutibua unyonge na hisia za kushindwa. Unasikiliza kinachomkera, kinachotishia heshima yake, kinachotishia kesho yake na hata kuchochochea hasira yake.

Unapokuwa na ukomavu wa kihisia, kwa hakika humsikilizi mwenzako kama mtu anayemsoma mwenzake ili kubaini mapungufu yake, wala humsikilizi ili umshauri, umrekebishe, umkosoe na kumfundisha cha kufanya bali kumuelewa yeye kama binadamu timamu, mwenye uhuru mwenye na utashi anayeishi kwenye dunia yake bila kuiingilia. Usikivu, kwa ufupi, ni kumsikiliza mwenzako kwa lengo la kujifunza maana, kwa hakika, unaheshimu uelewa wake hata kama huuelewi.
 
Back
Top Bottom