Ujamaa ubepari ufisadi na Rais Magufuli

AUGUSTINO CHIWINGA

JF-Expert Member
Apr 23, 2017
220
689
Na

Augustino Chiwinga

TUUJUE UJAMAA

Ujamaa ni siasa iliyoanzishwa kwa misingi ya sera za Hayati Julius Nyerere za maendeleo ya kijamii na ya ki uchumi katika Tanzania punde tu baada ya
Tanganyika kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka
1961 .
Ujamaa ni imani kama ilivyo imani za dini. Wanachama wanatakiwa waijue kikamilifu imani na kuishika, kama wanavyoshika imani zao za kidini.

Katika ujenzi wa Ujamaa walitakiwa viongozi bora (si bora viongozi), ambao wanakiri kwamba Ujamaa ni utu, kama walivyo viongozi wa kidini, wanakiri kwamba uongozi ni kuonesha njia. Kiongozi hawezi kuonesha njia kama hakuandaliwa.
Na ndio maana CCM iko mbioni kuanzisha Chuo chake kitakochokua kinawapika makada wake kwenye masuala ya uongozi na mtu hataruhusiwa kushika nafasi za uongozi kama hatopitia katika chuo hicho.

Mwaka 1967 Rais Nyerere alichapisha mwongozo wa maendeleo yake, ambao uliitwa Azimio la Arusha .
Azimio linaeleza dhana ya ujamaa kwa ufasaha kabisa linasema;
"Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanya kazi; haina ubepari wala ukabaila. Haina tabaka mbili za watu: tabaka la chini la watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka la juu la watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi. Katika nchi ya Ujamaa kamili mtu hamnyonyi mtu, bali kila awezaye kufanya kazi hufanya kazi, na kila mfanya kazi hupata pato la haki kwa kazi aifanyayo na wala mapato ya wafanya kazi mbali mbali hayapitani mno."

Dhamira ya Azimio ilikuwa kuzuia misingi hii ya kibepari isipanuke na kuenea. Azimio likaenda mbali kwa kuchukua hatua ili misingi ya kibepari isipanuke na kupanda misingi ya kujenga Ujamaa. Hatua hizi zilikuwa za awali kabisa na muhimu kati ya hizo ni:
Utaifishaji wa njia kuu za uchumi na kuweka umiliki na umenejimenti wake katika mikono ya Serikali au dola kwa maana ya kwamba dola ndio lilikuwa limechukuliwa kama mwakilishi wa wafanyakazi na wakulima, yaani chombo cha umma.

Sera ya kujitegemea badala ya utegemezi kwa maana ya kutegemea misaada na mikopo kutoka nchi za nje. Umuhimu wa kujitegemea ulikita kwenye mambo mawili: moja, kwamba huwezi ukawa na uhuru wa kujiamulia mambo yako kama unamtegemea mwingine; na, pili, kwa vyovyote vile, hakuna mjomba huko nje ambaye atakusaidia kukuletea maendeleo.

Gurudumu la maendeleo ni wafanyakazi na wakulima; kwa hivyo kwa mambo yote muhimu matabaka haya ya chini ndiyo yategemewe; yashirikishwe katika vyombo vya maamuzi na yapewe kipau mbele katika kuwapatia huduma za kijamii – afya, elimu, maji n.k. Kwa maneno mengine, maendeleo yawe maendeleo ya watu, si vitu au watu wachache.
Azimio lilitambua kwamba haitoshi kuweka umiliki wa njia kuu za uchumi katika mikono ya dola kama dola yenyewe si dola ya wafanyakazi na wakulima.

Azimio pia lilimtaka kiongozi na mtendaji wa ngazi ya juu na kati ya dola na mashirika yake pamoja na ya chama asiwe bepari au kabaila na asiweze kutumia nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali au kuishi maisha ya anasa kwa jasho la wananchi. Ndiyo maana Azimio likaweka *miiko ya uongozi*. Kwamba kiongozi:

Asiwe na hisa katika makampuni yoyote.

Asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.

Asiwe na mishahara miwili au zaidi.

Asiwe na nyumba ya kupangisha.

Mwalimu Nyerere alitumia Ujamaa kama msingi wa mradi wa maendeleo ya taifa. Aliitafsiri dhana ya Ujamaa kuwa mfumo wa usimamizi wa kisiasa na wa kiuchumi kwa namna mbalimbali kama;

1. Kuweka kwa mfumo thabiti wa kisiasa ili kusaidia katika kuimarisha mshikamano wa kujitegemea kwa
Tanzania iliyokuwa tu imejipatia uhuru.

2. Ustawishaji wa usawa kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuweko kwa demokrasia kuu; kukomesha
ubaguzi kwa misingi ya hali ya mtu; na kuzifanya sekta muhimu za uchumi kufikia taifa zima .

3. Kupeleka uzalishaji katika vijiji, ambapo ilifanya uwezo wa uzalishaji wa aina zote kufanyika kwa pamoja.

4. Kukuza kujitegemea kwa Tanzania kwa njia mbili: mabadiliko ya kiuchumi na mitazamo ya ki utamaduni . Kiuchumi, kila mtu angekifanyia kikundi chote kazi na kujifanyia yeye mwenyewe; kiutamaduni, ni lazima Watanzania wajifunze kujikomboa kutoka kwa
utegemezi wa nchi za Ulaya . Kwake Nyerere, hii ilijumuisha Watanzania kujifunza kujifanyia mambo wao wenyewe na kujifunza kuridhika na kile ambacho wangeweza kufikia kama nchi huru .

5. Utekelezaji wa elimu bila malipo na ya lazima kwa Watanzania wote ili kuwahamasisha wananchi kuhusu kanuni za Ujamaa.

Uongozi wa Julius Nyerere uliivutia Tanzania macho na heshima ya kimataifa kutokana na msisitizo wake wa maadili kama msingi wa maamuzi ya siasa . Chini ya Nyerere Tanzania ilipiga hatua kubwa katika vipengele mbalimbali vya maendeleo: vifo vya watoto vilipungua kutoka 138 kwa 1000 waliozaliwa hai mwaka 1965 hadi 110 mwaka 1985; tarajio la kuishi lilipanda kutoka miaka 37 (1960 ) hadi 52 (1984 ); uandikishaji wa wanafunzi katika shule ya msingi ulipanda kutoka 25% (16% tu kwa watoto wa kike) mwaka 1960 hadi 72% (85% kwa watoto wa kike) mwaka 1985 (ingawa idadi ya wananchi ilikuwa inaongezeka kwa kasi); asilimia ya watu wazima waliojua kusoma na kuandika ilipanda kutoka 17% mwaka 1960 hadi 63% mwaka 1975 (juu sana kuliko nchi nyingine za Afrika) ikaendelea kupanda.

NINI MAANA YA UBEPARI.

Nikitumia msamiati wa Azimio la Arusha, ubepari ni mfumo wenye tabaka mbili: ‘tabaka la chini la watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka la juu la watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi.’ Wanaoishi kwa kufanya kazi ndio wavujajasho na wanaoishi kwa kufanyiwa kazi ndio wavunajasho. Kwa maana hii, msingi mkuu wa mfumo wa kibepari ni unyonyaji wa kitabaka. Na unyoyaji hautokani na nia mbaya ya mtu binafsi bali ni msingi wa mfumo wenyewe bila kujali nia au dhamira za watu waliomo katika mfumo huo.
Matabaka haya mawili ni matabaka makuu ya mfumo ambao huainisha mfumo huo wa uzalishaji kama ubepari. Lakini pia, katika hali halisi ya nchi au jamii, kutokana na historia yake, kunaweza kukawa na matabaka mengine ya kati na ya chini na pia aina mbalimbali za vikundi vya kibepari na wafanyakazi. Kwa mfano, kuna tabaka la kati ambalo katika siasa-uchumi huitwa vibwanyeye, au kwa Kiingereza petty bourgeoisie . Kwa lugha nyepesi tunaweza tukayainisha matabaka haya matatu kama walalaheri, walalahai na walalahoi.
Ili mfumo wa ubepari uendelee yaani uwe endelevu hakuna budi bepari ajilimbikize mtaji unaotokana na ziada anayonyonya kutoka kwa wafanyakazi. Na mtaji huo anautumia kuwekeza ili kuendelea kumnyonya mvujajasho. Ulimbikizaji mtaji ndio kiini cha mfumo wa kibepari. Uhai wa bepari kama bepari hutegemea ulimbikizaji. Bila ulimbikizaji bepari hawezi kuishi kama bepari
.
Maslahi ya matabaka hugongana kwa sababu daima wavujajasho hutaka kupunguza juhudi yao ya kuzalisha ziada wakati, kwa upande mwingine, bepari hutaka ziada zaidi na zaidi. Migongano hii ya maslahi ya kitabaka ndiyo huzaa mapambano ya kitabaka. Ingawa mapambano haya huchukua sura mbalimbali, kamwe huwezi ukawa na mfumo wa kitabaka ambao hauna mapambano. Ili kuthibiti mapambano hayo yasije yakapasua mfumo wenyewe, unahitaji chombo cha mabavu; chombo hicho ni dola. Na dola hutafuta uhalali wa kisiasa ili matumizi ya mabavu yakubalike kwa wote ingawa kiini chake ni kuulinda mfumo wa kibepari.

SIFA 3 ZA MFUMO WA UBEPARI.

1.Mfumo wa kitabaka wenye matabaka mawili makuu, tabaka la wavujajasho ambalo huzalisha ziada na tabaka la wavunajasho ambalo hunyonya ziada. Ulimbikizaji na uwekezaji wa mtaji ambao hutokana na ziada ili kuendeleza uzazi wa mfumo wenyewe.

2.Migongano ya maslahi ya kitabaka ambayo huzaa mapambano ya kitabaka.

3.Chombo cha kisiasa, yaani dola, ambacho huhodhi mabavu, kuyadhibiti mapambano ya kitabaka kwa minajili ya kuhakikisha kwamba mfumo haupasuki au kupinduliwa.

UFISADI

Je, ufisadi ulikuwapo enzi za Mwalimu? Hapana haukuwapo. Je, rushwa ilikuwapo? Ndiyo ilikuwapo. Wakati wa Mwalimu wala hatukuwa na msamiati wa ufisadi. Kwa hivyo, Mwalimu hakuzungumzia ufisadi; lakini alizungumzia sana rushwa. “Rushwa ni adui wa haki,’ alirudiarudia kusema. Sasa tofauti ni nini?
Rushwa ni kishawishi unachotoa ili mpokeaji aipinde sheria au taratibu rasmi kwa kumrahisishia mambo yake mtoaji. Mtu akimpa chochote tarishi wa mahakama ili amtafutie faili lake au alifiche faili la mpinzani wake, hii ni rushwa. Bila shaka hongo yenyewe ni ndogo na mpokeaji ataitumia kwa mahitaji yake ya lazima au ya binafsi. Rushwa ya aina hii ilikuwapo wakati wa Mwalimu lakini haikuzagaa sana isipokuwa ilianza kuongezeka katika kipindi mwishoni mwa miaka ya 1970 na 1980. Hata hivyo rushwa ni rushwa haijalishi kwa ukubwa wake au udogo wake yote ni makosa yanyastahili mtu kupelekwa mahakamani ja kufungwa.

Mtumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) akikupatia nafuu katika kiwango cha kodi kwa kushawishiwa na hongo, hii pia ni rushwa. Lakini hongo hili ni ya mamilioni, itatumika kwa ajili ya kujenga nyumba ya anasa au kumnunulia gari kimada wa mpokeaji. Rushwa ya aina hii ilikuwa nadra wakati wa Mwalimu, lakini pia ilianza kuongezeka mnamo miaka ya 1980.
Mtumishi mkuu wa serikali au kiongozi wa kisiasa akipewa asilimia kumi yake ili arahishishe utoaji wa leseni ya madini, au utoaji wa eneo la mbuga kwa ajili ya uwindaji wa kitalii, au kumuuzia mtoaji shirika la umma kwa bei ya kutupa, hii pia ni rushwa. Lakini hi si hongo kidogo na kuna uwezekano mkubwa kwamba itatumika kwa ajili ya kujilimbikizia mali au mtaji. Hii hasa ni ufisadi. Hii haikuwapo wakati wa Mwalimu kwa sababu mfumo wenyewe haukuwezesha kuwapo kwake.
Kutokana na kwamba mfumo wa kibepari unahusisha unyonyaji wenye lengo la kupatwa ukwasi hivyo ni wazi kwamba mfumo huu ndio chimbuko la ufisadi.
Wapo viongozi kwa makusudi kabisa waliamua kuuacha mfumo wa Ujamaa na kuanza kua mabepari na kupelekea kua mafisadi wa kutisha.
Mathalani unasikia kiongozi wa shirika la umma amejenga nyumba 72 zenye thamani kubwa katika eneo moja unaanza kujiuliza alijenga kwa fedha halali au za ufisadi , jibu lake ni alikua fisadi maana katika hali ya kawaida mshahara wake pekee usingeweza kujenga nyumba hizo.
Kilichosababisha viongozi kujilimbikizia mali ni ukosefu wa usimamizi thabiti na madhubuti.

Kwa kauli yake anayoipenda kuitumia mara kwa mara Mh.Dr John Pombe Magufuli ni kwamba "Tanzania iligeuzwa kua Shamba la bibi"
Na ndio maana alipoingia tu madarakani alianza na kazi ya kutumbua majipu kwa mafisadi walioliingizia hasara nchi hii wakiwemo watumishi hewa.
Hii ni ishara sasa Taifa linarudi katika misingi yake ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo rushwa na ufisadi hauna nafasi.
Ni wazi Mh Rais Magufuli ameanza kuitibu kansa ya hii ya ufisadi iliyoisumbua taifa kwa muda mrefu sana.
Pia hata alipofanya uteuzi wa viongozi mbali mbali tulishuhudia wakila viapo na kusaini hati za ahadi ya maadili na uadilifu.
Hii yote ni katika kuwakumbusha kua wanatakiwa kuishi katika maisha ya uadilifu siku zote na kuacha kujilimbikizia mali na kutanguliza maslahi ya nchi mbele.

Hapa Rais Magufuli ananikumbusha Hayati Mwalimu Nyerere labda tujiulize swali hili;Kwani wakati wa Mwalimu viongozi hawakuwa na tamaa ya hela? Walikuwa nayo, lakini wangefanya nini na mamilioni ya RICHMOND? Wasingeweza kujilimbikizia mali – walikuwa hawaruhusiwi. Wasingeweza kujijengea hekalu! Wangeyaficha wapi? Wangeulizwa kujieleza.

Hivi ndivyo ilivyo hata hivi sasa kwa Rais Magufuli ameweza kudhibiti ufisadi Tanzania kutokana na umadhubuti wake wa kuwasimamia kwa karibu viongozi haswa upande wa uadilifu.
Ukijilimbikizia mali enzi hii ya Magufuli utakwenda na maji.

Mh Rais Magufuli hakuishia kwenye Serikali tu, kwa kutambua kua Chama Cha Mapinduzi ndicho chama chenye dola huko nako akiwa yeye ni Mwenyekiti Taifa wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM- NEC walibariki hoja ya kufanya mabadiliko ya katiba ambapo baadaye yakaja kupitishwa na wajumbe wa Mkutano mkuu wa CCM, ambayo nayo yanasisitizia juu ya uadilifu kwa viongozi na wanachama wa CCM.
Mabadiliko hayo ya CCM mpya yamehuisha pia misingi ya Azimio la Arusha hususani kwenye miiko ya Uongozi mathalani suala la mishahara miwili, ambapo sasa CCM imeweka kipengele kinachozuia mtu mmoja kuhodhi madaraka mengi kwenye chama.Maana yake ni kwamba sasa ukiwa Mbunge huwezi tena kua mkuu wa Mkoa au ukiwa Mwenyekiti wa CCM mathalani wa Mkoa huwezi kua Mjumbe wa Halmashauri kuu-NEC.

Hii yote ni katika kuongeza uwajibika ufanisi na uadilifu.
Pia mabadiliko hayo yana dhamira ya kudhibiti vitendo vya rushwa katika michakato ya chaguzi za ndani ya chama.
Sasa CCM imerudishwa kwenye misingi ya kuanzishwa kwake ambao huko tunakutana na hii Itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo itatumika katika kuleta usawa wa kimaendeleo kwa jamii bila ya unyonyaji wa aina yeyote ile.

Mfano mmojawapo wa ujamaa ni kwenye suala la elimu bure ambapo sasa hakutakua na mtoto yoyote wa Kitanzania atakayeshindwa kwenda shule kwa sababu ya ada au michango ya aina yoyote.
Mh Rais Magufuli alihaidi hilo na ameshatekeleza kwa kutoa Fedha shillingi Billion 18 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia mpango huo wa elimu bure.
Kwenye suala la elimu hakuishia hapo bali pia alienda mbali kwa kuhakikisha kila shule inajitosheleza kwa madawati ambapo hadi hapa ninapoandika hakuna mwanafunzi asiyekalia dawati shuleni.
Upande wa Afya nako ni hivyo hivyo gharama za dawa zimepungua kwa kiasi kikubwa kwa kuamua kujenga maduka ya bohari ya dawa ya serikali kwenye Hospitali kusambaza sehemu nyingine kwa gharama ndogo zaidi ambacho mwananchi wa kawaida atazimudu.
Mpango kwa matibabu bure kwa wazee nao ni aina mojawapo ya ujamaa ambapo sasa wazee watakua watibiwa bure katika hospitali za umma.

Hatua pia za kuzuia kusafirisha mchanga wa dhahabu nje ya nchi ni hatua nzuri inayoakisi msingi wa ujamaa ambao ni USAWA katika kuhakikisha kwamba raslimali za Tanzania zinatumika kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya watanzania wote.
Pia imelenga katika kuhakikisha taifa linapata pato stahiki ili liweze kujitegemea katika kufanya mambo yake bila kutegemea wahisani wa nchi za nje.
Juhudi za Mh Rais Magufuli katika kudhibiti uporaji wa raslimali za Watanzania ni hatua nzuri katika kufikia lengo la taifa la kujitegemea lenyewe maana ukweli ni kwamba tukiweza kudhibiti mianya hii ya kuibiwa katika raslimali taifa litapata fedha nyingi zitakazoiwezesha kupanga na kutekeleza miradi yake kwa uhuru na kwa wakati kwani hatutategemea tena fedha kutoka nje.

Kwa hiyo katika uongozi wa Rais Magufuli naiona mbegu halisi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Maneno “Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea” yamepewa fasili ifuatayo katika ibara ya 151(1) ya Katiba ya Tanzani kua: “Ujamaa na Kujitegemea ni misingi ya maisha ya jamii ya kujenga Taifa linalozingatia demokrasia, kujitegemea, uhuru, haki, usawa, udugu na umoja wa wananchi.”
Na hivyo ndivyo Mh.Rais Magufuli anavyofanya katika kuliletea taifa maendeleo , namuona Magufuli kama mkombozi na tumaini jipya linalotembea juu ya misingi ya sera za Ujamaa na Kujitegemea .
Miradi mingi ya maendeleo ya inatekelezwa kwa fedha zetu za ndani na hata mapato yanayopatikana yanaelekezwa katika kushughulikia na kutatua kero za wananchi hususani wale wanyonge.
Na ndio maama Mh Rais Magufuli anasisitiza watu wafanye kazi kwa bidii, juhudi, na maarifa k ili taifa liweze kujitemea na kupata maendeleo anuai kwa haraka. Kila mtu atimize wajibu wake pale alipo

Augustino Chiwinga
 
naomba mifano ya miradi ya maendelea iliyoanza na kutekelezwa na JPM na mingapi kwa fedha za ndani. Ni maantiki ukiweka chanzo cha takwimu zako. Hatutaki maneno yale ya "hosteli kwa shs bilioni 10" lakini wakiombwa mchanganuo wanakataa.
 
.."shamba la bibi" ndiyo maana akauza nyumba za serikali kifisadi, na kununua meli mkweche huku akiudanganya umma kuwa ni meli mpya.
 
Back
Top Bottom