Send this article
Tarime: Ni utata mtupu!
2008-10-03 19:22:43
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Licha ya jitihada za Jeshi la Polisi katika kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inaendelea kuwepo wakati wa Kampeni za kuwanadi wagombea wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Mbunge katika Jimbo la Tarime, hali bado imeendelea kuwa tata kutokana na kuongezeka kwa matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani ambapo jana, mama mmoja na wanawe wawili wanadaiwa kupigwa na kumwagiwa pilipili kwenye nyuso zao.
Inadaiwa kuwa mama huyo na wanawe wamepata kipigo na kupakwa pilipili baada ya kuhusishwa na dhihaka ya kitendo cha mbwa mmoja kuonekana mtaani akiwa amevishwa nguo zenye bendera ya chama kimoja cha siasa.
Imedaiwa kuwa tukio hilo limetokea jana , mishale ya saa 9:00 mchana.
Ikadaiwa na mmoja wa mashuhuda kuwa baada ya mbwa huyo kuonekana mitaani, watu wanaodhaniwa kuwa ni makomandoo wa chama kinachohasimiana na kile ambacho bendera yake imevishwa mbwa, wakamkamata mama mwenye mbwa huyo na wanawe kabla ya kuwapeleka porini na kuwasulubu kwa kipigo na kisha kuwasiliba nyuso zao kwa pilipili.
``Kabla ya kuwapiga, mama huyo na wanawe walivuliwa nguo na kumwagiwa pilipili ... inasikitisha sana,`` akasema mmoja wa mashuhuda. Hata hivyo, kiongozi mmoja wa kampeni wa CHADEMA, Bw. Msafiri Mtemelwa, amesema mama huyo na wanawe ni wafuasi wa chama chao na kwamba waliomtendea unyama huo ni watu wanaodhaniwa kuwa ni wa CCM.
Akasema Bw. Mtemelwa kuwa cha kushangaza, baada ya wao kutoa taarifa polisi, mama huyo na wanawe wakafuatwa huko waliko na kushikiliwa polisi badala ya wahusika wa tukio hilo kusakwa.
``Hivi sasa, tupo hapa Polisi tunashughulikia hatma ya mama huyu na wanawe... maana tunashangaa kuwa sisi ndio tuliotoa taarifa zake polisi ili asaidiwe, lakini badala yake yeye na wanae ndio wamekamatwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Liberatus Barow amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo la mbwa kuvishwa sare za CCM.
Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi, Kamanda Barow amesema amepata taafa za tukio hilo na kuwa yuko safarini kutoka Musoma mjini kwenda Tarime kulishughulikia.
``Taarifa ya tukio hilo nimezipata, lakini sina maelezo zaidi na hivi sasa niko njiani kwenda huko kulishughulikia,`` akasema Kamanda Barow.
Aidha Kamanda Barow ameiambia Alasiri kuwa tayari Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini,DCI, Robert Manumba, amewasili mkoani Mara ili kusimamia hali ya usalama.
Akasema pamoja na mambo mengine, DIC Manumba anakwenda kusimamia upelelezi wa sakata la usambazi wa waraka wa uchochezi unaodaiwa kusambazwa na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila.
Katika hatua nyingine, baadhi ya viongozi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya vurugu jimboni humo na kueleza kuwa havifai kwani ni vya hatari.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, CCM, Yusufu Makamba amelalamikia vitendo hivyo, vikiwemo vile vya kuzomewa kwa wagombea na pia viongozi wa chama chake wakati wa mikutano ya kampeni.
Amesema Makamba kuwa vitendo vya kuzomewa kwa viongozi vinaashiria vurugu ambazo zinaungwa mkono na wapinzani wao wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia, CHADEMA.
Hata hivyo alipoulizwa kuwa matukio hayo yanaathiri kwa kiasi gani mbio za chama chake za kulinasa jimbo hilo, Makamba alijibu kwa kifupi: ``Sina cha kusema. ``
Aidha, wakati Katibu huyo wa CCM akimwaga chozi dhidi ya hali ya vurugu ambayo amedai kuwa si njema kwani inazorotesha hali ya amani na utulivu, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe ambaye alikuwa pia jimboni humo, anadaiwa kuwa hadi sasa yuko nje ya nchi.
Imedaiwa kuwa Bw. Zitto yuko nchini Rwanda kwa shughuli za kikazi, kwani ana nyadhifa nyingi zinazomfanya awe akihitajika katika maeneo tofautitofauti.
Akizungumzia jambo hilo, Mwanasheria wa Chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CHADEMA, Bi. Halima Mdee, amesema safari za Zitto haziwezi kuhusishwa moja kwa moja na yale yanayojiri kwenye kampeni za uchaguzi.
Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Bi. Halima amesema Zitto ni kijana jasiri na kuwa hawezi kukimbia kauli ya Mkuu wa wilaya ambaye anajua wazi kuwa hana ubavu wa kuamuru kukamatwa kwake.
``Binafsi namjua Zitto kuwa ni jasiri, ingekuwa ni kukimbia angekimbia wakati ule aliposimamishwa bungeni, lakini nimjuavyo hawezi kukimbia kauli ya mkuu wa wilaya,``akasema Bi. Mdee.
Akasema kilio cha muda mrefu cha vyama vya upinzani kuwa watendaji wanatumia madaraka yao vibaya kwa manufaa ya vyama vyao au wao binafsi kimedhihirika kupitia agizo la mkuu huyo wa wilaya.
``Kwa muda mrefu tumekuwa na kilio chetu juu ya watendaji wa Serikali, Mkuu wa wilaya pale anamuwakilisha rais, lakini inaonyesha kuwa hawezi kutenganisha majukumu yake na siasa, sasa anatumia rungu lake kutaka kumuonea kila anayeona anahatarisha maslahi ya chama chake,`` akadai Bi. Mdee.
SOURCE: Alasiri
My take: wakuu huu ni unyama uliokithiri,hivi kumfanyia mwanamke unyama wa aina hii utavumilika kweli? Hapana sasa inabidi wananchi wamtetee huyo mama wakamtoe kwa nguvu huko polisi maanke kama polisi walishindwa kumkamata mhalifu insteady wakamkamata victim,basi hata wananchi wakivamia kituo cha polisi jeshi hilo litakua limejitakia.Hizi sheria mwitu dawa yake ni civil disobedience full stop!