Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,854
- 3,104
Wakati uongozi wa Chadema ukikutana na watia nia ya kugombea ubunge na udiwani katika ofisi ya makao makuu jijini Dar es Salaam Machi 3, 2025, kundi hilo linaundwa na wagombea na watiania wa ubunge 55 wa Chadema wa 2020 na 2025, limewasilisha maoni yake kwa maandishi likipinga kampeni ya No reforms, No election (Hakuna mabadikiko, hakuna uchaguzi).
Kundi hilo linalodai kuwakilisha zaidi ya watiania zaidi ya 200, linahusisha makada wa Chadema waliomuunga mkono Freeman Mbowe katika kinyang’anyiro cha uenyekiti ndani ya chama hicho Januari 2025.
Uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, ulishuhudia Tundu Lissu akishinda uenyekiti kwa zaidi ya asilimia 51, huku Mbowe akipata zaidi ya asilimia 48, huku John Heche akimshinda Ezekia Wenje katika nafasi ya umakamu mwenyekiti.
Licha ya kuwa na nia ya kugombea nafasi hizo, hakuna mwakilishi wa kundi hilo aliyefika kwenye mkutano wa watia nia na viongozi wa Chadema, ambapo wamedai kutishiwa na kauli za viongozi wa chama hicho.
Wakirejea kauli ya Lissu alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Iringa akisema, "wote wanaoona, "No Reforms, No Elections" haiwezekani ni wana-CCM pamoja na vibaraka woo, wakisema kauli hii ya Mwenyekiti tayari imezuia uhuru wetu wa kutoa maoni au ushauri mbadala dhidi ya kampeni hiyo.
Wamerejea pia kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, akihutubia mkutano jijini Arusha, amenukuliwa akisema kwamba "wote wanaotaka ubunge au udiwani bila reforms waondoke Chadema".
Kampeni ya No reforms no election iliyongazwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 2024 ambao CCM walishinda kwa asilimia 98.
Akizungumza katika mkutano wa watia nia, Mwenyekiti wa Chadema alieleza chanzo cha kampeni hiyo akisisitiza kuwa ataisimamia hadi tone la mwisho.
“Kama secretariat walikaa na kubuni No Reforms no Election ili wapandishiwe dau, mimi sina dau. Kama walipitisha kiutani utani basi mimi nipo serious kweli kweli, sifanyi siasa za udalali, nafanya siasa za ukombozi,” alisema Lissu.
Wataka chama kisizuie wagombea
Katika waraka wao walioutoa Machi 4, 2025 kuelekea kwa Katibu Mkuu wa Chadema yenye kichwa cha habari ‘Ushauri kwa Chama’ makada hao wamesema wanaunga mkono na wapo tayari kuongeza nguvu zaidi katika jitihada zote za Chama za kudai mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi (reforms), lakini wamesema hawaamii katika mpango wa Chama wa kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2025.
“Tunaona kuwa haiwezekani kuzuia uchaguzi kwa kuwa nje ya uchaguzi. Kujaribu kuzuia uchaguzi huku tukiwa nje ya uchaguzi itakuwa ni sawa na kufanya jinai. Uwezekano pekee wa kuzuia uchaguzi ni kushiriki uchaguzi wenyewe kwa kuhakikisha tunaingiza wagombea katika uchaguzi.
“Ni rahisi kwa wagombea kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi katika vituo mahsusi vya uchaguzi, katika kata au majimbo yanayoelekea kufanyiwa hujuma kuliko kujaribu kuzuia uchaguzi wote huku tukiwa nje kabisa ya uchaguzi wenyewe,” wamesema katika andiko hilo.
Kuhusu dhana ya "No Reforms, No Elections", wamesema ilianza kama kampeni Januari 2020 baada ya kikao cha kujipanga cha Kamati Kuu iliyofanyika Makueni, nchini Kenya, na haikuwa na tafsiri ya kuzuia uchaguzi bali ilikuwa inalenga kuhamasisha uungwaji mkono wa kudai mabadiliko.
“Kwa muda mfupi uliosalia, hatuoni uwezekano wa kutekeleza kwa ufanisi mkakati wowote madhubuti wa kuzuia uchaguzi. Tayari, uchaguzi wenyewe umeshaanza kupitia uandikishaji wapiga kura ambalo limeshafanyika kwenye mikoa mingi nchini na mchakato wa uchaguzi unaendelea kwa hatua ya mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi,” amesema.
Wamenukuu Katiba ya Chadema, ibara ya 4 inayohusu madhumuni ya chama, ikisema lengo kuu la Chama ni kuongoza dola na kutekeleza madhumuni mahsusi ya kisiasa kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 4.1, madhumuni ya kiuchumi yaliyopo kwenye kifungu 4.2 pamoja na madhumuni ya kijamii kama yalivyoainishwa katika kifungu 4.3.
“Kwa hiyo, kushiriki uchaguzi ili kuongoza dola ni sharti la kimsingi la kikatiba. Mpango wa kuzuia uchaguzi unaweza kukosa uhalali wa kutosha kikatiba kwa kuathiri haki za wanachama wa Chadema wanaotaka kugombea,” wamesema.
Wamedai kuwa wamebaini kuwa wadau wengi wa demokrasia wanaunga mkono madai yetu ya mabadiliko, lakini wanasita kuunga mkono mpango kamili wa Chama chetu wa kuzuia uchaguzi iwapo mabadiliko hazitopatikana.
Kuhusu athari za kutoshiriki uchaguzi, wamesema chama hicho kinaweza kuondokewa au kupoteza viongozi na wanachama wenye nia ya kuwania urais, ubunge, udiwani pamoja na nafasi za viti maalum vya ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini.
“Chama kitapoteza mvuto kwa umma, kitadhalilishwa kwa propaganda na hata kudhohofika. Hadi sasa Chama kimekatika katika vipande viwili vinavyosigana kuhusu jambo hili. Ikitokea tukashindwa kushiriki uchaguzi, mkatiko huu utakuwa ni wa wazi na athari zake zitakuwa mbaya zaidi.
“Chama kitapoteza kabisa ruzuku baada ya uchaguzi na hivyo kuathiri uhai na uendelevu wa shughuli za Chama, ari na hamasa ya wanachama kukichangia Chama itazidi kushuka kwani wananchi hawatoona faida ya kukichangia Chama kisichoshiriki uchaguzi.
Pia wamesema chama kitashindwa kujijenga zaidi maana na kupoteza uhusika na umuhimu wake kwa umma.
Wameshauri kwamba chama kiendelee kuongeza kasi na nguvu ya kudai mabadiliko yatakayoleta chaguzi huru na zenye kuaminika (reforms), lakini bila kuchanganya madai hayo na ajenda ya kuzuia uchaguzi.
“Upo uwezekano wa kushinda uchaguzi wa 2025 na kutangazwa katikati ya vikwazo vingi vya kikatiba, kisheria na utamaduni mbaya wa CCM wa kubaka demokrasia,” wamesema.
G55 wanaa athari gani kwa Chadema?
Akizungumza kuhusu kundi hilo, mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza amesema kundi la G55 halitakuwa na athari yoyote kwa Chadema, kwani halipo kisheria.
“Chama kinaendeshwa kwa vikao ambavyo ndivyo vilipitisha No reforms no election tena wakati Mbowe akiwa mwenyekiti, kwa hiyo ni uamuzi wa chama sio wa Lissu.
“Chama kinafuata itikadi, falsafa na miongozo, sio mtu, kwa hiyo kama wao ni wanachama ni lazima wafuate hivyo, lakini kama wanamuunga mkono mtu watapotea wenyewe,” amesema.
Alipoulizwa kama kundi hilo linaendeleza majeraha ya uchaguzi uliofanyika Januari 22, 2025 na kama chokochoko hizo zinaweza kukivuruga chama kinapoelekea kwenye uchaguzi, amesema hawataathiri kitu.
“Ni kweli wengi walimuunga mkono Mbowe, lakini yeye sio kiongozi kwa sasa, kwa hiyo wanaweza wasilete athari kwa chama.
“Wengi waliopo kwenye kundi hilo ama walikuwa waajiriwa wa chama au viongozi, kwa hiyo sasa wamepata nafasi ya kusemea baada ya kutolewa.
“Hawana uwezo wa kufanya kitu nje ya chama, kwa sasa,” amesema.