Ufafanuzi wa hoja tata kuhusu katiba inayopendekezwa

Mar 7, 2015
21
1
UFAFANUZI WA HOJA TATA KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA


MAKALA NO. 9



Katika mchakato wa kuitafuta katiba mpya, kumekuwepo na hoja ambazo zinaonesha kwamba kutokuwepo kwa mambo hayo katika katiba inayopendekezwa nisababu ya katiba kukosa ubora na kwamba hata baadhi ya hayo yaliyowekwa katika katiba pendekezwa bado hayajakidhi haja. Msingi mkuu wa hoja za namna hii unajikita zaidi kwenye malalamiko kwamba haya nimambo muhimu yaliyokuwemo kwenye rasimu ya Tume nakwamba bunge maalum la katiba liliyatupilia mbali.


Kwa manufaa ya watanzania wote ninafafanua kwa kuweka hadharani hoja hizo pia kuzitolea ufafanuzi pia uthibitisho ili watu waelewe ukweli na uongo ni upi.


Kuhusu Wabunge kuwajibishwa na wananchi
Rasimu ya Tume ilipendekeza kwa bunge maalum kwamba kutokana na malalamiko ya wananchi kutohudumiwa vema na wabunge wao, ipo haja ya wabunge wanamna hii kuwajibishwa na wananchi waliowachagua ili kuhakikisha uwajibikaji unakuwepo. Hata mimi ninapenda mbunge awajibishwe iwapo hatimizi wajibu wake. Ibara ya 129(c) ya rasimu ya Tume ilielekeza kwamba iwapo mbunge ataacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la jimbo la uchaguzi kwa muda wa miezi sita bila sababu za msingi iwe nisababu ya wananchi kumwajibisha kwa kutolewa madarakani. Ibara hii ilikuwa inatoa mwanya wa mbunge kufanyiwa hila za kutolewa madarakani kirahisi kutokana na ukweli kwamba sababu za mtu kuishi mahala fulani kwa kiasi kikubwa nisababu binafsi na ni uhuru wa mtu mwenyewe na inategemea pia sababu nyingi za kijamii ambazo pia mbunge nimwanajamii. Maisha yana siri nyingi binafsi ambazo siyo lazima ziwe wazi kwa watu wote. Mtu mwenyewe ndiye anaweza kujua sababu zakumfanya kuishi au kutoishi sehemu Fulani.

Vilevile ubunge nikazi na ni utumishi kama zilivyokazi nyingine tofauti yake na ajira nyingine nikwamba mbunge nimwajiriwa wa kisiasa. mfano maeneo ya mijini majimbo yanakaribiana sana kijiografia kiasi kwamba hakuna umbali mkubwa wamtu kutoka jimbo moja kwenda jimbo jingine pia hata vijijini hali ni ileile kwamba mpaka wa wilaya moja nimwanzo wa wilaya nyingine.

Ifahamike kwamba mbunge ana ofisi ambayo iko kwenye jimbo lake ambayo ndiyo kiunganishi chake pamoja na wananchi wake nasiyo makazi yake binafsi. Mbunge hafanyii kazi nyumbani kwake. Kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume siyo rahisi kujua sababu zisizo za msingi na zile zamsingi kwa kuwa kuishi sehemu Fulani kunategemea sababu binafsi hata hivyo Tume ilishindwa kuanisha mifano ya sababu hizo zisizo za msingi. Kwa upande mmoja upo umuhimu wa mbunge kuishi katika jimbo lake ila haina mantiki kumtoa mbunge madarakani kwa kuhamisha makazi yake nje ya jimbo lake. Makazi ni suala binafsi na siyo la kijamii wala kisiasa au msingi mkuu wa utumishi wa mtu.


Kwa upande wangu ninaungana na marekebisho yaliyofanywa na bunge maalum la katiba kufuta kipengele hiki kwa kuwa hakikulenga kuleta maelewano baina ya mbunge na wananchi wake, pia hakikuwa nadhana ya kumpa uhuru wa kuishi popote mbunge akiwa ni raia wa Tanzania na nihaki ya kikatiba. Mapendekezo haya ya Tume hayakuzingatia uhalisia kwamba mbunge anachaguliwa kila baada ya miaka mitano na kuna uwezekano wa mbunge wakipindi hiki kutokuwa mbunge wakipindi kijacho.


Ilikuwa ni busara Tume kupendekeza kwamba serikali ijenge nyumba za wabunge kwenye majimbo kwa kuwa niwatumishi wa wananchi kupitia siasa kuliko katiba kumfunga mbunge na kumyima uhuru wa kuishi sehemu aitakayo kama Tume ilivyokuwa imependekeza.


Kuhusu mbunge kupoteza sifa zakuwa mbunge Katika Ibara ya 128(d) rasimu ya Tume ilipendekeza mambo yanayoweza kumfanya mbunge apoteze sifa kwamba ni iwapo atapata maradhi kwa kipindi cha miezi sita mfurulizo au kuwa gerezani kwa muda kama huo. Ninaungana na mapendekezo ya mbunge kupoteza sifa kwa kuwa gerezani iwapo amehukumiwa au la ila siyo kwa kipengele cha maradhi. Kuugua ni tukio lisilo la ridhaa ya mtu mwenyewe pia wakati wa maradhi mgonjwa anatakiwa kufarijiwa na siyo kuumizwa.


Pendekezo la namna hii ninaliita la kikatili kwa kuwa halikujali afya ya mtu na utu ila maslahi ya kisiasa ndiyo yaliangaliwa zaidi na Tume. Hivi kweli iwapo mbunge amewatumikia wananchi wake vizuri kwa muda wa miaka minne au mitatu mfurulizo na katika kipindi cha kuelekea mwishoni mbunge akaugua tena wakati mwingine kwasababu za kuwatumikia wananchi wake itakuwa nisahihi aondolewe? Huu ni ukatili na unyama wakisiasa ambao bunge maalum halikutakiwa kuukubali kabisa kama lilivyofanya.


Ninakubaliana na ibara ya 143(1) (d) kama ilivyofanyiwa marekebisho na bunge maalum kuondoa kipengele cha mbunge kupoteza sifa kwa kuwa namaradhi na badala yake kubakiza kipengele cha mbunge kupoteza sifa kwa kuwa gerezani kwa muda usiopungua miezi sita mfurulizo. Kwa jinsi watu wanavyopenda ubunge bila shaka wangerogana ili mbunge augue muda mrefu atolewe nawengine waingie, kwa mazingira ya uchu wa madaraka waliyonayo watu, kipengele hiki kingetoa mwanya wakuhatarisha afya za wabunge wengi.

Hatuwezi kuwa na katiba ya ajabu isiyojali utu wa watu kama Tume ilivyokuwa imependekeza kuhusiana na jambo hilo.
Nivema ifahamike kwamba katiba ipendekezwa ibara ya 160-161 imeundwa Tume ya utumishi wa bunge ambayo inajukumu la kushughulikia masuala yote ya utumishi wa wabunge pia mbunge asiyetimiza wajibu wake kwa wananchi iko wazi kwamba hukumu yake ni kupitia uchaguzi kwa wananchi kumkataa kumchagua tena. Pia katiba pendekezwa katika ibara ya 228(1) imeunda Tume ya maadili ya viongozi ambayo ninashauri Bunge litunge sheria itakayoipa meno Tume hii kuwashughulikia pia wabunge kwa kuwa nawao ni watumishi wa umma kupitia siasa.


Kuhusu wajumbe wa baraza la wawakilishi kujadili mambo yote ndani ya bunge la Jamhuri ya muungano hata yasiyo ya muungano Hoja hii haizingatii uhalisia na mantiki ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania pamoja na dhana ya bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Jamhuri ya muungano wa Tanzania niyenye muundo wa serikali mbili ambazo ni Jamhuri ya muungano pamoja na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar. Katika muundo wa serikali hizi mbili bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania linayo mamlaka ya kuzisimamia serikali zote mbili kwa mambo yamuungano na kwa upande mwingine halina mamlaka ya kuisimamia serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya muungano. Pia bunge la jamhuri ya muungano linayo mamlaka kuisimamia serikali ya jamhuri ya muungano yaani Tanzania Bara kwa mambo yasiyo ya muungano.


Ifahamike kwamba Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ni sehemu ya bunge na anachaguliwa na wananchi wasehemu zote mbili za muungano na bunge linayo mamlaka ya kumwajibisha Rais kupitia wabunge. Hoja hii naiita ya kibaguzi kwasababu imejikita zaidi kwenye fikra za utanganyika na uzanzibar na siyo utanzania. Bunge ni Taasisi ndiyo maana kuna watu wengine ambao siyo wabunge lakini wanaingia bungeni kutokana na jukumu la bunge kuwa kubwa kwa maslahi ya Taifa. Mbona hili haliulizwi? Bunge kama Taasisi linakazi nyingi zaidi ya mijadala inayoendeshwa bungeni nayote yanafanyika kwa maslahi ya Taifa nasiyo majimbo tu. Muundo wa bunge siyo wakimajimbo niwakitaifa ndiyo maana pia wapo wabunge wakuteuliwa ambao hawatokani na majimbo lakini wanaingia bungeni. kwa fikra hizo je, hawa nao wanajadili nini ikiwa hawana majimbo?


Nisahihi kabisa kwa baadhi ya wajumbe wabaraza la wawakilishi kuingia na kujadili hoja zote ndani ya bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania na ndo maana likaitwa “bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania, ni bunge la nchi nasiyo bunge la serikali. (siyo bunge la serikali ya jamhuri ya muungano). kwa mtu mwenye fikra za utanganyika na uzanzibar nisahihi kwake kuleta hoja kama hii ya ubaguzi ila siyo kwamwenye fikra za utanzania.


Kuhusu madaraka ya Rais kwamba Rais ana madaraka makubwa sana. Hoja hii nimiongoni mwa hoja zinazochukua nafasi kubwa katika kuijadili katiba inayopendekezwa na inachukuliwa kuwa sababu yakuipinga katiba inayopendekezwa. Zipo hoja kwamba Rais ameendelea kuwa na madaraka makubwa ambayo anaweza kuyatumia vibaya nakwamba katiba inayopendekezwa haifai kwa sababu hii.


Katika nchi yoyote yenye misingi ya kidemokrasia, wananchi ndiyo msingi mkuu wa mamlaka ya nchi na Rais huchaguliwa na wananchi hao. Ibara ya 7(1) yakatiba inayopendekezwa inaweka wazi kwamba wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote. Haileti maana Rais aliyechaguliwa nakuaminiwa na watu wengi zaidi akose madaraka ya kuamua mambo muhimu kwa mustakabali wa Taifa. Hoja ya msingi kuhusu suala hili inatakiwa ijielekeze kuangalia kama mamlaka ya Rais yanadhibitiwa kikatiba au la. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo Rais wake hana madaraka makubwa isipokuwa madaraka yale huwekewa mfumo wa kuyadhibiti ili yasitumike vibaya.

Nafasi ya Rais katika utumishi wa umma ni nafasi kubwa naya juu sana hivyo lazima awe na madaraka makubwa. Haiwezekani nafasi ya Rais ikawa kubwa alafu mwenye nafasi hiyo akawa na madaraka madogo. Gari kubwa lazima liwe na injini kubwa, matairi makubwa, spare nzito na kubwa, gharama yake nikubwa pia hata mafuta lazima linywe mengi, isipokuwa pamoja na ukubwa wote huu lazima litumike kwa kuzingatia sheria za nchi.


Kwa mujibu wa katiba inayopendekezwa mamlaka ya Rais yamedhibitiwa kikatiba. Katika mamlaka yake ya Amir jeshi mkuu katiba inamtaka Rais kuleta azimio bungeni la kutaka nchi kuingia vitani ili kukubaliwa au kukataliwa na bunge. Ibar ya (83) inaweka ukomo wa uhuru wa Rais kwamba atalazimika kufuata ushauri pale katiba hii inapomtaka hivyo au kwa mujibu wa sheria nyingine yoyote itakayomtaka kuzingatia ushauri kabla ya kufanya jambo Fulani.


Ibara ya 97(1) bunge limepewa mamlaka ya kumshitaki na kumondoa Rais kwa matendo ya kukiuka katiba hii pia kuhusu uteuzi wa viongozi waandamizi wa serikali, Rais amepunguziwa madaraka ya kuwateua mojakwamoja viongozi hao. Katiba imeweka kamati mbalimabli za uteuzi wa viongozi waandamizi waserikali ambapo kamati zitapendekeza majina na kumpelekea Rais kufanya uteuzi kutoka miongoni mwa watu ambao kamati husika inaona wana sifa, kwahiyo kimsingi Rais atateua baada ya kamati za uteuzi kupendekeza majina yanayofaa
.

Pia katiba haijampa Rais uwezo wa kuyakataa mapendekezo hayo yatakayofanywa na kamati ya uteuzi. Mfano mzuri unajidhihirisha katika ibara ya 218, pia zipo ibara nyinine zenye maudhui ya namna hii. Hata kuhusu waziri mkuu ibara ya 110(2) ya katiba inayopendekezwa inaeleza wazi kwamba Rais atapeleka jina bungeni ili liungwe mkono na wabunge waliowengi. Hivyo siyo kweli kwamba Rais ana madaraka makubwa sana kama inavyoelezwa na baadhi ya watu. Kuhusu ukomo wa wabunge


Rasimu ya Tume katika ibara ya 125(2) (a) ilipendekeza kwamba ukomo wa mtu kugombea ubunge uwe ni vipindi vitatu vya miaka mitano yaani mwisho iwe ni miaka 15.mapendekezo kama haya ninayaita ya ubaguzi na hayakuzingatii democrasia ya kisiasa. Mbunge anachaguliwa na wananchi na hawana mkataba naye wakudumu wanaweza kumtoa kwa kutomchagua tena hata kwa miaka mitano ya mwanzo iwapo hawakuridhika naye. Vilevile mapendekezo kama haya niya kumnyima mtu haki yake yakisiasa ya kuchagua na kuchaguliwa. Hivyo mapendekezo ya Tume kuhusu jambo hili yalikiuka misingi ya demokrasia.


Mapendekezo kama haya yangeungwa mkono iwapo nchi yetu isingekuwa na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Ingekuwa bado nchi inafuata mfumo wa chama kimoja hata mimi ningekubali mapendekezo ya Tume kwa kuwa ni ukweli kwamba upo uwezekano wa mtu kuchokwa na wananchi ila akapendwa na chama Katika mfumo wa Demokrasia ya vyama vingi ambapo vyama vya siasa husimamisha wagombea tofauti na mtu kupewa uhuru wa kumchagua amtakaye, mapendekezo kama haya ilikuwa nisahihi kwa bunge maalum la katiba kuyatupilia mbal, hayakuzingatia hali halisi ya matakwa ya kidemokrasia ila mapendekezo ya Tume kama vile yalilenga kupambana na CCM ambayo kiukweli inaowabunge ambao wamedumu kwa zaidi ya miaka 15 katika nafasi za ubunge.


Mbunge anaweza kugombea maranyingi awezavyo kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani ilimradi anakubalika kwa wapiga kura wake ikizingatiwa kwamba huu ni wakati wa siasa za ushindani wa vyama vingi ambapo wananchi wanakuwa na uwanja mpana wa kuchagua viongozi. Ubunge siyo kazi inayohitaji maamuzi magumu yanayoathiri watu wengi kwa wakati mmoja nayenye madaraka makubwa kama ilivyo ya Rais, maamuzi ya mbunge yamegawanyika katika ngazi ya Taifa nayajimbo. kipimo chake kikubwa kipo katika ngazi ya jimbo kabla ya kumwangalia mbunge kitaifa ambapo wananchi katika jimbo ndio wenye vipimo vya aina ya mbunge wanayemtaka. Hoja ya kwamba wapo wabunge wamekaa bungeni kwa muda mrefu hivyo hawafai haina maana kwa sababu wapo pia wabunge vijana ambao hawajakaa bungeni muda mrefu lakini wameshindwa kuwaletea maendeleo wananchi katika majimbo yao.


Kuhusu maadili ya viongozi na watumishi wa umma Siyo kweli kwamba misingi ya maadili kwa viongozi na watumishi wa umma haikuwekwa kwenye katiba pendekezwa. ibara ya 6(2) (a-j) inaweka misingi ya utawala bora, Ibara ya 28 inataja maadili ya uongozi na utumishi wa umma,ibara ya 29 inaweka kanuni za uongozi wa umma, ibara ya 30 inaweka utii wa miiko ya uongozi wa umma, ibara ya 31 inataja vitendo ambavyo ni marufuku kuvitenda kiongozi wa umma, ibara ya 228 imeundwa Tume ya maadili ya viongozi.


Ibara ya 249 imeunda chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa. Pia katika mihimili yote mitatu ya serikali kila muhimili umewekewa chombo maalum cha kikatiba cha kuhakikisha maadili ya watumishi katika muhimili husika yanasimamiwa. Ibara ya 210 imeweka Tume ya utumishi wa umma, ibara ya 160Tume ya utumishi wa bunge, ibara ya 204 tume ya utumishi wamahakama ambapo miongoni mwa kila Tume katika kila muhimili ni kuhakikisha nidhamu ya watumishi inaimarishwa. Pia ibara ya 208 inaweka misingi mikuu ya utumishi wa umma.


Ibara ya 29(2) (f) bunge limepewa mamlaka ya kutunga sheria itakayoweka utaratibu wa utwaaji wa mali za kiongozi wa umma zinazopatikana kwa kukiuka sheria. Katika ibara 29(2) (b) bunge limepewa mamlaka ya kutunga sheria itakayoweka mashariti kwa viongozi wa umma kufungua akaunti za nje, hii inadhihirisha kwamba suala la ufunguaji wa akaunti za nje kiholela kwa viongozi wa umma halipo tena na limedhibitiwa kikatiba. Kutokana na ukweli huu hoja ya kwamba katiba haijazingatia maadili ya viongozi na watumishi wa umma inatoka wapi? Huo si uzushi?


Nivema ifahamike kwamba Katiba siyo sheria yakufanyia kazi yaani sheria inayotafsiriwa na mahakama, katiba inaweka misingi mikuu ambayo inatungiwa sheria na bunge. Misingi ya maadili imewekwa kwenye katiba inayopendekezwa ambapo bunge kama chombo cha kutunga sheria kimepewa wajibu wa kutunga sheria zitakazo simamia hii misingi iliyomo kwenye katiba.

Kuhusu kuwajibishwa viongozi na watumishi wa umma Zipo hoja kwamba katiba pendekezwa haina meno ya kuwawajibisha viongozi. Dhana ya kuwajibishwa viongozi na watumishi wa umma ifahamike kwamba lazima izingatie misingi ya utawala bora ambao ni utawala wa sheria. kwa mujibu wakatiba hii Kiongozi au mtumishi wa umma anawajibishwa kwa kufuata taratibu na sheria za nchi ambazo pia zinaunda sheria za utawala (Administrative Law) Katiba imeunda Tume mbalimbali ambazo zitakuwa na mamlaka ya kuwawajibisha viongozi nawatumishi wa umma katika kada tofauti za utumishi wao. Utaratibu wa kuwawajibisha viongozi na watumishi wa umma umewekwa vizuri katika katiba hii. Kwa wanaotoa hoja hii labda watwambie kwamba wao wanataka katiba ya kuwakomoa viongozi nawatumishi wa umma.


Katiba nzuri siyo yenye misingi ya kukomoana, ni ile ambayo inaweka na kulinda utawala wa sheria katika nchi. Pia sheria nzuri nizile zinazolinda utu wa watu kwa ujumla wao pamoja na haki za binadamu bila kubagua watu. Hata kiongozi ni mtu nayeye anastahiki kulindwa na sheria za nchi. Hoja hapa ilitakiwa kuangalia kama katiba imejenga misingi ya usawa kati ya wananchi wakawaida pamoja na viongozi katika utoaji wa haki na siyo kutaka katiba inayowaadhibu watu kikatili. Hata wanyama wanahaki zao kwa mujibu wa sheria iweje binadamu asilindwe na sheria? Au mnataka katiba kama ya kikoloni ambayo haikuzingatia misingi yahaki za binadamu?


Kuhusu Rais Kushitakiwa Mahakamani Upo umuhimu na ulazima wa kudhibiti matumizi mabaya ya mamlaka katika nafasi ya Urais kutokana na kwamba ni nafasi kubwa katika utumishi na ina mamlaka makubwa hivyo ikitumiwa vibaya ni rahisi kuleta madhara katika nchi.


Yapo maoni tofauti kuhusiana na suala hili, upo mlengo unaotaka Rais ashitakiwe mahakamani kwa makosa ya ukiukwaji wa katiba baada ya kutoka madarakanin pia wapo wenye mlengo kwamba Rais asishitakiwe. Hoja zote zinamantiki ila ni vema kuwa makini katika kuzichambua hoja hizi zote mbili. Nafasi ya Urais nikubwa sana katika utumishi kutokana na unyeti wa majukumu ya nafasi hiyo.

Pia katika uongozi kuna wakati kiongozi anatakiwa kuchukua maamuzi magumu ambayo kwa upande mwingine yanawaumiza wananchi wake kutokana na sababu mbalimbali. Suingi mkono sana Rais kuwajibika akiwa na fikra za kushitakiwa mahakamani baada ya kutoka madarakani pamoja nakwamba ni ukweli wapo viongozi ambao wanatumia vibaya madaraka yao kwa kutegemea kinga walizonazo kikatiba.

Nirahisi sana Rais kushindwa kuchukua maamuzi mazito kwa manufaa ya nchi na watu wake iwapo kifungu cha kumshitaki Rais kitaingizwa katika katiba ya nchi isipokuwa tu kwa matendo makubwa ya ukiukwaji wahaki za binadamu pamoja na ubadhilifu wa mali za umma hapo ninaunga mkono kifungu cha namna hii kuwemomkatika katiba.


Katika suala zima la kuhakikisha usalama wan chi, raia pamoja na mali zao Rais anaweza kutoa maamuzi kupitia vyombo vya usalama ambayo nikwamaslahi ya nchi ila yakawaathirka wengine hasa wale ambao nichanzo cha uvunjifu wa amani katika nchi, bila shaka maamuzi hayo yaonekana kukiuka haki za binadamu kwa upande ule usiopenda amanimkatika nchi.


Katika wakati huu ambo kuna siasa za vyama vingi kila chama kinahitaji kuchukua madaraka ya kuingoza nchi nirahisi sana wanasiasa kutumia hata mbinu chafu za kuvunja amani ya nchi ili wapate upenyo wa kuendelea au kupata nafasi ya kuiongoza nchi kwa maslahi ya kisiasa, bila shaka katika hali kama hii Rais atachukua maamuzi ya kuhakikisha amani ya nchi haiharibiwi ambapo vyombo vya dola vitalazimika kutumia nguvu ya kuwadhibiti wavunja amani, swali la kujiuliza hapa nikwamba iwapo chama au vyama vilivyoadhibiwa kwa kuvuruga amani ya nchi isipotee pindi vikiingia madarakani vitafanya nini kuhusu Rais aliyekuwepo kipindi hicho? Je, iwapo Rais ataacha kudhibiti uvunjifu wa amani kwa kuogopa kushitakiwa baada ya kutoka madarakani na amani ya nchi ikavurugika hali kwa upande wake itakuwaje baada ya kutoka madarakani?


Kuhusiana na jambo hili maoni yangu nikwamba, Katiba ya nchi iendelee kumpa kinga Rais ya kutoshitakiwa katika mahakama za ndani isipokuwa ashitakiwe katika mahakama za kimataifa kama ilivyosasa ambapo ni rahisi haki kutendeka kuliko mahakama za ndani kwa kuwa katika mahakama za nje siyo rahisi watumishi wa mahakama hizo kuwa na uhasama au woga wa kufanya upendeleo kwa Rais kutokana na kwamba hawaathiriwi na mfumo mzima wa madaraka ya Rais wanchi Fulani kuhusu kupatikana kwao. Nirahisi sana kwa mahakama za ndani kutotenda haki ya mashitaka dhidi ya Rais mstaafu kutokana na aina ya utawala utakaokuwepo kama unamizizi ya Rais mstaafu au ni utawala mpya wa waliokuwa wapinzani.


Falsafa ya mabadiliko ya katiba (sheria) inasema kwamba “ kundi lililoshindwa kuingia madarakani kidemokrasia (lililopoteza kisiasa) ndilo hushinikiza kuwepo mabadiliko makubwa ya kikatiba bila kujali madhara ya mabadiliko hayo ilimradi tu kundi hilo lipate ahueni kisiasa.


Ifahamike kwamba maamuzi mengi anayofanya Rais akiwa madarakani nikwa manufaa ya nchi hata kama yana leta madhara kwa kundi Fulani, nisehemu ndogo sana ya maamuzi ya Rais anayofanya kwa manufaa yake binafsi au kwa chama chake, hii nikwa dunia nzima. Ninasema hivi kutokana na uhalisia kwamba takribani siasa zote duniani zipo katika mifumo inayosimamiwa na vyama vya siasa hivyo siyo rahisi kwa Rais anayetokana na chama Fulani kuacha kabisa kulinda maslahi ya chama anachotoka.

Pia katiba ikiruhusu Rais ashitakiwe ndani ya nchi inaweza kuwa mwanzo wa vurugu na kutoweka kwa amani kutokana na kwamba Rais anatokana na chama ambacho kimsingi kina wafuasi wengi kuliko vyama vingine ambapo ni rahisi wafuasi wachama hicho kuhisi kwamba aliyekuwa kiongozi wao anaonewa hata kama tuhuma hizo zitakuwa nizakweli. Pia utaratibu huu utaondoa heshima ya viongozi wastaafu ndani na nje ya nchi. Mambo mengine hayataki kutumia sana sheria, yanatakiwa kuangaliwa kwa busara pia.


Ni rahisi sana iwapo Chama kinachotawala kikiangushwa na upinzani Rais aliyekuwepo kushitakiwa kwa hila za kukomoana kisiasa na kupelekea amani ya nchi kuvurugika. Ibara ya 96 ya katiba inayopendekezwa inaweka kinga ya mashitaka dhidi ya Rais kwa matendo atakayofanya kwa nafasi ya urais akiwa madarakani na baada ya kuondoka madarakani. Ibara hii iko sahihi nasiyo kwamba katiba imewalinda viongozi kisiasa.

Tunahitaji katiba inayotekelezeka, inayolinda heshima na utu wa watanzania, isiyotoa mwanya wa uonevu na kukomoana, inayowaunganisha watanzania, inayowapa viongozi nguvu na uhuru wa kufanya kazi, isiyotoa nafasi ya kuzuka vurugu, isiyo ya ubaguzi na inayolinda maslahi ya umma. Nafasi ya urais niyapekee katika kuingoza nchi na inahusisha maamuzi mazito katika kuingoza nchi hivyo lazima ilindwe kikatiba. Dhana ya katiba kuwasimamia viongozi isichukuliwe kama dhana ya katiba kuwaadhibu viongozi.

MWANASHERIA.
MWESIGWA ZAIDI SIRAJI.
0784 646220
 
Back
Top Bottom