UFAFANUZI KUHUSU MADUDU UCHAGUZI UMEYA KINONDONI NA UBUNGO
Juzi Ijumaa tarehe 21/10/2016 saa 6 usiku tulipata taarifa kupitia Madiwani wetu kuwa muda huo wanasambaziwa barua za kuhudhuria Mkutano Maalum wa Halmashauri ya Kinondoni na Ubungo; barua za Halmashauri zote zilisambazwa muda huo na watu tofauti na zikionesha kuandikwa na wakurugenzi wa Halmashauri za Ubungo na Kinondoni.
Hii ni kinyume cha Kanuni za Kudumu za Halmashauri kwani kwa mujibu wa Kanuni ya 8 (1) inamtaka Mkurugenzi kutoa taarifa ya Mkutano wa Uchaguzi wa Meya au Naibu Meya katika muda usiopungua siku 7. Hapa waliitisha Mkutano kwa ghafla wikendi ili tusiweze kwenda mahakamani kuweka zuio. Pia, Mkurugenzi hana mamlaka ya kuitisha Mkutano Maalum kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 5 wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Meya au theluthi mbili ya wajumbe; Mkutano Maalum hauwezi kuwa wa Uchaguzi wa Meya au Naibu Meya kwa mujibu wa Kanuni.
Kuhamisha Madiwani na Wabunge wa Viti Maalum; Kuna baadhi ya Madiwani na Wabunge wa Viti Maalum wamehamishwa kutoka kwenye Halmashauri ambapo ni wakazi na kupelekwa Halmashauri wasizoishi kinyume na Sheria. Hili limefanyika Makusudi ili kuiongozea wajumbe CCM Kinondoni na Kupunguza wajumbe wa UKAWA. Mathalani; Wabunge wote wa Viti Maalum wa CUF na CHADEMA (Susan Lyimo na Salma Mwassa) walipelekwa Ubungo ilihali wote ni wakazi wa Kinondoni; yaani Susan (Changanyikeni - Kawe) na Salma (Ndugumbi - Kinondoni). Pia, Diwani wa CUF, Layla Madibi alihamishwa, anaishi na aligombea Udiwani 2015 kata ya Mabwepande - Kawe. Wakati haya yakifanyika, Madiwani na Wabunge wa Viti Maalum CCM wamehamishwa kutoka Ubungo kwenda kuongeza idadi Kinondoni. Mfano; Naibu Spika, Dr.Tulia Ackson anaishi Mbezi Makabe ambayo ni Manispaa ya Ubungo. Pia, Diwani wa Viti Maalum CCM, Frolence Masunga anayeishi kata ya Saranga ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Mfuko wa Mbunge wa Jimbo la Kibamba Halmashauri ya Ubungo,naye amehamishiwa Kinondoni katika mchakato wa Umeya.
Kuongezwa kwa jina jipya, limeongezwa jina la Dr. Joyce Ndalichako katika Halmashauri ya Kinondoni ambaye hajawahi kuwa mjumbe wa Baraza hilo.
Madiwani kutotambulishwa kwenye Halmashauri yoyote, Diwani wa Viti Maalum wa CHADEMA anayeishi Kawe Manispaa ya Kinondoni ambaye pia ni Katibu wa Madiwani wa Kinondoni, Caroline Kazinza hakupewa barua ya Mkutano huu wa Uchaguzi kutoka Halmashauri yoyote kati ya hizi mbili na hata alipofuatilia kwa Mkurugenzi alielezwa kuwa si mjumbe na hivyo hawezi kupewa barua. UHUNI UHUNI UHUNI!
Awali idadi ya Madiwani wote kwa kuzingatia makazi na michakato yao ilikoanzia ilikuwa 36;yaani UKAWA 20 na CCM 16 lakini baada ya Uchakachuzi huu ikawa, UKAWA 16 na CCM 18. UHUNI UHUNI UHUNI!
Baada ya kuyaona hayo na mengine mengi, Madiwani wa UKAWA wa Halmashauri zote mbili waliandika barua, kuisaini na kuiwasilisha kwa wakurugenzi mapema leo asubuhi kwa kuwa jana Jumamosi Ofisi za wakurugenzi hazikufunguliwa makusudi kabisa. Lengo la barua hizo ilikuwa ni kuzitaka Ofisi za Wakurugenzi kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na baadaye kuitisha Uchaguzi wenye kuzingatia Kanuni na Sheria. Katika Manispaa ya Ubungo barua na ushauri huo ulizingatiwa na kupelekea Uchaguzi kuahirishwa lakini hali ilikuwa tofauti Kinondoni ambako ubabe ulitawala, polisi wenye silaha walitanda kila sehemu, walioruhusiwa kuingia getini ni Madiwani waliopewa barua tu na hata barua ya Madiwani ilipopelekwa ilikataliwa na Uchaguzi uliendelea kibabe.
Ikumbukwe kuwa katika Manispaa zote mbili zenye majimbo manne, CCM haikushinda hata Jimbo moja. Kuna Wabunge watatu wa CHADEMA na Mmoja CUF. Pia, CCM ina Wabunge wawili wa Viti Maalum na wanne wa kuteuliwa; wote wamebakishwa Kinondoni.
Hali kadhalika, Katika Halmashauri ya Ubungo CCM wana Madiwani 2 tu wa kuchaguliwa kati ya kata 14. Hivyo, walikuwa wameikatia tamaa Halmashauri ya Kinondoni na ndiyo maana UHUNI wao wote waliuelekeza Kinondoni.
Tukutane Mahakamani Kesho. .....
Mbusule C.Shillu
Afisa CHADEMA Kanda ya Pwani
Mwenyekiti BAVICHA (M) KINONDONI