hebu tuangalie impact ya majina yalioptishwa na wasi wasu\i wa baadhi yao na hali nzima ya uptishaji majina
Homa ya Uchaguzi Mkuu CCM Wanamtandao sasa wahofu kupigiwa kura za chuki
*Kauli ya Kikwete yawachanganya vichwa
*Yapongezwa kuziba ufa ndani ya chama
*Yadaiwa wengine walishaandaa safu zao
http://www.majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=3423
Na Mwandishi Wetu
SIKU chache baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC -CCM) kupitisha majina ya wanachama wanaogombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu ujao Novemba mwaka huu, baadhi wagombea wamekumbwa na kihoro kufuatia msimamo wa chama hicho.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kwamba maamuzi mazito ya kukinusuru chama yaliyofikiwa kwenye vikao vya juu vya CCM, vilivyomalizika hivi karibuni mjini Dodoma na 'kumiminiwa zege' na msimamo Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Jakaya kikwete, kupitia hotuba yake ya Julai kwa Taifa
Akihutubia Taifa muda mfupi baada ya kumalizika Kikao cha NEC mjini Dodoma, Rais Kikwete aliwataka wana CCM kuwakataa viongozi wataojinadi kwamba wametumwa na viongozi wa juu akiwemo yeye, mwenyewe kugombea nafasi hizo.
Rais Kikwete alibainisha kuwa binafsi hajamtuma mwanachama yeyote kugombea uongozi kwa nafasi yoyote na kuwataka wanaCCM kuwakata watakaowarubuni kwa mbinu hizo.
Alisema sifa kubwa kwa wanaogombea ni uwezo na kuzidi kuwatahadharisha wanachama hao kuzingatia hilo kwani wanaowachangua ni wawakilishi wao na hawaendi kumwakilisha yeye( Rais).
Kauli ya Rais Kikwete ilikuja siku chache baada ya Kamati Kuu ya CCM (CC) kupitisha maamuzi mazito zikiwemo taarifa za kupigwa marufuku kundi la wanamtandano ndani ya chama hicho ili kukinusuru chama .
Kundi la wanamtandano lilibuka na kujipatia umaarufu mkubwa ndani ya siasa za CCM baada ya kuongoza mapambano kwenye mchakato wa kinyang'anyiro cha mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Mei mwaka 2005 ambapo Rais Kikwete, aliibuka kidedea akiwabwaga wagombea wenzake 10 wa nafasi hiyo.
Baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2005 na mgombea wa CCM Rais Kikwete kushinda kwa kishindo dhidi ya wagombea wa vyama vingine, wanamtandao waliuona ushindi huo ni neema na pepo ya kisiasa kwao na kujenga dhana ya kuwaona wanaCCM wengine, 'wapangaji wao wenye nyumba.'
Dhana hiyo iliyowafanya baadhi ya wanachama, kutumia ukaribu wao na viongozi wa juu wa chama, kusaka maslahi zaidi ya uongozi ndani ya CCM na serikalini kwa kigezo kwamba ni washirika wa karibu wa viongozi.
Muda na wakati vilibainisha tishio la mshikamano ndani ya chama kutokana na dhana hiyo na kuchukuliwa hatua ya haraka za kusambaratishwa kundi hilo huku Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete 'akipigilia msumari wa mwisho' kwa kubainisha kuwa hakuna aliyemtuma kugombea uongozi na yeyote atakayesema hiyo wananchi wajue kuwa ni mwongo.
Baada ya vikao vya Dodoma, wanachama waliokuwa na dhana ya mtandao wamekumbwa na dhoruba nzito bila kujua pa kukamata hatua inayoelezwa kuwa imewachanganya wengi kisiasa.
Uchunguzi wa Majira umebani kuwa baadhi ya wanachama waliokuwa kwenye kundi hilo sasa wanahaha kutafuta namna nyingine ya 'kuelea' ndani ya chama baada 'nembo' ya uanamtandao kupoteza thamani yake huku wakiogopa kupigiwa kura za chuki na kukosa nafasi walizoomba.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti juzi baadhi ya wanachama, walisema kuwa Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete amewafumbua macho kwani tayari baadhi ya watu waliokuwa kwenye kundi hilo walikuwa wanaendesha kampeni kwa mwavuli wa wanamtandao na wengine wakitamba kuwa wameagizwa na kiongozi wa juu wa chama kuogombea ili wamsaidie majukumu yake.
Imeelezwa kuwa baadhi ya vigogo ndani ya chama na Serikali ndani ya chama hicho wamekuwa wakilikumbatia na kulienzi kundi la mtandao kwa maslahi yao binafsi.
Vyanzo vyetu vya habari vimedai kuwa wanachama hao wamekuwa wakitumia mtandao huo kupanga safu kwa maslahi ya kisiasa ndani ya chama hicho kikongwe na chenye mtandao mkubwa zaidi nchini.
Baadhi ya viongozi hao wanadaiwa kuandaa mikakati ya kuwasaidia baadhi ya wanamtandao wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho hususan kuanzia ngazi za wilaya hadi ujumbe wa NEC ili kuandaa mazingira mazuri ya kisiasa.
Mmoja wa wabunge mkoani Dar es Salaam (jina na Jimbo tunalihifadhi ) anadaiwa aliwahi kumtahadharisha mmoja wa vigogo hao kuachana na harakati za kuwasaidia wanamtandao hao na kumtaka asiingilie uchaguzi wa chama mkoani humo.
Wakati baadhi ya wanamtandao wakitafuta 'tawi la kushika' Majira limedokezwa kuwa wapo wengine wanahaha kuandaa mkakati mwingine kulikana kundi hilo kwa kutafuta baraka za wakongwe wachama hicho ili waweze kushinda nafasi walizoomba.
Habari zaidi zinadai kwamba pamoja na kundi hilo kusambaratishwa, baadhi ya wanamtandao sasa wanajaribu kupanga mbinu chafu za kuwachafua na 'kuwazibia' baadhi ya wagombea wanaoonekana tishio ambao hawakuwa kwenye kundi la mtandao kabla ya uchaguzi huo.
Hatua ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Kikwete kukemea makundi ndani ya chama na kuwakana wanaotaka kutumia jina lake kujipatia uongozi, imepongezwa na wana CCM wengi na kuonekana kama zege iliyoziba ufa mkubwa uliokuwa unainyemelea CCM.