University of Dodoma (UDOM)
Public Institution
- Feb 24, 2024
- 50
- 55
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Kampuni ya Barrick Gold Corporation zimeanza majadiliano ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati utakaolenga kukuza maendeleo ya sekta ya madini kupitia mafunzo kwa vitendo, tafiti za pamoja na ubadilishanaji wa utaalamu.
Majadiliano hayo yamefanyika leo Mei 5, 2026, katika ukumbi wa Baraza la Chuo UDOM, kufuatia ziara rasmi ya ujumbe wa Barrick ulioongozwa na Rais wa Utafutaji wa Madini Kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati, Nathan Kormanisky. Ujumbe huo ulipokelewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina.
Ushirikiano unaojadiliwa unalenga kuimarisha mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi, kuendesha tafiti za pamoja, pamoja na kutoa huduma za ushauri elekezi katika maeneo mbalimbali ya Sekta ya Madini ikiwemo utafutaji wa madini, ufungaji salama wa migodi, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya teknolojia zinazohusiana na uchimbaji madini.
Wanufaika wakuu wa ushirikiano huo wanatarajiwa kuwa wanafunzi na wahadhiri wa Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi ya UDOM, ambayo imeendelea kuwa kitovu muhimu cha kuzalisha wataalamu wenye mchango mkubwa katika sekta ya madini nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, UDOM ilisisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza ubora wa elimu ya juu na kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Kwa upande wake, Barrick Gold Corporation imeeleza utayari wake wa kuwekeza zaidi katika maendeleo ya rasilimali watu kupitia ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kukuza sekta endelevu ya madini nchini.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uhusiano kati ya elimu ya juu na sekta ya viwanda kwa lengo la kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.