BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,115
Posted Date::5/30/2008
Ufisadi BoT chamtoto
*Ripoti yabaini Sh 700 bilioni zachotwa kila mwaka
*Hii ni sawa na robo ya makusanyo ya kodi
*50% ya akinamama hujifungua kwa wakunga wa jadi
*Ajira milioni za Kikwete yadaiwa kiini macho
Na Muhibu Said
Mwananchi
WAKATI serikali ikiugulia maumivu ya upotevu wa Sh133 bilioni kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimedai kuwa serikali hupoteza Sh700 bilioni kwa mwaka kwa sababu ya rushwa.
Katika ripoti yake ya hali ya haki za binadamu Tanzania Bara na Zanzibar ya mwaka 2007, LHRC imedai upotevu wa kiasi hicho cha fedha, hutokea katika sekta za Ugavi na Manunuzi ya Umma. Fedha ambazo zinadaiwa kuibwa kila mwaka kutoka serikalini, zinaweza kugawiwa kwa kila Mtanzania Sh20,000 kwa idadi ya watu 35 milioni kwa sasa.
Ripoti hiyo ambayo ni ya saba kutolewa na LHRC, inafuatia utafiti juu ya hali ya haki za binadamu Tanzania Bara na Zanzibar, uliofanywa na kituo hicho, mwaka jana.
Uzinduzi wa ripoti hiyo ulifanywa na Mwakilishi wa Balozi wa Sweden nchini, Andreas Ershammat, Makao Makuu ya Kituo hicho, jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na Profesa Haroub Othman ambaye aliwakilisha Kituo cha Msaada wa Sheria cha Zanzibar (ZLSC) .
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Helen Kijo-Bisimba alisema katika uzinduzi huo kuwa, taarifa ya mwaka jana ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Mahesabu ya Fedha za Serikali (CAG), imethibitisha kuwapo matumizi mabaya ya fedha katika sekta hizo.
"Hata ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka huu, inaonyesha kuwa kuna matumizi mabaya ya fedha za serikali katika Sekta za Ugavi na Ununuzi wa Umma," alisema Kijo-Bisimba.
Akisoma muhtasari wa ripoti hiyo katika uzinduzi huo, Afisa Mipango wa LHRC, Clarence Kipobota aliinukuu Taasisi ya Kupambana na Viashiria vya Rushwa nchini (FACEIT), ikieleza kwamba mwaka 2007, iligundua kuwa kati ya asilimia 70 na 90 ya malipo yaliyofanywa katika mamlaka za ugavi na manunuzi ya umma, kulikuwa na viashiria vya rushwa.
Kipobota ambaye pia ni mmoja wa wanasheria na wakili wa LHRC, alisema kwa mujibu wa FACEIT, inakadiriwa kwamba, rushwa kwa mwaka uliopita, imeligharimu taifa kiasi cha Sh700 bilioni ambazo ni karibu asilimia 25 ya makusanyo ya kodi ya mwaka mzima.
Maelezo hayo ya FACEIT, yamerejewa kwenye ripoti hiyo ya LHRC, ukurasa wa 125.
Hata hivyo, CAG, Ludovick Utouh, alipotafutwa jana ili kuelezea suala hilo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi, ilikuwa imezimwa.
Awali, Kijo-Bisimba alisema mwaka 2007, umeshuhudia rushwa kubwa zikitokea, huku serikali ikiingia mikataba mibovu ya madini na makampuni ya nje.
Pia wananchi wameshuhudia rushwa katika mikataba mibovu ya umeme, kama vile Richmond, hali ambayo alisema inatishia mustakabali wa nchi.
Akifafanua, Afisa Mipango wa LHRC, Kipobota alisema utafiti huo umebaini kuwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (PCCB), ni wazito na waoga katika kutekeleza wajibu wao.
"Wanasubiri mpaka wapelekewe mtuhumiwa, hata wakipelekewa hawamshughulikii ipasavyo," alisema Kipoboto.
Kijo-Bisimba alisema mwaka 2007, ulikuwa ni wa 59 wa maadhimisho ya Tamko la Haki za Binadamu na pia wa maadhimisho ya miaka 23 tangu haki za binadamu ziingizwe kwenye Katiba ya nchi.
Hata hivyo, alisema pamoja na miaka mingi kiasi hicho, bado wameona kuna mapungufu mengi juu ya utekelezaji wa haki za binadamu.
Alisema kwa mfano, pamoja na ahadi nzuri zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2007, ikiwamo kushughulikia migogoro kati ya vyama vya siasa, migogoro hiyo bado ipo na imekuzwa mno katika awamu hii.
Vilevile, alisema katika kuboresha hali ya kipato kwa wananchi, hadi sasa serikali bado haijafanikiwa, huku maisha yakizidi kuwa magumu kwa kiasi kikubwa.
"Maisha yamekuwa magumu kupita kiasi. Ahadi ya ajira za milioni moja zimekuwa kiini macho," alisema Kijo-Bisimba.
Akifafanua, alisema utafiti umeonyesha kuwa kwa mwaka wanaohitimu katika vyuo vya elimu ya juu nchini, ni wanafunzi 700,000 na kwamba, kati yao, wanaoajiriwa katika sekta rasmi ni 40,000 pekee.
Kutokana na hali hiyo, alisema wanakadiria kuwa Rais Kikwete, katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake, atakuwa ametengeneza ajira zisizozidi 250,000, kinyume na ajira milioni moja alizoahidi.
Januari 7, mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kapteni John Chiligati aliwaambia waandishi wa habari kuwa, tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani mwaka 2005, imefanikiwa kutoa ajira zaidi ya laki nne kati ya milioni moja ilizoahidi kuzitoa kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Waziri Chiligati alisema hayo alipokuwa akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika wizara yake katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Alisema hadi kufikia Septemba, mwaka jana, ajira 401,390 kati ya milioni moja zilizoahidiwa na serikali katika kipindi cha miaka mitano, zimepatikana, huku sekta binafsi ikiongoza kwa kutoa mchango mkubwa katika utoaji wa ajira kwa wananchi.
Hata hivyo, Waziri Chiligati hakueleza sekta ambazo ajira hizo zimetolewa, badala yake, alisema serikali itaendelea kutoa ajira katika sekta mbalimbali, ikiwamo elimu, afya, kilimo, mifugo pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama.
Kijo-Bisimba alisema mwaka 2007, pia uliongoza kwa uvunjaji wa haki za binadamu ambapo polisi walitumia nguvu kupita kiasi wakati wa kushughulikia tatizo la ujambazi nchini.
"Watu waliodhaniwa kuwa ni majambazi 14 kutoka Kenya waliuawa kikatili ambapo polisi wangeweza kutumia mbinu nyingine katika kuwakamata," alisema Kijo-Bisimba.
Alisema katika mwaka huo, pia ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza nchini, wafungwa wakigoma karibu nchi nzima wakidai haki zao, kutoridhishwa na utendaji wa maafisa wa magereza na mahakama, upelelezi kucheleweshwa na kutoridhishwa na dhamana.
Akifafanua, Kipobota alisema utafiti huo umebaini pia kuwa magereza nchini yanachukua wafungwa kupita uwezo wake ambapo gereza linalotakiwa kuchukua wafungwa 22,000, linachukua wafungwa 46,000.
Alisema kwa mfano, chumba cha Gereza la Ngudu, mkoani Mwanza, kinatakiwa kihifadhi wafungwa 64, lakini kinahifadhi wafungwa 124.
Kipobota alisema utafiti huo umebaini pia kuwa asilimia 50 ya wanawake nchini, bado wanaendelea kuzalia kwa wakunga wa jadi katika miaka zaidi ya 40 ya uhuru.
Alisema imebainika pia kuwa maambukizi mengi ya ugonjwa wa ukimwi, yako vijijini tofauti na mijini, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa elimu, imani za kishirikina, mila na desturi na upungufu katika sheria ya ukimwi.
Kipobota alisema Aprili, mwaka 2006, Rais Kikwete aliahidi kushughulikia marekebisho ya sheria inayowanyima haki ya kupiga kura wananchi walioko nje ya vituo vya kupiga kura, kama vile wafungwa na wanaoishi nje ya nchi, lakini hadi mwaka 2007, unaisha, ahadi bado haijatekelezwa hadi sasa.
Ripoti hiyo yenye kurasa 189, imegawanywa kwa sura 11 ambapo sura ya kwanza inatoa maelezo ya jumla ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Sura ya pili hadi ya kumi, inachambua mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa haki za binadamu bara katika nyanja mbalimbali wakati sura ya 11 inatoa maelezo ya haki za binadamu Zanzibar.