Uchaguzi 2020 UDASA yatoa tamko kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu 2020 kuzingatia Kanuni, Sheria, Katiba

Mathayo Fungo

JF-Expert Member
Nov 13, 2018
319
510
TAREHE: 19 SEPTEMBA 2020

Ndugu Wananchi na Wanahabari, Mnamo Tarehe 26 Agosti 2020, Jumuiya ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) ilitoa tamko ambalo pamoja na mambo mengine lilitoa rai kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu 2020 kuzingatia kanuni, sheria, katiba, na maadili wakati wa kufanya kampeni zao zitakazowawezesha kuchaguliwa hapo tarehe 28/10/2020. Tulifanya hivyo katika kutekeleza wajibu wetu kwa jamii ya Kitanzania.

Ni takribani mwezi mmoja sasa umepita tangu kampeni za uchaguzi zianze mnamo tarehe 26 Agosti 2020. Katika kipindi hiki tumeshuhudia mambo mbalimbali yakiendelea katika kampeni ambayo yanatulazimu kutoa tamko jingine kwa kuwa tunao wajibu kwa jamii nzima ya kitanzania kuhakisha ustawi wa jamii hii.

Tamko hili la leo litajikita kuelezea yale tuliyoyaona kutoka kwa wagombea, wafuasi wa vyama vya siasa, Wananchi wa kawaida na walinda amani na usalama wa nchi yetu yaani polisi na vyombo vingine vinavyofanana nayo.

Kwanza kabisa, moja ya rai tulizozitoa awali ilikuwa ni kuwaasa wagombea kufanya kampeni za kistaarabu, zenye lengo la kunadi sera zao, na siyo lugha za matusi, na kejeli zenye viashiria vya kuchochea machafuko. Hadi hivi sasa tumekwishaona wagombea wa ngazi zote yaani nafai ya Urais, Ubunge na Udiwani wakiwa wamezindua kampeni zao. Jambo la kushtusha ni kuona wagombea hawa wakiwa wanatumia lugha za matusi, kubezana na hata kutishia kwa namna moja au nyingine.

Sisi kama wanataaluma, tunarudia kusema tena, kampeni za aina hii hazikubaliki na hazina tija kwa ustawi wa Taifa letu. Tunawataka wagombea wa ngazi zote kutumia muda wao wote wa kampeni kunadi sera zao na namna ambavyo watazitekeleza pindi watakapopewa hatamu ya uongozi baada ya uchaguzi wa tarehe 28/10/2020. Kufanya tofauti na haya ni uchokozi, uvunjifu wa katiba na uhatarishaji wa amani ya nchi yetu.

Sote tukumbuke kwamba Tanzania ni lazima iendelee kuwepo hata baada ya uchaguzi wa mwezi Oktoba. Lugha za kebehi, vijembe, dharau, dhihaka, ubaguzi, uchochezi hazitatusaidia kujenga mustakabali mwema wa nchi yetu. Vilevile, lugha za aina hii hazisaidii chochote katika kunadi sera. Tunawataka wagombea wote kuwa wastaaratibu si kwa masilahi yao na vyama vyao binafsi bali kwa masilahi mapana ya nchi yetu.

Wagombea waache kabisa ubinafsi na kuangalia kujipatia madaraka kwa nguvu yoyote hata iwe ya kuumiza watu wengine au kuhatarisha amani na usalama wetu. Badala yake wajikite katika kunadi sera za vyama vyao ili waweze kueleweka na kuaminiwa na Wananchi. Wagombea watambue kwamba hawatapigiwa kura kwa uhodari wao wa lugha chafu na zisizo na staha bali kwa kunadi na kueleweka kwa sera za vyama vyao.

Pili tunatoa rai kwa wafuasi wa vyama vya siasa kuwa na ukomavu wa siasa za vyama vingi lakini pia kuwa na ustahimilivu wa kisiasa katika mchakato mzima. Tayari tumesikia katika kampeni za kujinadi kupitia vyombo mbaalimbali vya habari baadhi ya wagombea wamekuwa wakishawishi wafuasi wao waibe vitambulisho vya kura vya wenza, ndugu, jamaa, na marafiki, kama wakiwa wanashabikia vyama tofauti na vyao. Tuseme wazi kabisa kwamba, kwanza hili ni kosa kisheria na halitakiwi kufumbiwa macho. Wafuasi vya vyama vya siasa wajiepushe kabisa kutekeleza maagizo kama haya hata kama anayeyatoa ni mgombea wa ngazi kubwa kiasi gani. Endapo mfuasi wa chama fulani ataamua kufanya hivi, na akitiwa katika mikono ya sheria atafifisha ustawi wa familia yake kwa kutumikia adhabu ya kosa
hilo kisheria.

Wafuasi wa vyama vya siasa wajikite katika kueneza sera na ahadi mbalimbali za vyama vyao husika na siyo kushiriki katika vitendo vyovyote ovu vinavyoweza kutafsiriwa kuwa na jinai ndani yake. Sambamba na hili, tunawasihi wafuasi wa vyama vya siasa kuacha mara moja kufanya vurugu katika kampeni za wagombea wasio wa vyama vyao. Waache kabisa pia tabia ya kuwadhuru wafuasi wa vyama visivyo vyao. Tukumbuke mila na desturi za nchi yetu ni upendo, umoja na mshikamano. Kujihusisha na vitendo kwa mfano vya kuchana mabango ya wagombea wa vyama vingine, kupiga wafuasi wa vyama vingine muda mwingine kwa kutumia silaha hatarishi havileti tija kwa ustawi wa jamii yetu ya kitanzania. Inaondoa utu na thamani yake na mbaya zaidi inajenga chuki miongoni mwa wafuasi wa vyama tofauti vya siasa. Tutambue ya kwamba wakati chuki itaendelea kudumu miongoni mwa wafuasi wa kawaida wa vyama vya siasa, wagombea watamaliza tofauti zao mapema na maisha ya kawaida miongoni mwao yataendelea. Tunasihi wafuasi wa vyama hivi kuwa wastahimilivu na wenye kuchukuliana katika kipindi chote cha kampeni hizi hadi kufikia Uchaguzi Mkuu.

Tatu, tunawasihi wananchi wa kawaida ambao si wafuasi wa vyama vya siasa wala siyp wagombea katika uchaguzi wa mwaka huu kuwa makini na wanasiasa katika kipindi hiki cha kampeni. Tuwapuuze wanasiasa wote wanaojikita katika kutukana, kudharau, kudhihaki, kutoa ahadi ambazo ni za uongo dhahiri na kubeza wagombea wengine badala ya kujikita katika kunadi sera zao. Tunarudia kusisitiza kwamba wananchi na wapiga kura wote jiandaeni kuwapigia kura wagombea ambao mmezielewa sera zao na mmewapima kuona kwamba wanawafaa kuwa viongozi katika maeneo yenu na katika nchi yetu kwa ujumla. Mjiepushe kabisa na wanasiasa pamoja na wafuasi wao ambao badala ya kunadi sera wananadi chuki ubaguzi, matusi na kejeli za aina tofauti tofauti. Tunatoa rai kwa watanzania wote kutojiingiza katika makundi ya siasa zenye uelekeo wa kuchochea chuki, utengano, na uvunjifu wa sheria kwani zinaweza kuliingiza Taifa katika machafuko na kuvuruga amani ya nchi yetu. Tusishabikie kwa namna yoyote vitendo viovu vinavyofanywa na wagombea au wafuasi wao. Tujitenge nao kabisa.

Nne, tunavisihi vyombo vya ulinzi na usalama hasa jeshi la polisi lenye jukumu la msingi na kulinda usalama wa raia na mali zao kuongeza nguvu kidogo katika kipindi hiki.Tunatoa rai kwa vyombo hivi kufanya kazi zao kwa namna ambayo weledi wao unawaongoza na si vinginevyo. Vyombo hivi vifanye kazi kwa haki na usawa kwa wagombea wote na kwa wafuasi wa vyama vya siasa vyote. Hili likifanyika, litaondoa kwa kiasi kikubwa manung’uniko baina ya wagombea wa vyama tofauti na wafuasi wao kwamba kuna baadhi yao wanapendelewa kuliko wengine. Vyombo hivi vya ulinzi na usalama vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha amani na utulivu wa nchi yetu inaendelea kudumishwa wakati wa kampeni, baada ya kampeni na hata baada ya matokeo kutangazwa. Jambo hili halihitaji nguvu kubwa sana kulitekeleza bali linahitaji utendaji wenye haki na usawa tu. Tunawasihi watu wa ulinzi na usalama
kutekeleza kazi zao kwa mujibu wa mila, sheria na kanuni na si kwa misukumo mingine yoyote ile.

Tano, tunavisihi vyama vyote vya siasa vyenye wagombea katika nafasi mbalimbali kuwa mstari wa mbele katika kukemea maovu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi. Kwa mujibu wa katiba yetu vyama vya siasa ndivyo hutoa wagombea na hivyo moja kwa moja vyama hivyo vinawajibika kuhakiksha wagombea wao wanayafanya yale yanayoelekezwa katika sheria za nchi na taratibu za uchaguzi. Ni bahati mbaya sana kwamba tumeshuhudia vyama vya siasa vikitumia muda wao mwingi kutetea wagombea wao hata pale ambapo wamekosea. Hatujapata kusikia hata mara moja vyama vya siasa vikikemea kwa ukali na uwazi wagombea wao waliofanya vurugu, kutoa lugha za matusi, ubaguzi, uchochezi au dhihaka Tunadhani kwamba huu ni udhaifu mkubwa kwa vyama vyote vya siasa kushindwa kutekeleza jukumu lao la msingi kabisa la kuwaongoza wagombea wao.

Mwisho, tunaendelea kuwasihi wadau wote wa mchakato huu wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na utamaduni wetu kama Taifa. Wafanye hivi wakitambua kwa uhakika kwamba kesho yetu kama Taifa ipo mikononi mwao. Ni rahisi kufanya hivi kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, ili wote tuweze kushiriki kwa amani Uchaguzi huu, hapo 28 Oktoba 2020.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
Asanteni

Dkt. George L. Kahangwa
Mwenyekiti wa UDASA
19 Septemba, 2020
Dar es Salaam.
 
Hii ni ngonjera kama ngonjera nyingine zilizotawaliwa na uoga.

Kama wanataalumaa huru mnashindwaje kutoa mifano ya ukiukwaji wa maadili na taratibu?

Mnangoja mpaka mambo yaharibike?

Mnakuwa kama tume inayosema kuna mgombea anayetukana bila kumchukulia hatua wala kuonyesha ni matusi gani ametukana.

Na umemalizia vizuri kwa kuweka namba ya simu, kuna ulazima?
 
Kumbe bora Ardhi University hawajishughulishi na siasa, wao wamebase kwenye academics, scientific research na consultancy sio huu utopolo toka UDSM. Yaani badala ya kudeal na uhuni na engua engua ya tume wanakuja na kitu kama hiki? Kipi kinahatarisha amani na kudhulumu haki ya watu kuchagua viongozi wanaowataka zaidi ya huu upendeleo wa wazi wa tume? Hii kupita bila kupigwa kwa wagombea wa chama kimoja haileti ukakasi kwa wasomi hawa? UDSM ilikuwa enzi zile bwana
 
Hii ni ngonjera kama ngonjera nyingine zilizotawaliwa na uoga.
Kama wanataalumaa huru mnashindwaje kutoa mifano ya ukiukwaji wa maadili na taratibu?
Mnangoja mpaka mambo yaharibike?
Mnakuwa kama tume inayosema kuna mgombea anayetukana bila kumchukulia hatua wala kuonyesha ni matusi gani ametukana.
Na umemalizia vizuri kwa kuweka namba ya simu, kuna ulazima?
Taaluma yao imeshindwa kuelimisha watawala muundo wa tume huru
 
Matamko ya kipuuzi kama haya yanapotolewa na wanaijiita jumuia ya wasomi ndio nazidi kuihurumia elimu yetu, hao wanaohatarisha amani ni wakina nani kama sio wale wanaowaondoa wagombea wa upinzani kwenye chaguzi bila sababu za msingi?
 
Back
Top Bottom