Je, ni kweli ugonjwa wa macho mekundu (Red eyes) huambikizwa kwa kutazamana?
- Tunachokijua
- Januari 15, 2023, Wizara ya Afya iliwaasa Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa macho mekundu (Red eyes), Maambukizi ya Kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis uliyoibuka nchini hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), Ugonjwa huu husababishwa na vitu vingi ikiwemo virusi, bakteria, mzio (Allergy), uwepo wa magonjwa mengine, fangasi na Kemikali mbalimbali.
Kwa mujibu wa utafiti, pamoja na uwepo wa visababishi vingi vya ugonjwa huu, adenovirus (aina ya virusi) ndio husababisha vusa vingi. Kwa ujumla wake, virusi huchangia takriban 75% ya visa vyote vya ugonjwa huu.
Uwepo wa viashiria vya Ugonjwa huu nchini
Taarifa ya Serikali iliyotolewa Januari 15 ilitanguliwa na uwepo wa taarifa mitandaoni zilizochapishwa na watu mbalimbali.
Mathalani, Januari 13, mdau wa JamiiForums.com alitoa dokezo linalohoji juu ya uwepo wa ugonjwa huu baada ya yeye kupata maumivu ya macho, na baada ya kupata ushauri wa daktari alifika kwenye duka la dawa (Famasi) na kukuta idadi kubwa ya dawa za macho zikiwa juu ya kaunta, na baadae kusikia mtaaani watu wengi wakilalamika.
Ugonjwa huu unaweza kuambukiza kwa kutazamana?
JamiiCheck imefuatilia njia za maambukizi za ugonjwa huu na kubaini kuwa hauwezi kuambukizwa kwa kutazamana.
Taarifa ya Wizara ya Afya iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, Januari 16, 2023, ilibaibisha njia mbili zinazoweza kusambaza ugonjwa huu ambazo ni kupitia kugusa tongotongo au machozi kutoka kwenye macho ya mtu mwenye maambukizi au kupitia kugusana mikono na mtu mwenye maambukizi au kwa kugusa sehemu au kitu ambacho kimeguswa au kuapata machozi au tongotongo.
Taarifa hii ilibainisha pia kuwa dalili zake huanza kuonekana kuanzia siku 5 hadi 14 baada ya kupata vimelea vya maambukizi. Aidha, mara chache inaweza kuchukua muda mrefu zaidi.
Kwa mujibu wa American Academy of Opthalmology, ugonjwa huu kwa lugha rahisi husambaa kwa kugusa kitu au mtu aliyeambukizwa. Aidha, haiwezekani kuupata ugonjwa kwa kutazamana pekee.
Hata baada ya kupitia vyanzo vingine vya kuaminika, JamiiCheck haijapata uthibitisho wa uambukizwaji wa ugonjwa huu kwa njia ya kutazamana.
Dalili za ugonjwa
Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, macho kutoa machozi na kutoa tongo tongo za njano.
Dalili hizi zinaweza kutofautiana ukubwa kati ya mtu mmoja na mwingine.
Matibabu
Taarifa za uchunguzi zinaonesha Maambukizi ugonjwa huu hasa ukisababishwa na Kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho, ujulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” husambaa kwa kasi kubwa.
Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba dalili huisha zenyewe ndani ya muda mfupi, ambao unaweza kufikia hadi wiki mbili.
Jinsi ya kujikinga
Katika kujikinga na ugonjwa huu, Wizara ya Afya ya Tanzania inashauri kufanya mambo yafuatayo:
- Jizuie usiguse macho yako kadri uwezavyo. Iwapo utagusa macho yako, nawa mikono na maji tiririka na sabuni.
- Jizuie usiguse mtu mwingine isipokuwa tuu pale unapokuwa
umetoka kusha mikono yako na maji tiririka na sabuni - Tupa au safisha kwa makini (kwa maji moto na sabuni) vitu vilivyogusa macho yako.
- Usichangie vipodozi na vitu vingine unavyotumia kama vile taulo za karatasi au nguo au dawa za macho
- Tumia taulo tofauti na leso tofauti kwa kila mwana familia.
- Funika mdomo wako na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
- Watoto wadogo wagoniwa wanaoenda shule wanashauriwa wakae nyumbani hadi dalili zinapoisha kwa kuwa ni ngumu kuzuia maambukizi yasisambae kwenye mazingira ya shule.