Uchaguzi 2010: Zitto, Mbatia wajitosa Ubunge!

Uchaguzi 2010: Zitto, Mbatia wajitosa Ubunge!

Ninatarajia kutangaza rasmi Jimbo nitakalogombea Ubunge mnamo siku ya Jumapili tarehe 28/3/2010.

Naomba ifahamike kuwa bado sijafanya uamuzi rasmi na kwamba uamuzi wangu utazingatia taarifa ya uchunguzi, ushauri wa viongozi wa chama changu (CHADEMA) na matarajio yangu ya kisiasa ya baadae. Ni muhimu kusisitiza kuwa nikiwa Mtanzania nina haki ya kugombea Ubunge mahala popote nchini.

Uamuzi wowote nitakaoutoa utazingatia kwa kiasi kikubwa sana umuhimu wa kujenga mfumo imara wa demokrasia ya vyama vingi na hasa kuwa na Bunge imara lenye wabunge wengi wa kambi ya upinzani.


(imesainiwa)
ZZK.
1/3/2010

Mh Zitto:

Katika moja ya thread zako hapa JF ulielezea kwamba ungependa kuwa Lecturer kwa siku za usoni. Ukaelezea kwamba unatarajia kuachana na siasa. Katika maelezo yako hapo juu (bold &italic) unaonyesha kwamba unazidi kunogewa na na siasa. Sasa ninakuomba unijibu maswali yafuatayo:

(i) Je! Umebadili vision yako ya kuachana na siasa kwa siku zijazo?
(ii) Kwanini unaamua kuachana na jimbo lako la sasa? Je! Ni njia ya kuepukana na upinzani mkali katika jimbo lako, au unakimbia maswali kutoka kwa wananchi endapo ahadi nyingi ulizozitoa kule haujazitekeleza?
(iii) Ndiyo ni haki yako kugombea ubunge sehemu yoyote, lakini vipi hawa wananchi wa eneo unaloliwakilisha kwa sasa, je! wamekwishafikia kiwango bora cha maendeleo kiasi ambacho unaona uwakilishi wako hauhitajiki?

*****************************************************
Sisimizi anaweza kuua Tembo
 
WAVAMIA MAJIMBO YA KINONDONI NA KAWE


Sadick Mtulya

MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe anatarajia kugombea ubunge katika Jimbo la Kinondoni huku Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia akitarajiwa kugombea Jimbo la Kawe, yote ya jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam viongozi hao walisema wataweka hadharani nia zao za kugombea nafasi hizo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu baada ya wiki mbili.

Zitto aliliambia gazeti hili kuwa mbali na jimbo hilo pia wananchi wa majimbo ya Geita, Kahama, Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini wote wanamuhitaji ili awawakilishe.

"Hadi sasa nimekwishapokea maombi mengi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Kinondoni, Kahama, Geita, Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini ili niwawakilishe bungeni," alisema Zitto.

Hata hivyo, Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema alisema hadi sasa bado hajafanya uamuzi rasmi wa jimbo gani kati ya hayo atakwenda kugombea.

Habari za Zitto kugombea Kinondoni ambako Iddi Azan wa CCM ndiye mbunge huenda zikatoa mshtuko kwa mbunge mwenzake wa Chadema, Suzan Lyimo ambaye pia inadaiwa analiwania jimbo hilo.

Zitto ambaye mwishoni mwa mwaka uliopita alitangaza kuachana na masuala ya siasa ili afanye kazi zake za kitaaluma alisema ameamua kuvunja msimamo wake huo kutokana na maombi ya wananchi kumtaka asiondoke katika medani ya siasa.

"Napenda kuchukua nafasi hii kutangaza kuwa nitagombea katika moja kati ya hayo majimbo ambayo wananchi wameniomba, lakini hadi sasa bado sijafanya uamuzi rasmi. Pia nimeuvunja msimamo wangu wa kujiondoa katika siasa kama nilivyotangaza awali, hii ni kutokana na maombi ya wananchi kutaka nibakie katika medani ya siasa," alisema Zitto.

Zitto alifafanua kwamba uamuzi wa kugombea moja kati ya majimbo hayo utategemeana na utafiti na uchunguzi ambao amekwisha uanza kuufanya kupitia watu wake maalumu pamoja na ushauri kutoka kwa viongozi wa chama chake, ndugu, jamaa na marafiki zake.

"Pamoja na kuhitajika katika majimbo hayo, siwezi kukurupuka na kutangaza tu kuwa nitagombea jimbo hili. Kwanza nimekwishaanza kufanya utafiti na uchunguzi wa kina katika hayo majimbo pia uamuzi wangu utategemeana na ushauri kutoka kwa viongozi wangu wa Chadema, ndugu, marafiki na jamaa zangu," alisema Zitto.

Zitto ambaye amerejea hivi karibuni kutoka nchini Ujerumani alikokuwa akisoma alisema wananchi wa Jimbo la Kinondoni wamemtaka kugombea jimboni humo ili aweze kupata muda mwingi wa kuwasaidia vijana nchini katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo katika siasa.

"Ukweli ni kuwa kugombea katika moja ya majimbo yaliyopo Dar es Salaam ni tofauti na majimbo mengine ya mikoani kutokana na kwamba ukiwa mikoani unahitaji muda mwingi kujipigia kampeni tofauti na Dar es Salaam ambapo anaweza kuwasaidia hata wanasiasa wengine ndani ya Dar es Salaam na mikoani pia," alisema.

Kuhusu jimbo la Geita na Kahama, Zitto alisema wananchi wa majimbo hayo wamemuhitaji kutokana na uwelewa wake wa mambo mengi yanayohusu sekta ya madini.

Katika Jimbo la Kigoma Mjini na la Kaskazini, Zitto alisema ni vigumu kuwaacha wananchi wa huko kutokana na kwamba ndiko alikozaliwa na kwamba wanamuumiza kichwa.

"Jimbo la Kigoma Mjini na lile la Kaskazini, yananiumiza kichwa kutokana na kwamba yote yapo nyumbani nilipozaliwa, lakini natumai uamuzi wangu nitakaoutoa utazingatia mambo muhimu na wananchi watahuheshimu na kukubaliana nami."

Tayari uongozi wa mkoa wa Kigoma, umemega eneo la Mwandiga la Kigoma Kaskazini ambalo Zitto anakubalika na kulipeleka Kigoma Mjini. Eneo hilo lililomegwa linadaiwa kuwa ngome kuu ya Zitto na kwamba hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama sababu ya kuhamia Dar es Salaam.

Naye Mbatia alisema uamuzi wa kugombea katika Jimbo la Kawe unatokana na msingi wa kikatiba na haki ya kila Mtanzania ya kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi zozote.

"Uamuzi wangu umezingatia msingi wa kikatiba na haki ya kila mtu kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi zozote nchini, pamoja na utashi wa kisiasa nilionao," alisema Mbatia na kuongeza;"

"Nimechukua uamuzi huu mgumu kutokana na hali halisi ya mazingira ambayo yanahitaji kuwa na mgombea ambaye ataweza kuleta upinzani mkubwa dhidi ya CCM ili iweze kushindwa."

Kwa sasa Jimbo la Kawe linashikiliwa na mbunge wa CCM, Rita Mlaki. Hata hivyo, mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Halima Mdee alikwisha tangaza kwamba katika uchaguzi wa mwaka huu anawania jimbo hilo.

Mbatia alisema kutokana na mazingira ya Bunge yalivyo yanahitaji wabunge wenye uwezo wa kutoa hoja pamoja na kulishinikiza Bunge liweze kuisimamia na kuiwajibisha serikali vizuri katika masuala nyeti na tete.

"Bunge jipya lijalo linahitaji kuwa na wabunge wenye nguvu na uwezo wa kutoa hoja pamoja na kulishinikiza Bunge liweze kuiwajibisha na kuisimamia ipasavyo serikali katika masuala nyeti na tete ambayo kwa muda mwingi yanaitafuna na kuimaliza nchi," alisema Mbatia Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema ataweka nia hiyo hadharani baada ya wiki mbili kuanzia sasa.

"Wananchi wasiwe na wasi kila kitu kitakuwa bayana baada ya wiki mbili kuanzia sasa ya ama mimi nitagombea au la,"alisema Mbatia ambaye amewahi kuwa mbunge wa Vunjo mwaka 1995-2000.

Mbatia kama mwenyekiti wa NCCR Mageuzi anaungana na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kugombea nafasi ya ubunge.
Mbowe amekwisha tangaza nia ya kugombea katika Jimbo la Hai wakati Mrema anagombea Jimbo la Vunjo.
 
Mwisho wa Zitto kuwa mbunge naona unakaribia. Namshauri tu asithubutu kuja kugombea jimbo lolote Dar es Salaam, atabwaga chini na bungeni hana lake. Politics is a dirty game!!!! Wanamdanganya!!! Mbunge wa sasa ataendelea kutetea kiti chake!!!!

Utafiti utafiti! Wa nini? tumempa sana kichwa huyu kila uchao Zitto.. zitto....., inauma sana hasa ukizingatia wengine tulilaza matumaini yetu kwake na kumwamini kama mbunge kijana. Ni rafiki yangu sana lakini potelea mbali sasa naona anaanza kunikera. Kwanza alianza na kusema hatagombea tena ubunge, tukajadili na kumbembeleza sana akatoa tamko kuwa alikuwa anapima hali ya kisiasa kule Kigoma kaskazini lakini atagombea.
Pili akaja na mpya akidai kuwa Siasa halikuwa chaguo lake, wenye busara tukamanyamaza tukajua kuwa tayari huyu alishalewa umaarufu.
Leo wakati bado tunawaza na kuwazua kazua jingine anadai anataka kugombea mara Kawe, Kahama, Geita na sijui wapi tena, sisi wenye macho yetu tukajua huenda hiyo ni kazi ya CCM.
Jambo moja najiuliza inamaana Zitto kumegwa kwa jimbo hilo kumemtisha kiasi cha kuikimbia Kigoma Kaskazini, au hao wapiga kura 15,000 ambao wanahamishiwa jimbo la Kigoma mjini ndiyo pekee waliokuwa wanamkubali na sasa akigombea atashindwa hivyo anatafuta njia ya kutokea.
Hata hivyo nahiusi kama kutaja maeneo mengine anazunguka sana, kwani Taarifa toka ndani ya CCM zinaeleza kuwa Zitto ameshajengewa nyumba huko Geita (ninafuatilia kujua aliyemjengea) ambayo ilikuwa ikisimamiwa na mmoja wa viongozi wa Chadema aliyetajwa kwa jina la Lyimo na sasa lengo lake ni kugombea Geita hivyo anatafuta njia ya kujibariki kwa utafiti.
Haya kila lakheri lakini hiyo ndiyo sdafari yako ya mwisho kisiasa, ila kwa vile siyo chaguo lako, poa.
 
-Sasa JK anaweza jiskia kwamba upinzani umemgwaya

-Upinzani unaelekeza nguvu zake Bungeni,ukisikia upinzani wa kweli sasa ndiyo huo.Kipindi kijacho kama JK ndiye atakua Rais kitakua kipindi kigumu kuongoza kuliko kipindi chochote alichowahi ongoza Rais yoyote Tanzania
 
Hivi James Mbatia na Halima Mdee kugombea jimbo moja imekaaje? Mbatia nadhani alitakiwa aweke mkkati mzurizaidi...lengo pia ni kuongeza viti vya upinzani bungeni
 
Mimi nitagombea jimbo la bunda kupitia chadema

Karibu sana poti upambane na tyson a.k.a Stephen Wassira Masatu.
Lakini angalia usije kuitwa mvuta bange, tehe...tehe... tehe......!!
Mi najitolea kukusaidia kufanya kampeni, nitakusaidia maeneo ya mugeta hadi mekomalilo.
 
Namwamini sana Zitto Kabwe sio sawa na wanasiasa wa ajabu ajabu maana niliwahi kusema kuwa siasa za Zitto Kabwe ni za kwake pekee na sio watu wengi wanavyo fikiria. Asante sana na Nakutakia kila la kheri kaka yetu
 
Hata akigombea Kinondoni aweza shinda alimradi kuzibiti wale manyangau wa kuiba kura kama walivo mfanyia Mnyika ubungo 2005!
 
Huyu bwana aliwahi kutangaza hapahap ukumbini kwamba anastaafu siasa; nashindwa kuelewa misimamo yake.
 
Zitto alikuwa na nia ya kugombea ubunge katika mojawapo ya majimbo ya mkoa wa Dar es salaam, alitoa sababu eti anataka kuwa mbunge wa kitaifa. Anaamini kwamba akiwa mbunge jijini Dsm atakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuzungumzia masuala ya kitaifa kuliko kuwa mbunge wa Kalinzi ambako muda mwingi anatakiwa kuzungumzia masuala ya jimbo lake zaidi kulio masuala ya kitaifa.
Nadhani umaarufu alioupata baada ya kutimuliwa bungeni kwa kumkomalia Karamagi na issue ya buzwagi ilimfanya apate wazo kwamba anakubalika nchi nzima kwahiyo anaamini kwamba anaweza kugombea jimbo lolote na kuibuka mshindi, kitu ambacho ni chema ingawa kwa tabia za wakazi wa Dar es salaam, asijekushangaa jinsi watakavyomshangaza!!Watu wa dsm hawaaminiki sana, tumeshuhudia jinsi walivyomimina kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana kwa nambari wani!!
Afadhali agombee kigoma mjini angalau kuna uhakika walau asilimia 70 ya kushinda, ukizingatia wapiga kura wake wa mwandiga wamehamishiwa huko.
Lakini kwa kuwa ameunda synovate yake ngoja tusuiri majibu na uamuzi wake hapo tarehe 28 march. Ila awe mwangalifu sana na huo utafiti wa synovate yake. Suala la msigi aangalie mtego wake wa nyumbu usije ukamnasa simba, atabaki kusimulia tu.......!!!!
Mkuu Mwita Maranya, umemaliza kila kitu. Najua unajua Jiji la Dar lilivyogumu.

Ukweli ni kwamba Zitto anatakiwa kuwa makini sana na Jimbo atakalochagua kugombea. Maana uchaguzi huu hautafanyika mara nyingi kiasi kwamba akishindwa katika moja ya majimbo hayo, ataweza kwenda kwingine na kupata ushindi kabla ya mwaka 2015.

Dar es Salaam inawadanganya wengi kuwa ni rahisi kupata ushindi. Ila ukweli unajidhihirisha kila mara kuwa sio rahisi kiasi hicho.
 
Mbunge kijana machachari ambaye aliasisi mapambano dhidi ya kashfa ya Buzwagi miaka kadhaa iliyopita, Zitto Kabwe, ameunda kamati ya watu watatu kusaka jimbo atakalogombea ubunge Oktoba mwaka huu.

Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alitoboa mkakati huo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari aliyotoa jana kupitia jukwaa la wanabidii, hata hivyo hakutaja majina ya watu hao mbali tu ya kusema ni watalaam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mbali na jimbo lake la sasa, Zitto ameelekeza matamanio yake katika majimbo ya Kigoma Mjini (Kigoma), Kahama (Shinyanga), Kinondoni (Dar es Salaam) na Geita (Mwanza).

Jana magazeti kadhaa yanayochapishwa kila siku, yaliandika habari kwamba Zitto atagombea ubunge jimbo la Kinondoni huku Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akielezwa kugombea huko Kawe, yote ya jijini Dar es Salaam.

Kutokana na taarifa hiyo, Zitto alisambaza waraka kwa vyombo vya habari jana, kuelezea kile alichokiita kuwa ni ufafanuzi kuhusu habari hiyo.

Zitto alisema kamati hiyo ni ya uchunguzi (Exploratory Committee) itakayofanya utafiti wa kina kubaini jimbo linalomfaa kwa ajili ya kugombea.

Alisema majimbo aliyoomba yaangaliwe ni pamoja Kigoma Kaskazini, ukiondoa kata ya Mwandiga ambayo imependekezwa kukatwa na kupelekwa Jimbo la Kigoma Mjini.

Alisema Kata ya Mwandiga ina zaidi ya wapiga kura 15, 000 ambao awali walikuwa katika jimbo la Kigoma Kaskazini.

Pia Zitto ambaye amewahi kukaririwa akisema kwamba siasa halikuwa chaguo lake la kwanza akifananisha na kazi ya kufundisha aliyoitamani zaidi, aliyataja majimbo mengine kuwa ni Kigoma Mjini, Kahama, Kinondoni na Geita.

“Nimeelekeza kufanyike utafiti (survey) wa kina ili nitakapofikia kufanya maamuzi, nifanye maamuzi kutokana na taarifa za kutosha,” alisema.

Zitto alisema utafiti huo utafanywa na wanataaluma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao pia watafanya uchambuzi wa hali ya kisiasa na kutoa mapendekezo.

Alisema kwa mujibu wa mpangilio wa kazi, anatarajia kutangaza rasmi jimbo atakalogombea ubunge ifikapo Machi 28, mwaka huu.

“Naomba ifahamike kuwa bado sijafanya uamuzi rasmi na kwamba uamuzi wangu utazingatia taarifa ya uchunguzi, ushauri wa viongozi wa chama changu (Chadema) na matarajio yangu ya kisiasa ya baadaye,” alisema.

Zitto alisema akiwa Mtanzania, ana haki ya kugombea ubunge mahala popote nchini.

“Uamuzi wowote nitakaoutoa utazingatia kwa kiasi kikubwa sana umuhimu wa kujenga mfumo imara wa demokrasia ya vyama vingi na hasa kuwa na Bunge imara lenye wabunge wengi wa kambi ya upinzani,” alisema.

Wakati Zitto akifikia hatua hiyo, watu mbalimbali wametoa maoni tofauti kuhusu uamuzi huo.

Ayoub Kafyulilo akichangia kwa njia ya mtandao, alipinga hatua ya Zitto kufanya utafiti wa jimbo gani agombee.

Kafyulilo alisema kuna hoja ambazo Zitto anastahili kuzifafanua, ikiwa ni pamoja na kama hakuwa na mipango ya muda mrefu katika jimbo la Kigoma Kaskazini analoendelea kuliwakilisha bungeni.

“Au (mipango ya Zitto) ilikuwa inaishia miaka mitano tu, kama ilikuwa ya muda mrefu unafikiri ni nani ataweza kuikamilisha kiusahihi kama ulivyoipanga wewe,” alihoji katika mchango huo kwa Zitto.

Aliendelea, “na kama hukuwa nayo, je, waweza kuwa kiongozi mzuri kiasi gani, kwa nani, nini kinacho kusukuma kutafuta jimbo lingine, unatafuta mahali unapokubalika ili uweze kushinda, au unatafuta mahali ambapo maendeleo yapo duni unataka ukahamasishe maendeleo huko.”

Kafyulilo alisema anaamini kama Zitto alilitumikia kwa uaminifu jimbo la Kigoma Kaskazini kwa miaka mitano, atakuwa amezoeana vema na watendaji na kujua mikakati mizuri ya kuboresha hali zao za maisha.

Naye James Dongwe, alisema anaunga mkono hoja za Kafyulilo kuwa ni miongoni mwa watu wanaotoka Kigoma Kaskazini.

“Zitto nimejifunza mengi kupitia wewe, umefanya mambo makubwa katika national level (ngazi ya kitaifa), lakini ninaona kuna negative impact (matokeo hasi) katika local level (ngazi ya msingi),” alisema katika mchango wake.

Hata hivyo, Zitto alijibu hoja hizo na nyingine akisema hajaamua agombee jimbo gani na kusisitiza anachokifanya utafiti aliouita kuwa ni exploratory work. Zitto alisema baada ya Mwandiga kuelekea kuhamishiwa Kigoma Mjini, kumekuwa na maoni mengi kutoka kwa watu mbalimbali kwamba akagombee ubunge Kigoma Mjini.

Pia alisema wapo waliomshauri abakie Kigoma Kaskazini na wengine walitaka agombee katika majimbo mengine kama Kinondoni.

Alisema jimbo la Kinondoni alilianza kulifikiria tangu mwaka 2005, lakini ikaonekana Kigoma Kaskazini ilikuwa muafaka kwa kugombea.

Zitto alieleza kuwa wakazi wa majimbo ya Geita na Kahama wamekuwa wakimuomba agombee tangu mwaka 2007. “Lakini ni hatari sana kukubali tu maombi ya watu fulani fulani, ni vema kufanya siasa kisayansi, exploration huwa zinatangazwa na baadaye by elimination (kwa kuondoa mengine) unabakia na jimbo moja na sababu za jimbo hilo,” alisema.

Alisema utafiti wa kisiasa anaouita kama political exploration ni mpana kwa mwanasiasa na unatumika zaidi katika nchi zilizoendelea.

“Huku kwetu tumezoea kusema nimeombwa na wazee niende nikagombee, halafu mtu aliyeombwa anaenda anapata kura kiduchu, mpaka unashangaa hao waliomwomba hawakumpa,” alihoji.

Zitto alisema kutokana na hali hiyo, inabidi vijana kubadili siasa na kwamba uamuzi atautoa Machi 28 Machi, mwaka huu katika viwanja vya Mwandiga Sokoni, wilayani Kigoma.

Alisema hatua yake ya kutogombea Kigoma Kaskazini haina maana kuwa Chadema haiwezi kumsimamisha mgombea ubunge.

“Kuna vijana wengi sana wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kuwa wabunge wazuri, kwani nani alinijua mimi kabla sijapewa heshima hii na watu wa Kigoma?” alihoji.

Alisema bado ana imani ya kufanya uamuzi sahihi kuhusu jambo hilo.


CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom