Wa Ndima
JF-Expert Member
- Aug 13, 2010
- 1,526
- 323
Niliipenda hii hoja, hebu tujadili.
Nimekuwa nikifuatilia mjadala huu juu ya Zanzibar uliosababishwa na marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar. Mawazo mengi yameshatolewa, mengine yakirejea nyuma kwenye historia ya Zanzibar na mengine yakiangalia hali ya kisiasa ilivyo hapa nchini, na mgawanyiko wa kijamii ulivyo huko unguja na kijamii, kuwepo au kutokuwepo kwake.
Mimi nataka nitoe mchango wangu kidogo katika masuala mawili, la kwanza ni dhana zinazotumika/au zilizotumika katika katiba na mjadala huu, na pili historia ya nchi inayoitwa Zanzibar na hii wengi wanaojadili wanaiita Tanganyika. Nianze na dhana: katika mjadala wa marekebisho haya humu JF na kwingineko maneno NCHI, TAIFA, JAMHURI (REPUBLIC), STATE (DOLA) yamekuwa yakitumika. Na wengi wetu tumekuwa tukiyatumia na kuonesha hisia zetu bila kutafakuri mfanano au utofauti wa maana za dhana hizo. Nchi kwa mfano, ni pande la ardhi, lenye mipaka inayotambulika, wenye nchi yao wakaitambua hivyo na majirani zao na walimwengu wengine wakaitambua hivyo. Ukiangalia maana ya dhana hii - pengine tusingekuwa na ubishi sana juu ya Zanzibar kuwa nchi au si nchi - kwa maana hii hapana shaka kuwa Zanzibar ni nchi. Na kwa kuangalia historia, Tanganyika tunayoizumngumzia imekuwa Nchi baada ya ukoloni, kumbuka Berlin Conference, mipaka yake tunayoililia imewekwa na mkoloni. Hapakuwa na Tanganyika kabla ya hapo (wajerumani walipotutawala). Na kama kutawaaliwa na wageni ndio kunatupa nchi, basi Zanzibar imekuwa NCHI awali zaidi ya Tanganyika. Hilo mosi.
Pili, kuna suala la Dola - mamlaka inayotawala katika pande la nchi, mamlaka hiyo ina vyombo vyake ambavyo ni Serikali, Bunge na Mahakama. Sasa tujiulize hapa je Zanzibar ni dola kwa maana hii, tunaweza kubishana pia, lakini kilicho wazi ni kuwa kabla ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar zilikuwa Dola kamili zenye mamlaka katika masuala yote ya ndani na nje ya nchi zao pamoja na suala la Uraia. Baada ya Muungano, kinadharia, Tanganyika iliachia mamlaka yake yote na kuikabidhi dola ya Tanzania, na Zanzibar ilikabidhi baadhi tu ya masuala, yale yanayoitwa ya Muungano (yalikuwa 11 1964 sasa yako 22). Suala la kuachia mamlaka yote au sehemu ni la kawaida katika aina zote za muungano, Mathalani, tukiwa na sarafu moja ya Afrika Mashariki, tutakuwa, kama dola ya Tanzania tumekabidhi baadhi ya mamlaka na maamuzi kuhusu fedha kwa mamlaka ya juu ya Afrika Mashariki (ndio maana kwenye EU baadhi ya nchi kama Uingereza kwa kutaka kubakia na Sarafy yao hawawa sehemu ya Euro japo wao ni wana EU). Hoja yangu hapa ni kuwa hata Zanzibar wanayo dola, japo haina mamlaka juu ya mambo ya siasa za nje, usalama na ulinzi wa nchi, kati yamambo mengine. Utaifa, nayo ni dhana nyingine, Taifa ni kundi kubwa la watu - wenye historia moja, lugha moja, utamaduni mmoja, uchumi mmoja, na pande la ardhi (nchi) yenye mipaka inayotambulika. Mwalimu alitambua kuwa Tanganyika haikuwa bado Taifa ndio maana akaanza juhudi za Ujenzi wa Taifa, ili sote tulio Tanzania tujihisi kuwa tu Watanzania na tujitambue na kujitambulishaa hivyo. Mradi huu umeachwa na watawala wa baada ya Mwalimu na baadhi ya hoja zinazotolewa ni kielelezo cha kutokukamilika kwa mradi wa Ujenzi wa Taifa. Hoja yangu hapa ni kuwa hata Watanganyika, kama Mwalimu alivyokuwa akisema, bado si wamoja kwa maana hiyo ya utaifa. Hebu tuvunje muungano halafu tuone. Rwanda pale ile Genocide ilitokeaje (hili ni suala jengine kabisa japo muhimu kwetu kutafakari). Kuna dhan hii nyingine, ya Republic (Jamhuri), hii ina maana ya utawala ambao msingi wa mamlaka yake ni watu na Mkuu wa Nchi ni Rais wa kuchaguliwa na watu. Dhana hii chimbuko lake ni karne nyingi zilizopita ambapo Ulaya kwa sehemu kubwa iliamua, baada ya mapambano makali, vita na mapinduzi kuachana na utawala wa kifalme (ambapo chimbuko la mamlaka haikuwa watu bali mfalme). Sasa Tanzania, na pengine Zanzibar katika zipo katika hadhi hiyo katika hali halisi. Kweli tunayo Jamhuri Moja ya Muungano wa Tanzania, yenye mamlaka juu ya masuala yote ya iliyokuwa Tanganyika na baadhi ya Zanzibar. Sasa mgogoro uko wapi katika marekebisho haya ya katiba? Kinachojadiliwa ni nini hasa U-Nchi wa Zanzibar, U-jamhuri wake, U-Taifa wake, au U-dola wake? Ni nini haswa kinagomba?
Mara nyingi, katika masuala kama haya watu hutumia 'mtima' na sio akili kufikir, matokeo yake huwa ni kufikia hitimisho zisizo na mantiki ambazo madhara yake huwa yenye gharama kubwa. Rai yangu, marekebisho haya yameleta suala la kutufanya tujadili masuala na mustakabali wa nchi yetu, lakini tukiongozwa na ufahamu usio shaka wa kile tunachokijadili. Vinginevyo tutajikanganya tu.