Uchaguzi unakuja, pombe, pilau, kanga na fulana! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uchaguzi unakuja, pombe, pilau, kanga na fulana!

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Pdidy, Aug 8, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Aug 8, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,132
  Likes Received: 5,571
  Trophy Points: 280
  TUNAHITAJI fikra mbadala katika siasa zetu. Hili ni dhahiri. Nilijaribu kujadili hali halisi ilivyo katika chaguzi zetu na hasa za wabunge. Nikaeleza changamoto na matatizo muhimu yanayotukabili kama taifa.

  Kitu cha msingi ambacho kwa fikra mbadala tunatakiwa kukijadili sasa ni maana ya chaguzi zetu na kama tunaamini ndizo njia ya kutupatia viongozi tunaowastahili na maendeleo tunayoyataka sana.

  Nimejaribu kuonyesha katika udadisi wangu huko nyuma kuwa biashara ya uchaguzi (na ni biashara kweli ukizingatia hongo, fulana, kofia, pilau, pombe, usafiri, n.k. vinavyotawala wakati wa uchaguzi) haiwahakikishii wapigakura kwamba watapata wanachokistahili.

  Katika kampeni, wapiga kura wanapewa ahadi za kitapeli, zikiwamo zisizotekelezeka, au wanapewa fulana, kanga, pombe, pilau, na wao wanampigia kura aliyewanunua. Kinachofanyika leo hakina tofauti na wafanyabiashara ya utumwa kutoka ng'ambo walivyokuwa wakija na kuwapatia machifu na wafanyabiashara wetu shanga, kanzu, kofia, bangili na goroli na wao kupewa binadamu kadhaa kama watumwa.

  Wakati ule; walau bangili iliweza kukaa mkononi miaka kadhaa kuliko fulana ya "chagua fulani" ambayo huwa ni kauka nikuvae na huchakaa ndani ya mwaka au miwili.

  Miaka ya kwanza ya ujenzi wa taifa hili mfumo wa uchaguzi ulilenga kuwapata wawakilishi wa watu. Kama anavyosisitiza Professa Issa Shivji na wanamapinduzi wengine kuhusu jambo hili, wawakilishi wa watu hupatikana kutokana na watu wenyewe na bila kuwepo shinikizo au ushawishi wa rushwa.

  Wawakilishi wa watu hawanyeshi tu kama mvua. Hawashuki tu ghafla kutoka juu na kuwanyeshea watu walio chini na baadaye kuwaacha wakikimbizana kijikinga au kukwepa athari za mafuriko.

  Wawakilishi wa watu ni kama umande. Hainyeshi mvua, hakuna mafuriko, lakini majani yanakuwa na unyevu wake.

  Wawakilishi wa watu unawaona wakiwa na watu wao, wakishirikiana nao, wakisaidiana nao, wakifikiri nao, wakila nao, wakihangaika nao, wakianguka nao na kuamka nao.

  Mfano ninaoutumia sina maana kuwa wawakilishi wa watu ni lazima wawe wanaishi katika nyumba za nyasi kule kijijini na kuendesha maisha yao kama kila mtu pale kijijini. Maana kubwa ya mfano huu ni kwamba wawakilishi wa watu maana yake wanakwenda bungeni kuwakilisha mawazo, changamoto, dukuduku na matarajio ya wale wanaowawakilisha. Lakini pia wanashirikiana na wapigakura wao kukabili changamoto zao pamoja.

  Wawakilishi wa watu wanatakiwa kusikia maumivu wanayoyapata wapiga kura wao na kuchukua hatua za dhati za kuwashirikisha wananchi katika kuyashughulikia.

  Leo hii tunapoelekea katika uchaguzi wa 2,010 hatuna budi kuanzisha na kukuza mijadala itakayowasaidia watu wetu kujua ni nini au nani wanamchagua kuwa kiongozi wao.

  Pamoja na kwamba mijadala hii inawaogopesha baadhi ya watu, njia pekee tuliyo nayo ya kutusaidia kubakia salama kama taifa ni kuhakikisha wananchi wanachukua hatua kama waajiri wakuu wa viongozi hapa nchini kuchagua watu makini na wenye kuitakia heri nchi hii na watu wake wote.

  Nitaeleza kwa ufupi yanayoweza kutokea katika uchaguzi mkuu ujao: Kwanza, wapiga kura wanaweza kuendelea na tabia yao ya kuendekeza tamaa ya vijisenti vya msimu, kanga au fulana. Wanaweza kuendekeza kiu yao ya pombe au soda na njaa ya siku moja wakashiba kwa siku moja na kuchagua kiongozi wa kukaa madarakani miaka mitano.

  Na wapiga kura wetu wanaweza kufanya makosa hayo na kudhani wanaweza kuishi kwa matumaini (kama walivyozoea) hadi uchaguzi mwingine unapokuja wakahongwa tena pilau, pombe, fulana na kanga.

  Wanapofanya hivyo wanakuwa wamehalalisha mambo makuu mawili. Kwanza, wanakuwa wamehalalisha sababu za wao kuonekana majuha kwa sababu hakuna shinikizo la mwakilishi wao kuwajibika ipasavyo.

  La pili, wanakuwa wamehalalisha kuwa na viongozi wanaoweza kuuza nchi na kuwauza hata wapiga kura wenyewe bila wao kujua. Iko hivi. Fursa ya uchaguzi ilikuja kwa wapigakura baada ya miaka mitano. Wao badala ya kuitumia fursa ya uchaguzi kwa umakini na kwa kufikiri vizuri, wakaongozwa na tamaa ya pilau, pombe na vijisenti vya kutumia kwa siku moja au wakahadaika na ahadi hewa.

  Kwa sababu ya kuhadaika, watachagua matapeli, wauza bangi na wenye tamaa ya kujitajirisha wao binafsi. Wakichagua matapeli, basi, wawe tayari kuongozwa kitapeli na wasilalamike. Wajue kuwa wao wenyewe wapiga kura ndio walichagua utapeli.

  Lakini kwa upande wa pili, ni kwamba wapiga kura wa Tanzania wanaweza kuamua kuamka. Wakachukua rungu wanalopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakakaa nalo kipindi cha kampeni hadi siku ya uchaguzi. Wakalitumia kuchagua viongozi kwa umakini wa kipekee. Na ili kujiridhisha kuwa wanachokichagua wanakijua wajiulize maswali yafuatayo:

  Mosi, huyu anayeomba tumchague ni nani? Katokea wapi? Ni mvua au umande? Je historia yake ikoje? Je, ni kwa nini anatuomba tumchague yeye? Je anaahidi nini? Je kinatekelezeka?

  Je, anaamini katika mambo gani kitaifa na ameonyeshaje kuyasimamia kwa dhati hata pale maslahi yake binafsi yalipokuwa hatarini? Je ana msimamo kwa anayoyaamini au ni mtu wa kuyumbayumba kutegemea na maslahi yalipo?

  Pili, huyu anayeomba kura ameifanyia nini nchi yetu au ameufanyia nini ubinadamu kwa ujumla? Je ni wapi na lini katuonyesha kuwa anaweza kuwa kiongozi? Je rekodi yake ya uongozi huko alikotoka ikoje?

  Tatu, huyu anayeomba kura kwetu anatumia njia gani kufanya hivyo? Je anajaribu kutushawishi kwa rekodi yake au na yeye anatutupia vijisenti vya kula leo, fulana, kanga na pilau ili tumchague?

  Je tuna ushahidi gani kuwa huyu anayetuomba kura leo anatuthamini sisi kama watu, kama binadamu, kama wananchi na hatutumii tu kama ngazi ya kupandia kuelekea katika "ulaji" wake binafsi? Je anazifahamu vyema changamoto zetu na jinsi ya kuzikabili au naye pia ana mlolongo tu wa ahadi za kutafutia kura?

  Nne, je ni vigezo gani tutakavyotumia kupima utendaji wake tokea siku ya kwanza tutakapokuwa tumemchagua kuwa kiongozi ili, ikiwezekana, hata kama hajatimiza kipindi chake cha miaka mitano tumuite tumweleze kuwa hatufai na huko anakotupeleka (au asikotupeleka) siko tulikokubaliana kwenda wakati wa uchaguzi?

  Tano, je ni mtu anayejitegemea kimawazo au ni yule tegemezi anayesukumwa na wenye mitaji na maslahi binafsi ili aje agombee ubunge kisha aingie bungeni kutetea maslahi ya waliomtuma?

  Hili la mwisho ni la kujihadhari nalo kupita mengine yote. Leo hii nchi yetu inaelekea pahala ambapo watu wanaweza kutengeneza fedha kupitia ujuha wa wananchi na kisha wakazitumia fedha zile zile kudandia uongozi wa nchi na hatimaye kujihakikishia wao, familia zao na kikundi kidogo wanaendelea kushikilia uchumi na rasilmali za nchi.

  Ujuha wa wapigakura unaweza kutoa uhalali kwa kikundi cha matapeli wachache kuteka nchi halafu kikaanza kuiuza nchi na hatimaye wananchi wenywe. Ipo nchi ya jirani yetu, katika Bahari ya Hindi, ambayo hivi karibuni ilikuwa karibu iuze sehemu kubwa ya ardhi yake kwa nchi moja tajiri eti kwa ajili ya kilimo. Rais wa nchi hiyo alishtuka dakika za mwisho akasitisha uuzwaji ule.

  Huko tunakoelekea, ambako kuna nyang'au wa nje wanaotaka sana kushirikiana na nyang'au wa ndani, tusijeshangaa ikitokea kwamba fedha za kununulia wapigakura wapenda pilau, pombe, kanga na fulana zinapatikana kirahisi na kugawiwa ovyo kwa kila ****. Na baadaye nchi ikajikuta iko rehani au chini ya himaya ya wageni waliotukopesha ili tushinde uchaguzi kwa kununua wapigakura wetu na baadaye tukashindwa kuwalipa.

  Leo hii nchi yetu inashuhudia kujitokeza kwa makundi mbalimbali yanayotoa madai mbalimbali yanayopaswa kushughulikiwa. Mengi ya madai yanayotolewa yana maana na pengine nia nzuri tu. Lakini zipo dalili kwamba baadhi ya madai haya yanaweza kutekwa na matapeli wa kisiasa na wakayatumia katika uchaguzi ujao kuhakikisha wanashinda.

  Na matapeli hao wachache wanaweza hata kuyaombea madai hayo fedha nje ya nchi ili zitumike kununua kura. Ole wao wapiga kura wanaosubiri pilau, pombe, kanga na fulana!
   
 2. MotoYaMbongo

  MotoYaMbongo JF-Expert Member

  #2
  Aug 8, 2009
  Joined: Jan 7, 2008
  Messages: 1,858
  Likes Received: 198
  Trophy Points: 160
  Kwa kweli tunahitaji kufanya kazi ya ziada kuwabadilisha wananchi wa taifa hili. Inaskitisha kwa mfano, unakuta kijana anasema tena kwa kujiamini kabisa bila aibu,"aah mimi sipigi kura mwakani kwa sababu hata nikipiga watashinda CCM". Hili ni tatizo. Yani mtu wa aina hii hajui thamani ya kura yake kuwa inaweza kumng'oa au kumuingiza mtu madarakani. Wengine wanasema eti hata hao wapinzani tukiwapa na wenyewe watakula, yani mawazo muflisi kabisa. Yani mtu anaona ni heri CCM waendelee kula eti kwa sababu hata wapinzani akiwapa na wenyewe watakula. Yani wana JE kazi tunayo na tufanye kazi kwelikweli kila mtu kwa nafasi yake kutoa elimu ya uraia, hawa watu wa-change. MUNGU ibariki Tanzania.
   
 3. Kigogo

  Kigogo JF-Expert Member

  #3
  Aug 8, 2009
  Joined: Dec 14, 2007
  Messages: 20,498
  Likes Received: 1,453
  Trophy Points: 280
  umenifurahisha pilau...walahi mie namchangua mbungee kwa vile ametupa mapilau yakheee
   
Loading...