SEERIKALI SIKIVU ILIZIBA MASIKIO MUDA MREFU kuHUSU SAKATA HILI KWANI KUNA MASLAHI YAO:-
=======================================================================================================
Contributions
Mdee, Halima James[CHADEMA]
Kawe Constituency
Session No Seating No Contribution Date Contribution To
4 39 3 August 2011
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 Wizara ya Uchukuzi (Reli, Bandari na Usafiri wa Majini)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kukushukuru, lakini vile vile naomba nichukue fursa hii kusema kwamba hili suala ni letu sote. Hili suala halichagui chama, halichagui kabila na wala halichagui rangi. Kimsingi nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati Wabunge wote waliochangia kwa kutokuunga hoja hii mkono kwa sababu na mimi siungi mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge kutoka Mkoa wa Dar es Salaam. Tunapozungumzia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam nikiwa kama Mbunge wa Jimbo pamoja na Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni Wajumbe. Kwa hiyo, aibu ya UDA ni aibu ya Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wote. Kwa hiyo, ninapozungumza hapa Halima ndivyo ujue anavyozungumza Mheshimiwa Iddi Azzan, ndivyo ujue anavyozungumza Mheshimiwa Zungu na ndivyo ujue anavyozungumza Mheshimiwa Mnyika na wengine wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi haya ya kubariki ufedhuli huu yalifanywa kwa kuvizia wakati sisi hatupo. Sisi ni Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kikaitishwa Kikao cha Kamati ya Uongozi kwa tarehe 29 Juni, 2011 na kikaitishwa kingine cha Baraza tarehe 20 Julai, 2011, sisi tuko huku na mbaya zaidi vikao vyote havina akidi. Ndio maana tunasema kwa hili Meya wa Jiji hawezi kukimbia uwajibikaji hapa, watazunguka wee! Meya hawezi kukimbia uwajibikaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshukuru kwamba hatimaye leo tunazungumza lugha moja. Tarehe 15 Julai, 2011 kama sikosei. Mheshimiwa Mnyika aliuliza swali hapa akai-task Serikali kwa Waziri Mkuu, jamani UDA kuna uchafu huu na huu umefanyika. Serikali inachukua hatua gani, alijibiwa kisiasa. Alijibiwa kwa sababu tu aliangaliwa Mheshimiwa Mnyika anazungumza hakuangaliwa hoja yake. Sasa matokeo yake leo tunafika final maana watu wa Simons wapo wanasema waliitwa na Wizara kuja kutoa inputs zao kuhusiana na Wizara masuala ya uchukuzi na UDA, kwa maana yake wanatambulika na Serikali. Tumefika final kama suala la umeme tunajibizana wee, tukiona huku wananchi wame-react na sisi tunakwenda na upepo wa kisiasa, hatutaendesha nchi hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo mambo ndio yamefika shingoni, tunategemea Waziri kiujanja ujanja atasema hili sio lake ni la Waziri Mkuu ili hotuba yake ipitishwe, lakini Serikali ni hii moja. Kwa hiyo, tusitarajie mtupe majibu ya kupindapinda, hamtoi majibu ya uhakika kwa UDA hakipiti kitu hapa. Hamtoi majibu ya uhakika kwa reli, aibu. Shilingi bilioni sijui 15, sijui 17 rehabilitation. Lakini wakati huo huo Mheshimiwa Mwakyembe, Mwalimu wangu hapa wakati anamjibu Mheshimiwa Machemli kuhusiana na sh. 348,000,000,000/= ambazo mmesema kwenye kile kitabu hamjazichambua kuonyesha zinatumika kwa matumizi gani? Majibu ya Mheshimiwa Mwakyembe anasema fedha hizi ni Special Road Construction Projects kwa ajili ya kama akitokea mtu anataka kujenga ama offer kutoka nje inayotaka Serikali ichangie, hizi ndio fedha zimetengwa mahsusi kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama nilikosea kukupata unaweza ukanirekebisha kwa lugha sahihi. Lakini kama ni fedha ambazo zinasubiri ambazo hata kwenye maandiko yetu ya barabara mbalimbali hazipo lazima tufikirie cha kufanya hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba kama Kambi na tunaamini Wabunge wenzetu wanatuunga. Kama hizi sh. 348,000,000,000/=, tafsiri yake ni maelezo aliyoyatoa wakati akitoa taarifa kwa Mheshimiwa Machemli, tuna kila sababu ya kutoa mafungu kwenye hizi fedha kuboresha bajeti ya Wizara hii. Tuna kila sababu. Lazima tuongezee kwenye nishati, tutoe hapa. Kwa sababu hatuwezi kukaa ku-forecast vitu ambavyo hatuvijui kama vitakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la UDA watu wamewataja watuhumiwa mbalimbali. Kinachonisikitisha na naweza kuwataja kwa majina naogopa kwa sababu nawaheshimu kweli. Kinachonisikitisha ni kwamba kama nchi tumekuwa hatujifunzi kuwapa mamlaka watu ambao sio waaminifu, kwa nini nasema hivyo. Wanaotajwa hapa kipindi kilichopita kwa kashfa hizi hizi ilibidi wajiuzulu. Wanaotajwa hapa ni watu ambao walianzisha Kampuni inayoitwa NICO, Watanzania wakakusanyishwa fedha zao, lakini kinachonisikitisha zaidi tunakoelekea tumesikia Kampuni inaitwa AGRISOL ambayo inatoka Mkoa wa Rukwa kwa Waziri Mkuu ambayo itapora ardhi ya Watanzania isiyopungua hekta laki mbili, hawa jamaa wamo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujifunzi ule mkataba ambao Halmashauri inapewa shilingi mia tano, mia tano na mia mbili, mia mbili wameingia hapo Serengeti sijui Consultants sijui nini, Advisors, fedheha! Kwa hiyo, anaonekana they know how to manipulates, inaonekana wana connection within kwa maana wako protected. Kuna documents zinaonesha kabisa fedha hii imeingia sehemu fulani. Jamani leo Shirika la UDA limekuwa PRIDE. Leo Shirika la UDA limekuwa mtu fulani kwa jina, lakini wanatembea mtaani. Wakati vibaka huko wakikamata kitu hizo hizo fedha shilingi 200/= yuko selo. Sasa naomba Serikali ituambie hawa watu ambao kuna ushahidi wa dhahiri kwamba wameiba fedha zetu za umma wamechukuliwa hatua gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mantiki hiyo hiyo, mimi nilikuwa Mjumbe wa Mashirika ya Umma kipindi kilichopita. Kuna mtazamo kwamba labda maneno yakiwa yanasemwa na mtu fulani hayakai vizuri. Mheshimiwa Zitto alikuwa Mwenyekiti wangu nakumbuka tulizungumza miaka ile miwili na nusu kama 2010, tukasema jamani Serikali yetu ina hisa kwenye Makampuni mbalimbali ambayo ni chini ya asilimia 50 lakini hatuna mamlaka ya kukagua kwa sababu sheria zimeelekezwa tuna mamlaka ya kukagua Makampuni ambayo Serikali ina hisa kiasi gani, chini ya asilimia 50 hatuwezi kuzikagua. Kuna Kampuni kubwa kama BP hebu just imagine utajiri gani uliopo BP, lakini we know nothing. ZAIN we know nothing, Kiwanda cha Urafiki we know nothing. Hii UDA ni cha mtoto, sasa tunasema lini tutajifunza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli tunatoka kwenye madini tumeliwa wee, tunaamka wakati madini yamepotea. Tunakuja kwenye ardhi sasa, ardhi wameshaibariki, Ofisi ya Waziri Mkuu wanafanya mikataba, worst kinyume cha Sheria ya Ardhi inavyotaka mwekezaji mgeni kumiliki ardhi. Hatukomi sasa tumekuja kwenye UDA, watu wamegeuza UDA mali yao binafsi. Sasa niiombe Serikali ilichukulie hili suala kwa mapana yake. Niiombe Serikali yale maagizo na mapendekezo yanayotolewa na Kamati mbalimbali, tulizungumza hapa jamani Wabunge msiingie kwenye Bodi mnakuwa wapole, tukija kusimamia Serikali tunapigwa maneno. Lakini unakuta Wabunge hao hao ambao wako kwenye hizi Bodi hawazisaidii. Kama ni Wajumbe wa Kamati wanakuja ku-lobby kwenu, mnaambiwa jamani eeh Bodi yangu inakuja kaukeni. Hatuendi hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tunaomba tunapoangalia maslahi ya nchi jamani, tuweke maslahi yetu pembeni. Nasikitika kwa sababu kuna lack of seriousness kubwa sana. Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma amezungumza vizuri sana, lakini hapa kuna hii taarifa nadhani ya Serikali ya CHC If, I am not mistaken. Ukurasa wa (4) anasema kabisa "Bodi ya UDA ilikiuka kanuni za Utawala Bora kwa kutowashirikisha wanahisa katika mchakato wa kuuza hisa za UDA na ambazo hazijagawiwa na Simon Group. Hata hivyo, kwa kuwa taratibu zilizokiukwa ni za ndani ya Kampuni internal matters kosa hili halitaathiri kisheria mauzo ya hisa yaliyofanywa kwa Simon Group". Hii ni taarifa ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linasema "Mkataba wa kugawa hisa UDA ingawaje mkataba huu ni halali, ulikuwa haujaanza kutumika kwa sababu masharti yaliyoko katika kifungu fulani ilikuwa bado haijatekelezwa". Wanakiri kwamba mbali na mapungufu mkataba ulikuwa umevunjwa haijakiuka, lakini wanahalalisha kuvunjwa ama kukiukwa kwa mkataba ili Simon Group waendelee kuwa Kampuni. Kitu kibaya kuna barua mbalimbali zinazoonyeshwa kulikuwa kuna mawasiliano kutoka UDA kwa Mwenyekiti kwenda kwa Miundombinu kwenda kwa Wizara ya Fedha na vile vile ikatoka nyingine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda kwa Meneja Mkuu wa Shirika la Usafiri wa UDA. Kila barua inazungumza lugha yake. Kutoka UDA kwenda Wizara ya Fedha inasema tumepata mwekezaji. Kutoka Wizara ya Fedha kwenda Miundombinu wanaambiwa andaeni utaratibu wa kumpa huyu mwekezaji pamoja na hizo annulated shares. Ukitoka huko kwa Waziri Mkuu naye anakuja na lugha yake at least ikawa inatia matumaini, lakini tumechelewa. Lakini Wazungu wanasema it's never too late, nyie ndio watawala. Unapokuwa mtawala maana yake umeshikilia mpini sio, sasa tuonyesheni kwa namna gani mmeshikilia huo mpini mtusaidie kuokoa Shirika letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, wananchi wa Dar es Salaam wajue
Wabunge wao wote tuko against na huu ufisadi na ufedhuli unaofanywa wa kuliuza Shirika la UDA.
Wakiona bajeti hii imepitishwa, wakiona Shirika la UDA limeuzwa wajue ni Serikali imeshindwa kuwasikiliza Wabunge pasipo kujali chama. Ahsanteni sana.
http://parliament.go.tz/index.php/sessions/contribution/1339/2010-2015/41
=======================================================================================================
JE; TUKISEMA KUNAMKONO WA MKUBWA TUTAKOsea??????????????