CCM WANAJUA NAMBA, HAWAJUI HESABU!!!
Na. Mtatiro J.
Nimerejea jana DSM. Usiku huo huo nimekutana na madiwani wa UKAWA ambao leo watakuwa wanapambana kulinda ushindi wa wananchi wa Oktoba 25 kwa kuhakikisha Mameya na Manaibu Meya wa Manispaa za Ubungo na Kinondoni wanatoka UKAWA.
NAMBA ZIKOJE KINONDONI:
Madiwani wa CCM kwenye Manispaa ya Kinondoni wako 17 (ukimjulisha hadi Dk. Tulia Ackson - mbunge wa kuteuliwa na Rais). Madiwani wa UKAWA kwa Manispaa ya Kinondoni wako 20.
MCHEZO UKOJE KINONDONI:
Kwanza, Mkurugenzi wa Kinondoni (DED) amewaandikia barua Madiwani wanne wa UKAWA na kuwajulisha kuwa wao si wapiga kura wa Manispaa ya Kinondoni, madiwani hao ni pamoja na Salma Mwasa (Mbunge wa CUF) ambaye amepatia Ubunge wake Jimbo la Kawe lililoko Manispaa ya Kinondoni na hata michakato yote ya kupata Ubunge wake imefanyikia Kawe na NEC na Mkurugenzi wanazo nyaraka zote zinazothibitisha kuwa Mwassa ni diwani wa Kinondoni.
Wakati huo huo mhe. Suzan Lyimo (Mbunge wa Viti Maalum Chadema wa Manispaa ya Kinondoni naye amehamishwa kwa nguvu kwa barua akipelekwa Manispaa ya Ubungo). Uhuni anaofanyiwa Lyimo ndio anaofanyiwa Salma Mwassa wa CUF.
Pili, Mkurugenzi (DED) wa Kinondoni amekokotoa upya idadi ya madiwani wa UKAWA na kumuondoa mmoja, kinyume kabisa na sheria. Mkurugenzi anajisahaulisha kwamba, mamlaka yenye majukumu ya kukokotoa idadi ya madiwani au wabunge wa kila chama ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na tume hiyo hufanya hivyo mara baada ya uchaguzi mkuu. Ukokotozi huu mpya wa DED wa Kinondoni ni aibu kuu isiyotekelezeka kisheria, kimantiki na kikanuni.
Tatu, DED wa Kinondoni ameitisha Mkutano wa Uchaguzi ndani ya saa 24 (kwa dharura) huku akiuita Mkutano Maalum. Nimepitia Kanuni za Uendeshaji wa Manispaa na kujiridhisha kuwa Mkutano wa Uchaguzi wa Meya na Naibu Meya hauingii kwenye "mikutano maalum". Huu pia ni uhuni wa karne, DED alipaswa kutoa notisi walau ya siku 7 ili madiwani wajiandae na uchaguzi huu kwa mujibu wa kanuni. Kinyume chake, anazivunja kanuni za Manispaa kwa makusudi kabisa.
Hayo ni baadhi ya masuala yanayoweza kuitwa UHUNI, ambayo nimeyabaini. Yapo mengine kadhaa siwezi kuyataja.
WITO WANGU;
Mwaka jana (2015) wananchi wa DSM walizungumza, tena walizungumza kwa sauti kuu. Manipaa ya Temeke wakasema madiwani wengi watoke CCM, Ilala wakasema ni UKAWA, Kinondoni wakasema ni UKAWA pia. Hakuna maajabu yoyote yatakayobadilisha hali hiyo, hakuna ushindi wa mezani wala kujuana na REFA.
Serikali ya Magufuli isilazimishe mambo yasiyowezekana. Manispaa ya Kinondoni madiwani wengi ni UKAWA, wako 20. Hakuna namna ya leo kuwafanya wawe 16, hakuna atakayekubali. "PUNDA ATAKUFA LAKINI MZIGO UTABAKI" na lazima ushindi wa UKAWA hapa Dar ulindwe kwa gharama yoyote.
Nawatakia kila la heri madiwani wa Manispaa ya Kinondoni, wakalinde na kutetea SAUTI na Maamuzi ya wananchi. 20 ni kubwa kuliko 17, hata mwanangu Alexa anajua hivyo. Upande wa Manispaa ya Ubungo ushindi wa UKAWA hauhujumiki.
Mpenda haki
23 Okt 2016.